Thursday, November 16, 2017

WAZIRI AISHAURI SERIKALI JINSI YA KUPINGA RUSHWA KUANZIA NGAZI YA CHINI KABISA

 Na Queen Lema, Arusha

Waziri wa nchi,ofisi ya rais na utumishi George Mkuchika ameishauri wizara ya elimu kutoa elimu dhidi ya mapambano ya rushwa kwa wanafunzi kuanzia shule za msingi hadi chuo kikuu ili kuwawezesha kutambua madhara yanayotokana na rushwa.

Mkuchika aliyasema hayo  alipokuwa akizungumza katika ufunguzi wa mkutano wa nchi za umoja wa Afrika zinazopambana na rushwa unaoendelea jijini hapa

Alisema kuwa endapo kama elimu ya rushwa itaweza kutolewa mashuleni kuanzia ngazi za awali itawezesha kupunguza kasi ya rushwa kwa nchi husika na hivyo taifa husika kupata haki zake za msingi

Aliongeza kuwa watu wengi wanatoa rushwa kwa kushindwa kufahamu haki zao za msingi hivyo elimu hiyo ikitolewa kuqnzia ngazi za chini itapunguza vitendo vya rushwa ambavyo vimekithiri kwa baadhi ya nchi.
Alitolea mfano nchi za Norway na Sweden ambazo zimekuwa zikitoa elimu ya rushwa kuanzia ngazi za chini mpaka vyuo vikuu ambapo imesaidia kila mtu katika nchi hizo  rushwa kuwa adui wao.

Kwa upande wake mkurugenzi wa Takukuru  hapa nchini Valentine Mlowola alisema kuwa kutokana na rushwa kukithiri hapa tanzania wamefanikiwa kuokoa kiasi cha shilingi bilioni 14 kwa kipindi cha mwaka huu ambazo zilikuwa zikitumika kwenye rushwa.

Alidai kuwa kwa sasa rushwa imekuwa tatizo la kimataifa hivyo kupitia mkutano huo wa umoja wa nchi za afrika wataweza kupanga mikakati ya kupunguza tatizo la rushwa katika nchi hizo.

Ameongeza kuwa nchi za afrika hazitaweza kujikwamua kiuchumi bila kumaliza tatizo hilo kutokana na maliasili nyingi zinazopotea kwenye bara hili zimekuwa zikipotea kutokana na rushwa.

Friday, November 3, 2017

WAFANYAKAZI WA EXIM WAHUKUMIWA KIFUNGO CHA MIAKA 27 JELA KWA KOSA LA UTAKATISHAJI NA UHARIBIFU WA NYARAKA


WAFANYAKAZI wa Benki Ya exim waliokuwa wanakabiliwa na makosa 318 ikiwa ni pamoja na kugushi,kuharibu nyaraka,na utakatishaji fedha haramu na wizi wa dola za kimarekani 521,000 wamehukumiwa kifungo cha miaka 27 jela huku wafanyakazi wengine saba wakiachiliwa huru kutokana na mahakama kushindwa kudhibitisha makosa yao


Aidha wafanyakazi hao wamehukumiwa mapema leo kwenye MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha/Arumeru ambapo wamekutwa na hatia mbalimbali kinyume cha sheria.


Akisoma hukumu hiyo kwa zaidi ya masaa 5 kuanzia saa 4.30 asubuhi hadi saa 9.07 Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo Deusdedit Kamugisha aliwataja aliowatia hatiani ni pamoja na mshitakiwa namba mbili Liliani Mgeye{33},Daudi Nhosha{39},Doroth Cjijanja{50},Genes Massawe{32},Christopher Lyimo{34} na DeusdediT Chacha{35}.


Alisema watuhumiwa wengine waliokutwa na makosa ya kugushi nyaraka na kuharibu nyaraka ambao ni pamoja na Nhosha Massawe na lyimo wamehukumiwa kwenda jela miaka minne kila mmoja kwa kosa hilo.

Hakimu Kamugisha aliwataja walioachiwa huru na mahakama baada ya upande wa jamhuri kushindwa kuthibitisha katika ushahidi wao kuwa watuhumiwa hao walitenda makosa hayo ni pamoja na mshitakiwa wa kwanza katika kesi hiyo ambaye alikuwa meneja Mkuu wa  Exim Benki{T} ltd tawi la Arusha Bimel Gondaili.

