Wednesday, February 20, 2013

TANZANIA INAHITAJI NYUMBA MILIONI TATU –NHC


TANZANIA INAHITAJI NYUMBA MILIONI TATU –NHC

Na Queen Lema,Arusha

TANZANIA ina mahitaji ya Nyumba Milioni Tatu ambapo kwa  sasa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limeweka mikakati ya kuhakikisha kila mwaka inajenga nyumba zaidi ya elfu tatu ili kupunguza tatizo hilo hapa Nchini

Hayo yamelezwa na Waziri wa Ardhi,nyumba, na maendeleo ya makazi,Profesa Anna Tibaijuka leo wakati akizundua mradi wa nyumba za makazi katika eneo la Levolosi ambazo zimejengwa chini ya Shirika la nyumba

Tibaijuka alisema kuwa  mahitaji hayo ya nyumba kila mwaka yanaongezeka kwa kiasi cha nyumba laki tatu lakini ongezeko hilo ni lazima liweze kupunguzwa tena kwa haraka sana kwa kubuni aina mbalimbali ya nyumba ambazo zitarahisisha makazi bora na imara

Aliongeza kuwa Hitaji ni kubwa sana la nyumba hapa nchini hivyo jitiada za haraka sana zinahitajika katika kuhakikisha kuwa hata nyumba ambazo zinajengwa ziweze kuwa imara na ziweze kuwasaidia hata zaidi wananchi wa vijiijini ambao mara nyingine wanaonekana kukosa nyumba bora na imara

Alisema kuwa kama Shirika hilo amblo kinaendeshwa lenyewe litaweza kuwa bunifu na kujenga nyumba nyingi zaidi basi litachangia kwa kiwango kikubwa sana ongezeko hilo la nyumba zaidi ya Laki tatu kwa kila mwaka kuweza kupungua na hata baadhi ya miji kuweza kupangika kwa uraisi sana

“Tanzania kwa sasa tunakabiliwa na changamoto hii lakini ni vema sasa Shirika kwa kushirikiana na wadau mbalimbali tukahakikisha kuwa tunasonga mbele zaidi na hata kuangalia jinsi ya kupunguza tatizo hilo ambalo kama halitaaweza kutatuliwa kwa uraisi basi litasababisha madhara kwa kuwa wapo baadhi ya watu ambao watakosa sehemu za kuishi’aliongeza Tibaijuka

Katika hatua nyingine alisema kuwa nao wanasiasa wana nafasi kubwa sana ya kushirikiana na Shirika hilo kwa kuwa bado shirika hilo linakabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile kushindwa kujenga kutokana na Ardhi ambayo inauwza kwa bei ya juu sana lakini kama watasaidiana basi wataweza kutatua changamoto hiyo ambayo nayo inafanya shirika hilo kushindwa kuendelea kujenga nyumba nyingi zaidi

Awali mkurugenzi mkuu wa Shirika hilo Nehemia Mchechu alisema kuwa ili kukabiliana na tatizo hilo la ongezeko la mahitaji ya Nyumba  hapa Nchini Shirika hilo limeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kuwa mpaka 2014 watakuwa tayari wameshajenga nyumba elfu kumi na tano huku kila mwaka wakijenga nyumba elfu tatu

Mbali na hayo alisema kuwa kwa Mkoa wa Arusha wanatarajia kuanza kujenga nyumba za garama nafuu katika wilaya ya Arumeru pamoja na Arusha huku lengo halisi likiwa ni kuhakikisha kuwa mji wa Arusha unaendelea kuboreka zaidi kwenye hadhi za kimataifa na kuachana na ujenzi holela ambao mara nyingine unasababisha ukosefu wa nyumba

MWISHO

WATUMIENI MAAFISA VIJANA MUEPUKANE NA KERO ZA VIJANA MITAANI- DKT FENELA



WATUMIENI MAAFISA VIJANA MUEPUKANE NA KERO ZA VIJANA MITAANI- DKT FENELA

Na Queen Lema, Arusha

WAZIRI  wa habari,michezo na Utamaduni,Dkt Fenela Mkangara amezitaka Halmashauri zote ndani ya mkoa wa Arusha kuhakikisha kuwa zinajiwekea utaratibu wa kuwa na maafisa Vijana kwa kuwa kama wataweza kufanya hivyo basi watachangia kwa kiwango kikubwa sana kuweza kujadili kwa pamoja changamoto mbalimbali ambazo zinawakabili vijana

Zipo Halamshauri ambazo zinakabiliwa na masuala ya changamoto za Vijana lakini hakuna afisa yoyote ambaye  ana uwezo wa kutatua kero za vijana hivyo asilimia kubwa ya vijana wanabaki wakiwa  wanalalamika ovyo juu ya Serikali

Waziri huyo aliyasema hayo Jana Jijini hapa wakati akiongea na viongozi mbalimbali wa Jiji la Arusha akiwemo Mkuu wa Wilaya kuhusiana na maendeleo ya Vijana pamoja na changamoto,utatuzi wake kwa kipindi miaka iliyopita.

