Wednesday, July 24, 2013

NYATI WA AJABU AIBUKA NGORONGORO

Na Bety Alex, ngorongoro


Wahifadhi, watafiti na wataalam kadhaa wako katika harakati za kumsaka
Nyati wa ajabu anayedaiwa kuwa na rangi ya maziwa, ambaye hivi
karibuni amekuwa akionekana katika mwambao wa bonde kuu la Ngorongoro
(Kreta), na kusababisha tafrani kubwa.



Kwa mujibu wa mtalaam wa ikolojia katika mamlaka hiyo Patrice Mattay,
uwepo wa nyati (mbogo) huyo wa aina yake hifadhini hapo kumeibua suala
jipya katika utafiti wa wanyama pori kwani hakujawahi kuwepo Nyati
mwenye rangi nyeupe popote duniani.



Kwa kawaida Wanyama wote aina ya nyati huwa na ngozi yenye rangi nyeusi.



Nyati huyo mweupe aligundulika kwa mara ya kwanza na maafisa wa polisi
wanaofanya kazi katika kituo cha polisi kilichopo ndani ya hifadhi
hiyo ambao wanasema mnyama huyo hupita katika maeneo ya kituo hicho
majira ya asubuhi akiwa miongoni mwa Mbogo wengine takribani 20.
Ngorongoro ina nyati wapatao 350.



“Ni kweli hata mimi binafsi nimemshuhudia Nyati huyo mweupe akikatiza
katika sehemu mbalimbali za hifadhi ya Ngorongoro majira ya asubuhi
akiwa katika kundi la mbogo wengine,” alisema Mkuu wa kituo cha
Ngorongoro Afisa wa Polisi JJ Paul.



Hadi sasa ni maaskari wanaofanya doria katika maeneo ya hifadhi hiyo,
hususan nyakati za asubuhi, ndio wanaothibitisha kwa kiwango kikubwa
kumuona Nyati huyo wa ajabu ambaye sasa anatarajiwa kuwa atakuwa
kivutio kipya cha utalii katika Tanzania nchi ambayo ndiyo pekee
duniani mnyama huyo atakuwa anapatikana.



Meneja wa Uhifadhi katika mamlaka ya Ngorongoro, Amiyo T. Amiyo
amesema tayari shirika lake limekwisha tuma askari wake kadhaa kumsaka
Nyati huyo wa ajabu ili kubaini eneo ambalo anapatikana kwa ajili ya
kuwezesha utafiti zaidi.



“Na kwa mtu yeyote mwenye kutuletea taarifa kuhusu Nyati huyo mweupe
zitakazotuwezesha kumpata mnyama huyo basi naye pia atazawadiwa
ipasavyo,” alisema Amiyo.



Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro ndiyo inayoongoza kwa kupata watalii
wengi nchini na kwa mujibu wa Afisa utalii wa shirika hilo, Asantaeli
Melita, zaidi ya wageni 585,000 hutembelea eneo hilo, na hasa Kreta,
kila mwaka. Tanzania kwa ujumla hupata watalii milioni moja kwa mwaka.



Idadi ya wanyamapori walioko Ngorongoro kwa sasa inafikia 300,000
wengi wao wakiwa ndani ya bonde lenyewe huku baadhi, na hasa twiga
wakiishi nje ya kreta.



Mbali na Mbogo wa jabu aliyegunduliwa hivi karibuni, eneo la
Ngorongoro pia lina maajabu mengine kadhaa, ukiwemo kilima cha mchanga
unaotembea bila kusambaratika, idadi kubwa ya Kakakuona, mnyama
anayedaiwa kuwa na uwezo wa kutabiri, pamoja na idadi kubwa ya wanyama
adimu kama Mbwa-mwitu na Faru.

MAAFISA MAENDELEO YA JAMII 120 WAFUNDWA


ZAIDI ya maafisa maendeleo ya jamii 120 wa halmashauri za wilaya na
wakuu wa Vyuo vya maendeleo ya wananchi wapatao 36 katika mikoa
mbalimbali nchini wamepewa mafunzo malumu  yanayohusu haki za watoto
,ikiwemo Uhsai, Ulinzi, Maendeleo  Ushiriki wa bila kubaguliwa ili
waweze kuzilinda na kuhakikisha hakuna mtoto anayenyanyaswa.