Wengine ni pamoja na Livingstone Mwakihaba{37} maarufu kwa jina la ‘’stone’’,Joyce Kimaro{36},Evance Kashebo{40},Tutufye Agrey{32},Joseph Neki{30} na mfanyabiashara Gervas Lubuva{54}.

MWISHO WSA








NA WAANDISHI WETU,ARUSHA


KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida mbunge wa jimbo la Arusha mjini Goodbless Lema, amesema kuwa yeye pamoja na chama chake wanatarajia kuwa wapole sana katika chaguzi za madiwani zinazotarajia kufanyika mapema mwezi huu lakini pia watakuwa wa Mwisho kuonewa na kunyimwa haki kwenye chaguzi mbalimbali

lema aliyasema hayo mapema leo kwenye kata ya Murieth iliopo jijini Arusha wakati akimtambulisha rasmi mgombea wa udiwani wa kata hiyo ya Murieth bw Mosses Mollel  ambaye atapeperusha bendera ya chama cha demokrasia na maendeleo

Lema alisema kuwa kusema kuwa wao wanatarajia kuwa wapole haimanishi kuwa watakubali kuibiwa kura au kuteswa kwa namna yoyote bali watatembeza upole pamoja na ustaarabu kama wanavyofanya kwenye kampeni mbalimbali

"sisi tutaongoza kampeni zetu kwa njia ya ustarabu lakini pia tunatarajia hapa Murieth kuwa wamwishio kabisa kuonewa kwa namna yoyote ile na kamwe hatutakubali kudhalilishwa endapo kama upole wetu hautaweza kujidhirisha'aliongeza lema

alisema kuwa mgombea wao amekidhi viwango vyote vya uchaguzi na hivyo basi wanamleta kwennye jamii waweze kumdhibitisha na kumpa nafasi ya kushinda katika uchaguzi ujao

Awali mgombea udiwani wa kata hiyo ya Murtieth kupitia chama cha demokrasia na Maendeleo, Mosses Mollel alisema kuwa wananchi wa kata hiyo wanatakiwa kumchagua na kumpa kura za ndio kwa sababu yeye  ni kiongozi wa wananchi na sio tajiri wa wananchi

Mollel alibainisha kuwa wananchi wanatakiwa waweze kumpitisha kwenye chaguzi hizo kwani anatarajia kufanya mabadiliko makubwa sana ukilinganisha na vipaumbele ambavyo anavyo mpinzani wake kutoka CCM

jamii yatakiwa kuwakumbuka wajane

Jamii kwa kushirikiana na viongozi mbali mbali wameombwa kujitoa kwa hali na mali  kumsaidia mjane aliyeunguliwa na nyumba yake katika kitongoji cha kanisani kata ya  Imbaseny katika halmashauri ya Meru ili kumwezesha aweze kurudia katika hali yake ya kawaida.

Wito huo umetolewa na mhadhiri mwandamizi chuo  kikuu cha  tumaini makumira ambae pia ni mjumbe wa mkutqno mkuu  ccm taifa dr danieli mirisho palangyo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari  mara baada ya kukabidhi misaada ya mabati na mchele kwa mjane huyo aliyeunguliwa na nyumba yake hivi karibuni  katika kitongoji cha imbaseny .

Dr Palangyo amesema kuwa kufuatia janga kubwa alilopata mjane huyo ambae aliunguliwa  na nyumba yake hivi karibuni kutokana na chanzo ambacho hadi sasa hakijajulikana jamii,na viongozi mbali mbali ndani ya wilaya ya arumeru wanapaswa kuungana kwa pamoja na jamaa wanaojitolea kumsaidia mjane huyo ili aweze kujengewa nyumba yake na kuweza kurudi katika hali yake kwani kwa sasa anaishi mazingira magumu sana.

Amedai kuwa akiwa kama kiongozi amewiwa kufika kwa mjane huyo na kuweza kutoa bati 23   pamoja na mchele kg 25   kwani mama huyo pamoja na watoto wake wapo katika hali ngumu ambayo bila michango hataweza kurejea katika hali yake.