Dkt Fenala alisema kuwa endapo kama Hallkmashauri zote za Jiji la Arusha zitaweza kuwatumia vema hao maafisa Vijana basi zitachangia sana maendeleo ya Vijana kwa kuwa asilimia kubwa ya vijana wa sasa wanabaki wakiwa wanalamikia Serikali  kwa kushindwa kuwajua na kuwatambua jambo ambalo si la kweli

Alisema kuwa kupitia Maafisa Vijana hao ambao wataweza kutatua changamoto ikiwa ni pamoja na kuweka mikakati mbalimbali ya vijana lakini kwa kuwa  kwa sasa hakuna maafisa hao basi Halmashauri zinasema kuwa zinawasaidia vijana huku mitaani vijana bado wakiwa wanakabiliwa na changamoto nyingi sana.

“Wizara yangu imeweka mikakati ya kuondoa matatizo ya vijana lakini halmashauri pekee haziwezi hii kazi ni nzito jamani ni lazima mtekeleze ahadi Raisi ya kuwa na maafisa Vijana ambao wataweza kutukusanyia hawa vijana na kisha hata kama tunakitu cha kuwapa tuweze kuwapata kwa ukaribu sana na pia hii itasaidia sana vijana hawa waache kulalamika ovyo:”aliongeza Dkt Fenela

Awali Mkuu wa Wilaya ya Arusha, John Mongela alisema kuwa tatizo kubwa la vijana hasa wa mkoa wa Arusha wanachokitaka kikubwa sana ni Pesa na wala sio mawazo mazuri ya upataji  wa pesa na mitaaji imara hivyo bado asilimia kubwa sana ya Vijana wanabaki wakiwa wanalalamikia Serikali

Mongela alisema kuwa hali hiyo inasababisha vijana kuona kuwa Serikali haiwathamini,lakini bado Jiji la Arusha limeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kuwa inawapa fursa vijana wa mkoa wa Arusha sanjari na kuwaboreshea mazingira mazuri na imara ya kufanyia biashara zao pamoja na shuguli za kila siku.

MWISHO

WATENDAJI WA SACCOS WASIOKUWA NA ELIMU YA MAHESABU CHANZO CHA SACCOS KUFA


Na Queen Lema,Arusha

WATENDAJI WA SACCOS WASIOKUWA NA ELIMU YA MAHESABU CHANZO CHA SACCOS KUFA


IMEELEZWA kuwa kutokana na baadhi ya watendaji pamoja na viongozi wa vyama vya kuweka na kukopa(SACCOS) kukosa eliumu ya mahesabu kumesababisha sana baadhi ya vyama hivyo kushindwa kufikia malengo yake mbalimbali ambayo yamekwa huku pia hali hiyo ikisababisha migogoro

Hayo yameelezwa na Afisa ushirika jiji la Arusha Bw Huruma Kibwendwa wakati akiongea na wanachama wa Saccos ya Balimi ya jijini hapa mapema jana mara baada ya Saccos hiyo kufikia malengo yake mbalimbali

Huruma alisema kuwa kwa sasa ndani ya mkoa wa Arusha tatizo kubwa sana ni ukosefu wa elimu ya mahesabu kwa kuwa viongozi wengi wanaochaguliwa hawana elimu hiyo hivyo kusababisha madhara makubwa sana ndani ya vyama hivyo vya kuweka na kukopa

Alitaja madhara hayo kuwa ni  pamoja na migogoro ya mara kwa mara ambayo wakati mwingine husababisha hata kufa kwa vyama hivyo, huku madhara mengine ni pamoja na kusababisha utoaji wa mikopo ambayo haikidhi vigezo hali ambayo nayo inachangia sana hasara kubwa sana  kwenye mitaji ya vyama hivyo

