Thursday, September 20, 2012

TANZANIA KUWA MWENYEJI WA MKUTANO WA MAPINDUZI YA KIJANI


na gladness mushi,arusha

TANZANIA inatarajiwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa jukwaa la mapinduzi
ya kijani Afrika utakaofanyika kuanzia septemba 26 hadi septemba 28
mjini Arusha utakaokutanisha viongozi mbali mbali wa kimataifa
ambao watajadili namna ya kuchukua hatua katika kuboresha usalama wa
chakula duniani .

Aidha katika mkutano huo viongozi hao wataweza kujadili sera ya
mapinduzi ya kilimo na uchumi wa Afrika ,njia za kukuza masoko pamoja
na namna ya kubadilisha mfumo wa kilimo.


Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa Rais wa umoja wa
mapinduzi ya kijani Afrika (AGRA) bi Jane Karuku alisema kuwa
mkutano huo ni hatua inayofuata katika kuendeleza bara la Afrika
kupata ufumbuzi katika masuala ya usalama wa chakula.

Karuku alisema kuwa Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo katika
kukuza sekta ya ukuaji wa kilimo inawakilisha uchunguzi uliofanywa
katika wilaya ya kilombero mkoa wa morogoro juu ya njia bora za
kilimo.


Alieleza kuwa uchunguzi huo uliwezesha uzalishaji wa mahindi kwa
wakulima wadogo wa wilaya hiyo kuongezeka kutoka tani 1.5 hadi 4.5 kwa
hekta ,ambapo kwa upande wa mavuno ya mpunga yaliongezeka kutoka tani
2.5 hadi tani 6 hali iliyopelekea Tanzania kupata fursa hii ya kuwa
mwenyeji wa mkutano huo.


Aidha alisema kuwa jukwaa hilo litatoa nafasi ya kujadili namna bora
ya kuendeleza mipango ya uwekezaji wenye tija kwa ajili ya kuongeza
maendeleo ya kilimo barani Afrika pamoja na kujadili namna bora ya
kuunganisha nguvu ya jamii na sekta binafsi katika kuboresha usalama
wa chakula duniani


Aliongeza kuwa jukwaa hilo pia litaweza kujadili na kutafuta njia bora
za kuboresha kilimo barani Afrika na kuwawezesha wakulima wadogo
wadogo kushirikiana na vyama vya ushirika na wadau wengine ambapo
mjadala huo utatoa njia bora za matumizi ya rasilimali na kukabiliana
na changamoto zinazowakabili mamilioni ya wakulima barani Afrika.


“Wakulima wadogo wadogo ni kitovu kwa yale yote tuyafanyayo hivyo
mtazamo wetu ni kuwapatia wakulima wa afrika dhana za kilimo
wanazohitaji ili waweze kukua zaidi na kuongeza kipato chao na
watatuongoza katika kupata mafanikio mazuri”Alisema bi Jane.

No comments:

Post a Comment