Hayo yamo katika hotuba ya mkuu wa mkoa wa ARusha, Madesa Mulongo,
aliyoyatoa hivi karibuni katika maadhmisho ya siku ya mtoto wa afrika
ambazo kimkoa zimeadhimishwa katika kijij cha Kikatiti wilayani
Arumeru.

Ameseema kuwa katika kuhakikisha haki za watoto zinalindwa na
kupatikana tayari wlaya 84 zimeshaunda mabaraza ya watoto ikiwemo jiji
la Arusha, kwa ajili ya kulinda na kusimamia haki mbalimbali za watoto
.

Magesa Mulongo, amesema katika kuhakikisha haki hizo zinapatikana
tayari serikali imeingiza kwenye mitaala ya Vyuo vya maendeleo ya
jamii sanjari na kuwepo kwa sera  ya maendeleo ya mtoto nchini
masuala ya haki za watoto ili kuepuka utumikishwaji  wa watoto kwenye
kazi zenye madhjara katika mazingira hatarishi .

Aidha amesema kuwa katika juhudi hizo za kuhakikisha haki za watoto
zinalindwa zaidi ya watoto 720 mkoani Arusha, waishio kwenye mazingira
 magumu wameondolewa kwa ushirikiano na mashirika yasiyokuwa ya
kiserikali likiwemo shirika la Mkombozi ambalo limeweza  kuondoa
watoto 29 na kuwaunganisha katika mfumo rasmi wa elimu ikiwemo Ufundi

Amesema kuwa watoto 6 wameunganishwa na familia zao ,watoto 8
wameunganikatika familia zao na kupatiwa elimu ya kujitegemea, watoto
20 wamepelekwa kwenye kituo kingine cha Mkombozi kilichopo Moshi
mkoani Kilimanjaro na kuunganishwa kwenye mradi wa bustani 40 sanjari
na kuhudumiwa i  elimu wakiwa katika familia zao

Ameongeza kuwa katika mlolongo huo familia 60 kutoka kata za Unga
limited na Ngarenaro, zimewezeshwa kiuchumi ili ziweze kumudu kulea na
kutunza watoto wao

Amesema kuwa pia Shirika lingine la Action for Children, limeweza
kutoa  elimu  katika shule 12 mbalimbali ambayo inahusu utetezi na
ushawishi ,haki za watoto na kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi
21,  katika halmashauri 3 za Jiji la Arusha, Halmashauri ya Meru, na
Arusha DC.

Amesema kuwa mkoa huo unaendelea na vita dhidi ya dawa za kulevya na
utumikishwaji wa watoto kwenye mazingira hatarishi  kupitia Idara za
maendeleo ya jamii katika halmashauri mbalimbali kwa kushirikiana na
mashirika yasiyokuwa ya kiserikali ambapo elimu ya madhara ya dawa za
kulevya imekuwa ikitolewa .

MSISUBIRI MSIMU WA NANE NANE UFIKE NDIO MUANZE KUWEKA VIPANDO MNAWANYIMA WAKULIMA NA WAFUGAJI HAKI ZAO-MAGESA MULONGO



Halmashauri za kanda ya kaskazini zimetakiwa kujiwekea utaratibu wa
kuweka vipando na mashamba darasa katika viwanja vya maonesho ya
wakulima na wafugaji(TASO)kila wakati na kuachana na tabia ya
kustawisha pamoja na kuweka vipando hivyo mwezi mmoja kabla ya
maonesho hali ambayo wakati mwingine inasababisha maana halisi ya
kilimo kwanza kufa.

Wito huo umetolewa Jana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha,Bw Magesa Mulongo
wakati akiongea na wadau wa kilimo wa chama cha wakulima na wafugaji
kanda ya kaskazini (TASO) kwenye maandalizi ya maonesho hayo
yanayotarajiwa kuanza hivi karibuni

Alisema Halmashauri za kanda ya kaskazini zinakabiliwa na changamoto
hiyo hivyo jitiada mbalimbali bado zinahitajika ili kuweza kuboresha
kilimo kwanza hususani kwenye suala la vipando ambavyo baadhi yake
hufanywa kama mazoea tu

Alizitaja changamoto kubwa ambazo zinafanya halmashauri kupanda
vipando hivyo kwa mazoea ni pamoja na kutojua maana halisi ya chama
hicho pamoja na maonesho kwani asilimia kubw ya watu wanafikiri kuwa
viwanja hivyo vinaweza kutumika kuanzia Agust Moja hadi kumi kwwa kila
mwaka