Akizungumza mara baada ya kupokea kwa misaada hiyo mjane huyo aliyetambulika kwa majina ya Maria Kimario mkazi wa imbaseny alisema kuwa nyumba yake iliungua tarehe 29 mwezi uliopita na kusababisha kupata hasara ya milioni 16 kwani vifaa vyote viliteketea kwa moto huo huku chanzo cha awali kikiwa bado hakijajulikana kwani alikuwa anatumia umeme unaotokana na Mobisol.

Aidha bi maria aliwaomba wadau mbali mbali kujitokeza na kumsaidia ili aweze kurejea katika hali yake kwani kwa sasa anaishi mazingira magumu pamoja na watoto wake huku akiwa hana chochote ikiwemo nguo,chakula ,na mahala pa kuishi
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha

Jeshi la Polisi mkoani Arusha limeunga mkono juhudi za Umoja wa Boda Boda Jiji la Arusha (UBOJA) za kutaka kuanza kusajili wanachama wake pamoja na vituo vyote kwa njia ya kisasa katika mfumo wa kompyuta kama hatua ya kuweka kumbukumbu itakayosaidia watambulike haraka kwa sura, majina yao, vyombo vyao vya usafiri na maeneo yao wanayoishi kuanzia ngazi ya kata hadi wilaya.

Akizungumzia nia ya kufanya hivyo na namna itakavyotekelezwa jana katika ukumbi wa bwalo la Polisi ulilopo jijini hapa, Mwenyekiti wa UBOJA Bw. Maulid Makongoro alisema kwamba wameamua kufanya hivyo ikiwa ni mkakati wa kuliunga Jeshi la Polisi katika kutokomeza uhalifu.

Bw. Makongoro alieleza ili kufanikisha suala hilo la usajili, kila kituo kitatakiwa kwanza kilipe ada ya mwaka mzima lakini pia kitatakiwa kulipia gharama ya Shilingi 20,000 ambapo wanachama wake bila kujali idadi waliyonayo wote watapigwa picha na taarifa zao zitapelekwa kwa viongozi wa wilaya likiwemo Jeshi la Polisi lakini pia kila mmoja atakuwa na kitambulisho.

“Usajili wa awali ulikuwa wa kibubu bubu kwa mfano baaadhi ya vituo vilikuwa vinamsajili mwanachama bila kumpiga picha lakini kumbukumbu zilikuwa hazifiki ngazi ya juu lakini wa sasa utakuwa wa Kidijitali kwa kuwa ofisi ya UBOJA itakuwa na kumbukumbu hizo kwenye vitabu na kwenye mfumo wa kumbukumbu wa Kompyuta”. Alifafanua Bw. Makongoro.

Alisema wameamua kufanya hivyo ili kuwadhibiti watu wanaofanya uhalifu kwa mgongo wa waendesha boda boda jambo ambalo linaweza kuwaletea taswira ambayo si nzuri machoni mwa watu.

Naye mgeni rasmi wa mkutano huo, Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo alisema kwamba, Jeshi la Polisi linaunga mkono moja kwa moja wazo hilo la UBOJA kwani hatua hiyo itasaidia kudhibiti uhalifu.

Alisema hatua hii inaonyesha nia njema walionao UBOJA kwa Jeshi la Polisi katika kushirikiana na kudhibiti vitendo vya uhalifu katika jiji la Arusha lakini pia mbali ya kuonyesha taswira nzuri kwa jamii itawasaidia kwa usalama wao.

Kamanda Mkumbo alisema kwa hivi sasa ushirikishwaji wa jamii katika kudhibiti uhalifu ni muhimu sana na kuwataka waendelee kuliunga mkono Jeshi hilo kwa kutoa taarifa mbalimbali za uhalifu hasa unaotokea maeneo yao ya kazi.

“Kwa hivi sasa wezi wengi wanapenda kuwatumia kwa kuwakodi waendesha pikipiki; kukagua eneo la kufanya uhalifu lakini pia baada ya kufanya uhalifu wanatoroka kwa pikipiki hivyo ukimgundua mtu wa namna hiyo toa taarifa haraka kwa askari yeyote unayemuamini au kwa viongozi ili tumkamate”. Alisisitiza Kamanda Mkumbo.

Aliwaasa katika utendaji wao wa kazi kutoweka mbele sana pesa bali waangalie uhai wao kwanza hasa wanapoona baadhi ya abiria wanawakodisha kwa pesa nyingi na kuwapeleka maeneo tete hasa usiku kwani wengine hawana nia nzuri.