“haya madhara ni makubwa sana na kwa hali hiyo basi napenda kusema kuwa hawa viongozi wa vyama hivi wanatakiwa kuhakikisha kuwa wanatafuta elimu hii ili kuweza kunusuru vyama vya kuweka na kukopa ndani ya Jiji la Arusha lakini kama watakuwa wanaendesha vyama vyao kwa mazoea kutasababisha kukithiri kwa udanganyifu wa mahesabu ndani ya vyama hivyo” aliongeza Huruma

Akiongelea maendeleo ya Saccos hiyo ya Balimi Mweka hazina wake,Bw Gerald Kazungu alisema kuwa mpaka sasa wamefanikiwa kuwa na mtaji wa kiasi cha Milioni 73 ambapo kwa kipindi cha mwaka huu 2013 wameweza kugawa Gawio la kiasi cha zaidi ya  Milioni nane kwa wanachama wake mara baada ya kutengeneza faida ambayo imetokana na wanachama wake

Huruma alisema kuwa malengo halisi ya Saccos hiyo ni kuhakikisha kuwa wanaendelea kukopesha zaidi wanachama walio wengi zaidi ambapo kama watakuwa na wanachama wengi zaidi basi wataweza kuchangia kwa kiwango kikubwa sana kuokoa wananchi wa Jiji la Arusha dhidi ya Umaskini ambao unatokana na ukosefu wa Mitaji.

Awali Mwenyekiti wa Saccos Hiyo Bw Richard Mugyabuso alisema kuwa pamoja na kuwa wamefanikiwa kupata faida ya zaidi ya Milioni kwa kipindi cha Miaka miwili lakini bado wakopaji walio wengi wanakabiliwa na changamoto ya mautumizi mabaya ya mikopo hali ambayo inafanya wanakopa washindwe kurudisha fedha hizo huku vyama navyo vikiwa vinategemea marejesho kwa ajili ya kujiendeleza

Mugyabuso alisema kuwa wapo baadhi ya wakopaji katika baadhi ya vyama vya kuweka na kukopa wanakopa kwa malengo kama vile kufanya sherehe,kufikiria zaidi maisha ya kifahari,starehe huku hali hiyo ikisababisha kushindwa kulipa hasa wanapotakiwa kulipa,huku hali hiyo ikisababisha shuguli mbalimbali za vyama kukwama kutokana na Mtaji kupungua badala ya kuongezeka.

MWISHO

Tuesday, February 12, 2013

ASKOFU ASHANGAZWA NA MANABII WANAOENDESHA MAISHA YAO KWA KIFAHARI ILIHALI WAUMINI WAO NI MASKINI


ASKOFU ASHANGAZWA NA MANABII WANAOENDESHA MAISHA YAO KWA KIFAHARI ILIHALI WAUMINI WAO NI MASKINI 

Na Bety Alex,ARUSHA

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida askofu wa kanisa la uzima na ufufuo jijini Arusha Stanley Kilima amewataka baadhi ya manabii wa mkoa wa Arusha ambao wanasindikizwa na kulindwa na mapolisi wakiwa barabarani(ESCORT)wakristo wawaogope sana kwa kuwa inadhirisha wazi kuwa wapo kimaslahi zaidi


Kilima aliyasema hayo Jumapili iliyopita wakati akiongea na waumini wa kanisa la uzima na ufufuo lilipo Maua Ungalmtd Jijini hapa ambapo alidai kuwa wapo wakristo ambao wanachekwa na shetani bila kujua kuwa shetani anawacheka

Alisema kuwa kwa sasa wakristo ambao wanakwepa neno la mungu ndio wanaodanganywa kwa kuwa watu wanaojiita ni Manabii wanatumia vibaya hilo jina na kisha wanajisafisha hata kwa majeshi mbalimbali kwa kuomba Escort bila kujua kuwa wanafanya vibaya sana kwa kuwa kama Mungu amewaita basi wasingeitaji Ufahari ambao hauna maana


Pia alisema kuwa kwa sasa wakristo wanapaswa kuwajua na kuwatambua wanaojiiita manabii kwa kuomba hekima kutoka kwa Mungu na kisha kuwachunguza kwa kuwa asilimia kubwa ya wanaojiita wao ni manabii wapo kifedha zaidi ambapo kwa sasa wengi sana wanashindania mambo ya kifahari yakiwemo magari ya kisasa

Aliongeza kuwa hali hiyo ya wakristo kufumba macho na kisha kuwatambua watu hao kama manabii kumbe ni wapenda fedha ndio inayozaa zaidi fedha chafu za nchi pamoja na mateso yasiyoisha ndani ya makanisa kwa kuwa shetani anawacheka badala ya kuwaogopa watu hao kama wana wa mungu


