Wednesday, September 5, 2012

WATOTO WENYE ULEMAVU WALIA NA SERIKALI ARUSHA

NA BERTHA ISMAIL, ARUSHA

Watoto wenye walemavu waishio mkoani Arusha waililia serikali juu ya kuboresha mfumo wa elimu hasa sekondari unaowatenga hali inayowafanya kukata tamaa ya kuthamini elimu.
Akiongea na gazeti hili kilipotembelea shule ya msingi Meru kwa niaba ya wanafunzi wenzake wenye ulemavu wa aina tofauti tofauti Brenda honest mwenye ulemavu wa kutosikia alisema kuwa  mfumo wa elimu hasa wa shule za sekondari haiwajali wala kuthamini walemavu kama wao.

Brenda aliendelea kusema kuwa ingawa wao ni walemavu lakini jamii itambue kuwa ulemavu huo hawakuuchagua hivyo ameiomba serikali na jamii yote kwa ujumla kuwasaidia kwa kuwasapoti katika mambo mbali mbali zitakazowawezesha kujitegemea hapo baadae na siyo kuwa tegemezi siku zote za maisha yao.

Akitolea mfano mambo wanayohitaji kuungwa mkono Brenda alisema kuwa mfumo wa elimu hasa katika shule za sekondari na kuendelea, haijawapa kipaumbele walemavu hasa wa kusikia, kuona, wenye mtindio wa ubongo n.k kwa uboresheji vifaa vya kufundishiwa, walimu maalum kwa ajili yao pamoja na punguzo la ada hali itakayowafanya kupata moyo wa kusoma.

"kutokana na hayo basi, sisi walemavu tunalia na serikali kwa kuendelea kututengenezea mazingira ya sisi tuendelee kuwa watu tegemezi badala ya kujitegemea wenyewe kiuchumi hapo baadaye kwani kuna wenzetu wengi tu wamefundishwa vizuri shuleni hapa walipoenda secondari wakashindwa masomo na kukata tamaa baada ya kuona hawaelewi masomo lakini wanaendelea kusogeza madarasa" alisema Brenda

"Mbali na kuililia serikali kupewa upendeleo wa kielimu, pia sisi walemavu wasichana mashindano mengi ya kitaifa tumekuwa tukishuhudia kwa wenzetu tu lakini sisi hatushirikishwi hali inayotufanya kujiona tumetengwa zaidi hivyo nitumie nafasi hii kuiomba serikali itambue mchango wa walemavu kiuchumi, kijamii, na hata kisiasa pindi tunapopiga kura kuwaweke madarakani"alimalizia Brenda.

Kwa upande wake mwalimu mkuu wa shule hiyo ya msingi Meru, ambaye pia ni mlezi mkuu wa watoto walemavu wawapo shuleni Bwana Mussa Luwambano alisema kuwa katika shule Meru wana watoto 76 wenye ulemavu tafauti tofauti ambapo hafundishwa zaidi ya miaka saba ikilinganishwa na wenzao wasio walemavu.

Akielezea changamoto kubwa wanayokumbana nazo katika kuwawezesha wenye ulemavu kupata elimu itakayowasaidia katika maisha yao hapo baadae katika kujitegemea Luwambano alisema kuwa ni ukosefu wa vifaa vya kufundishia pamoja na usafiri maalum hali ambayowalemavu wamekuwa wakichelewa shule sambamba na baadhi yao kupoteza maisha kwa kugongwa na magari hasa viziwi wasiosikia milio wala honi za magari.

Pia aliongeza kuwa mbali na hilo pia mfumo wa elimu ya walemavu haujajizatiti katika elimu ya sekondari kwa kuwepo na walimu maalum wa kuwafundusha, madarasa, vifaa na hata miundo mbinu kwa ujumla hali inayosababisha baadhi ya watoto kuishia elimu ya msingi na kuendelea kuwa tegemezi kwa zinowazunguka kitendo ambacho ni kikwazo kikubwa kwa uchumi wa nchi yetu.

"Baada ya kuona watoto wengi tunaowafundisha wakifaulu kwenda sekondari hurudi kwa kushindwa masomo, tumeamua kuwajengea chuo cha ufundi ili wamalizapo elimu ya msingi angalau wajiendeleze kiufundi, hivyo serikali hasa halmashauri yetu ya jiji la Arusha , taasisi ,mashirika na watu binafsi wajitokeze kuisaidia chuo hicho kukamilika ili watoto hawa wajiendeleze kiufundi kuliko kubaki mitaani na kuwa ombaomba"Alisema mwalimu Luwambano.

Aidha pia mwalimu Luwambano aliwataka wananchi kutambua kuwa malezi ya watoto ni jukumu kila mmoja wetu bila kujali ni mlemavu au laa hivyo wajitokeze kuwasaidia pindi wawaonapo wamepata shida hasa wakiwa  barabarani wawavushe kuepusha kugongwa na magari.
                       .............           MWISHO 

No comments:

Post a Comment