Kwa upande wake Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoa wa Arusha Mrakibu wa Polisi (SP) Joseph Charles Bukombe, aliwataka wananchi wote wa mkoa huu wafuate sheria za usalama barabarani kwani kwa kufanya hivyo hakuna mtu atakayewakamata.

Mkuu huyo wa Usalama Barabarani alisisitiza suala la kuvaa kofia ngumu “Helmet” kwa dereva na abiria na kusema hatakuwa na msamaha kwa mtu yeyote atakayekaidi hilo awe mtumishi wa serikali au mwendesha pikipiki za abiria na kuongeza kwamba endapo vyombo vya usafiri vitaendeshwa salama basi vitabaki salama na watu watakuwa salama na kutaja kauli mbiu ya mwaka huu ya wiki ya nenda kwa Usalama Barabarani inayosema “ENDESHA SALAMA HATUTAKI AJALI TII SHERIA TUNATAKA KUISHI”.

Mkutano huo uliohudhuriwa na Mkuu wa kitengo cha Polisi Jamii mkoani hapa Mrakibu Msaidizi (ASP) Edith Makweli na msaidizi wake Mkaguzi wa Polisi Shabani Shabani ulihudhuriwa na washiriki 220 toka kanda tano ambao ni viongozi wa kata na vituo vya waendesha pikipiki ambapo Jiji la Arusha linakadiriwa kuwa na jumla ya vituo vya bodoa boda 400.


VIJANA 50 WAPEWA ELIMU YA KUTAMBUA SERA NA FURSA KWENYE JAMII


na mwandishi wetu, Arusha

VIJANA zaidi ya 50 kutoka katika kata tano za jiji la Arusha wamefanikiwa kupewa elimu ya matumizi na fursa za sera mbalimbali za nchi ya Tanzania ili waweze kunufaika na sera zilizopo


Aidha mafunzo hayo yametolewa na asasi ya Intiative for youth(INFOY) kwa kushirikiana na asasi ya the Foundation for civil Society    yameweza kuwanufaisha vijana kutoka katika kata za Sombetini, Elerai, Sinon, Ngarenaro,  pamoja na Sokoni 1huku lengo likiwa ni kujua na kutambua umuhimu wa sera  za nchi
hataivyo mbali na vijana hao  kufanikiwa kufahamu sera za nchi kwa sasa asilimia kubwa ya vijana wa kitanzania hawajui sera na nchi na dunia hali ambayo wakati mwingine inasababisha kukosa fursa mbalimbali

 Akiongea kwenye mafunzo hayomapema jana mratibu wa asasi ya INFOY  Bw Laurent Sabuni  alisema kuwa ukosefu wa elimu ya sera umekuwa ni kikwazo kikubwa sana kwa vijana wa sasa

Sabuni alisema kuwa kutokana na ukosefu wa elimu hiyo ya sera umekuwa sababu mojawapo ya vijana kushindwa kutambua fursa mbalimbali ambazo zipo kwenye jamii hali ambayo inachangia umaskini mkubwa kwenye maisha yao

Aliongeza kuwa kwenye mataifa yalioendelea duniani vijana wake huwa wanakuwa na desturi ya kuchambua na kufuatilia sera zao na za nchi jirani hali ambayo inawafanya waibue mambo mbalimbali kwenye jamii


katika hatua nyingine alibainisha kuwa vijana hao 50 ambao wamefanikiiwa kupewa elimu ya kutambua sera na faida zake pia wataweza kuunda mabaraza mbalimbali ambayo nayo yatalenga kuibua fursa za vijana kwenye jamii

Sabuni alidai kuwa kwa sasa ndani ya mkoa wa Arusha  hakuna mabaraza ya vijana kitu ambacho wakati mwingine vijana wanakosa sehemu ya kujadilia mambo yao kama ilivyo kwenye nchi ambazo zimeendelea barani Afrika.



Alimalizia kwa kusema kuwa vijana sasa wanatakiwa kujumuika kwenye mabaraza ya kata na hata wilaya na kuachana na tabia ya kukwepa vikundi au umoja kwani umoja unaweza kuleta mabadiliko makubwa sana kwa nchi ya Tanzania

MWISHO