Alimalizia kwa kutoa hata wito kwa viongozi wa makanisa kuhakikisha kuwa kamwe tamaa ya vitu vya misaada haiwangilii kwa kuwa napo kwa sasa wapo baadhi ya watumishi wa Mungu ambao wanakwenda nje ya nchi na kuomba misaada ambayo wakati mwingine si kwa ajili ya utukufu wa Mungu bali ni kwa ajili ya maitaji yao binafsi


MWISHO

TANZANIA YAINGIA KWENYE MAAJABU SABA YA AFRIKA



TANZANIA YAINGIA KWENYE MAAJABU SABA YA AFRIKA

Na Queen Lema,Arusha

TANZANIA kupitia shirika la Hifadhi za Taifa limefanikiwa kuingia katika maajabu saba katika bara la Afrika hali ambayo itafanya Sekta ya utalii hapa nchini iweze kukua na kuimarika sana tofauti na hapo awali.

Akitangaza Vivutio hivyo vitatiu mjini hapa mapema jana Dr Philiph Imler ambaye ni mwanzilishi na raisi wa maajabu saba barani Afrika alisema kuwa Tanzania kwa wakati huu umefanikiwa kupata vivutio vitatu

Alitaja vivutio hivyo kuwa ni Pamoja na Mlima Kilimanjaro,hifadhi ya Serengeti pamoja na bonde la Ngorongoro ambapo vivutio hivyo viliweza kupigiwa kura nyingi sana na hivyo kuvipa ushindi wa hali ya juu kwa pia ndani ya vivutio hivyo kuna maajabu ya aina mbalimbali ambayo hayapatikani popote barani Afrika na duniani kwa ujumla

“leo nina furai kutangaza kuwa Tanzania imeingia ndani ya maajabu saba na hivyo basi hii ni kama changamoto ya kuhakikisha kuwa bado mnaendelea kufanya viendelee kukua na kuinarika zaidi ili hata wakati mwingine muwe na vivutio vingi zaidi’aliongeza Dkt Imler.

Katika hatua Nyingine Waziri mkuu wa Tanzania,Mizengo Kayanza Pinda alisema kuwa bado Nchi za Afrika zinahitaji zaidi kuwekeza zaidi katika masuala ya Utalii ikiwa ni pamoja na kuongeza zaidi jitiada za utalii kwani bado kuna changamoto kubwa sana katika masuala ya utalii.

Pinda aliongeza kuwa endapo kama Nchi hizo zitaweza kufanya hivyo basi Nchi hizo zitakuwa na Vivutio venye maajabu mengi sana duniani hali ambayo nayo itachangia sana kuweza kuimarisha utalii wa ndani na hata wa nje ya nchi husika.

Aliongeza kuwa ndani ya Nchi  ya Tanzania kwa sasa wamejiwekea juhudi za makusudi kuanzia ngazi ya kitaifa ambapo kupitia ngazi mbalimbali wataweza kuharakisha maendeleo ya utalii hususani utalii ili maajabu mbalimbali ya Tanzania yaweze kufahamika duniani.

Awali mkurugenzi wa shirika la hifadhi za Taifa hapa nchini(TANAPA)Alan Kijazi alisema kuwa wanatarajia mapato kuongezeka hasa katika mlima Kilimanjaro,bonde  la Ngorongoro, na hifadhi za Serengeti kwa kuwa vivutio hivyo vimetangazwa rasmi kama vivutio venye maajabu ya kutosha

Kijazi alisema kuwa pamoja na kutangazwa kwa vivutio hivyo lakini bado TANAPA limejiwekea mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kuwa wanaendeleza shuguli za utalii hapa nchini ingawaje bado kuna changamoto kubwa sana kwenye masuala ya utalii wa ndani

MWISHO

TFDA YATEKETEZA BIDHAA ZA MILION SABA HUKU BAADHI YAKE ZIKIWA NI BIDHAA AMBAZO ZINAWAFANYA WANAWAKE WAONEKANE WANENE KUMBE NI UGONJWA

TFDA ARUSHA YATEKEZA BIDHAA ZA MILIONI SABA

Na Queen Lema,Arusha


MAMLAKA ya Chakula na Dawa nchini TFDA, jana imeteketeza tani moja na robo ya Shehena kubwa ya bidhaa mbalimbali zenye thamani ya shilingi milioni 7 ambazo zimekwisha muda wake wa matumizi na zingine hazijasajiliwa na pia hazionyeshi lini muda wake wa matumizi utakwisha.

Akizungumza katika zoezi hilo la kuteketeza biddhaa hizo kwenye Jalala kuu , lililopo eneo la Muriet, halmashauri ya Jiji la Arusha, Meneja wa kanda ya Kaskazini, wa Mamlaka ya Chakula na Dawa, TFDA, ,Damas Matiko, amesema bidhaa hizo zimekamatwa katika msako uliofanyika ndani ya wiki moja katoka maduka ya Vyakula na Super market.jijini Arusha.

Amezitaja bidhaa hizo zilizoteketezwa kuwa ni  Mafuta ya vyakula, Juice, Soda aina ya Pepsi zilizoko kwenye makopo, Majani ya Chai, Dawa za miswaki za Kichina, Sukari, Maji ya Chupa, Unga wa maziwa wa uji wa watoto uliopo kwenye makopo, Vinywaji vikali, (Pombe)

Matiko, amesema kuwa bidhaa hizo hazikidhi viwango vuinavyotakiwa ,hazijasajiliwa na Shirika la Viwango nchini TBS, na zingine zimeandikwa lugha isiyofahamika ,zingine zimeghushiwa tarehe ya mwisho ya kutumika, hivyo zina madhara makubwa kwa watumiaji na pia hazimhakikishii Usalama mlaji.

Amesema zoezi hilo la kukamata bidhaa hizo bandia limefanyika kuanzia Februari 4 hadi February 8 mwaka huu ,ambapo Mamlaka hiyo imelazimika kuendesha msako huo kwenye maduka baada ya kubaini kuwepo kwa bidhaa zisizokuwa na viwango na hivyo kuathiri afya za walaji.


Matiko alitoa wito kwa  wananchi wanaonunua bidhaa zao kwenye maduka makubwa ya kuuza vyakula,{Super market}, kusoma maelezo ya bidhaa wanazonunua ili waelewe muda wa matumizi badala ya kununua kwa haraka na kwenda kutumia wakati mwingine wanaweza kununua bidhaa ambazo muda wake umeshakwisha na zikawa ni madhara kwao.

"wananchi wawapo na mashaka na bidhaa hizo zilizoko kwenye maduka zikiwemo ambazo lugha na maelezo yake hayaeleweki watoe taarifa kwa Mamlaka hiyo ya chakula na dawa TFDA, au Idara ya afya halmashauri ya jiji la Arusha,lengo ni kulinda afyas za walaji" alisisitiza Matiko.


Ameyataja baadhi ya madhara hayo kuwa ni pamoja na kupata magonjwa kama vile Saratan, kuharisha ,maumivu ya tumbo ,kupata mzio unaotokana na kula vyakula vya aina Fulani, wengine hunenepa na kuwa na miili mikubwa mfano kwa wanawake.

Kwa upande wake kaimu afisa afya mkuu wa jiji la Arusha, Alan Sumari, mewataka wafanyabiashara kuingiza nchini bidhaa zenye viwango ili kuepuka hasara ya bidhaa hizo kuteketezwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa TFDA.

Thursday, February 7, 2013

ASKOFU THOMAS WA KKKT LAIZER AFARIKI DUNIA MKOANI ARUSHA

ASKOFU THOMAS WA KKKT LAIZER AFARIKI DUNIA MKOANI ARUSHA

kkkt Askofu Thomas Laizer enzi za uhai wake

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Kaskazini.Askofu Thomas  Laizer amefariki duniaalasiri ya leo katika Hospitali ya Rufaa ya Selelian ya Mjini Arusha.
 
 Jana Februari 6, 2013 Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alimtembelea  na kumjulia hali Askofu Thomas Laizer wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati.
Taarifa zilipasha kuwa Askofu Laizer alilazwa Hospitalini hapo kwa zaidi ya mwezi mmoja, na hakuna daktari wala ndugu aliye tayari kusema ugonjwa unaomsibu.
 
Pinda alikwenda hospitalini hapo jana saa 9 alasiri na kukaa zaidi ya nusu saa, huku waandishi wa habari wakizuiwa kuingia katika chumba alimolazwa cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu.
 
Hata hivyo, baada ya kutoka katika chumba hicho kama ilivyo ada ya viongozi kuzungumzia hali ya mgonjwa, Pinda hakuzungumza na waandishi wa habari na kulikuwa na ulinzi mkali ambapo pia waandishi wa habari walizuiwa kuzungumza naye.