Mbali na hayo alisema kuwa katika kipindi hiki cha kuelekea katika
maonesho ya wakulima na wafugaji pia kila Halmashauri zinatakiwa
kujituma kwa bidii na kuachana na tabia ya kulalamika kuwa hawajapata
zawadi

Alifafanua kuwa,tabia ya kutojituma ipasavyo na kutotumia mbinu bora
za kilimo kwanza kwa watazamaji ndio inayochangia kwa kiwango kikubwa
Halamashauri zilizokosa zawadi kuona kuwa walionewa na majaji

Akifunga kikao hicho Mwenyekiti wa TASO bw Athur Kitonga alisema kuwa
lengo la chama hicho ni kuendeleza sekta ya Kilimo na wafugaji kwa
kila mwaka lakini Halmashaauri bado hazipeleki wafugaji na wakulima
kujifunza katika mabanda yao mpaka ifike msimu wa maonesho ya Nane
Nane.

MWISHO

NGORONGORO YATOA MICHE LAKI TATU KWA AJILI YA SHULE ZA SEKONDARI NA MSINGI



Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro (NCAA)imetoa miche ya miti laki tatu
kwa shule za Sekondari na Msingi ambazo zinapakana na Mamlaka hiyo
huku lengo halisi likiwa ni kuwafundisha wanafunzi umuhimu wa misitu
pamoja na kuhifadhi mazingira

Akiongea na waandishi wa habari mwisho wa wiki Afisa Misitu wa mamlaka
hiyo ambaye Ni Bw Naaman Naaman alisema kuwa huo ni mpango mojawapo wa
mamalaka hiyo wa kuhakikisha kuwa wanafunzi wanakuwa na elimu ya
misitu ili wawe mabalozi wazuri wa mazingira

Bw Naaman alisema kuwa mradi huo wa kutoa miche ya miti ambayo ni ya
matunda, mbao, na vivuli ulianza rasmi mwaka 2009 na mpaka sasa baadhi
ya shule za sekondari na msingi zimeshanufaika huku shule nyingine
zikianza rasmi kuzalisha miche yao

Alifafanua kuwa toka kuanza kwa mradi huo ambao mpaka sasa umegharimu
kiasi chazaidi ya Milioni mbili umeweza kuwa na faida kubwa sana
tofauti na hapo awali ambapo mradi huo haukuwepo kwenye mpango wa
mamlaka hiyo

Akitaja faida hizo alisema kuwa ni pamoja na wanafunzi kuanza
kiujifunza aina mbalimbali ya miti toka wakiwa shuleni huku hali hiyo
ikiweza kuwafanya wao waweze kudyahifadhi mazingira na kuona kuwa kuna
umuhimu wa kuhifadhi mazingira

Faida nyingine aliyoitaja ni pamoja na kuanza kujijengea tabia ya kuwa
na misitu ya kifamilia ili kuweza kukabiliana na tatizo la mabadiliko
tabia Nchi ambayo limeathiri sana eneo hilo la Ngorongoro.

Wakati huo huo alisema kuwa mpaka sasa mradi huo unakabiliwa na
changamoto kubwa ya uharibifu wa misitu hasa  kwa upande wa wafugaji
kwani bado mifugo yao inaharibu misitu ambayo imeoteshwa na mamlaka
hiyo.

Kutokana na Changamoto hiyo alisema kuwa ni vema kama viongozi wa
Kijiji wakajiwekea utaratibu wa kuelezea jamii umuhimu wa mradi huo
lakini pia umuhimu wa kuhifadhi mazingira ili kuepusha eneo hilo na
ukame .

MWISHO

UKOSEFU WA GARI LA KUBEBEA MAZIWA WASABABISHA MAZIWA LITA 700 KUSHINDWA KUUZIKA KILA SIKU WILAYANI KARATU



Kiwanda Cha Ayalable Dairy kilichopo katika Wilaya ya Karatu Mkoani
Arusha kinakabiliwa na changamoto ya usafiri hali ambayo inasababisha
waweze kupokea maziwa lita 800 kwa siku badala ya lita 1500 kwa siku
moja kutoka kwa wafugaji jambo ambalo wakati mwingine linasababisha
hasara kubwa sana kwa wafugaji pamoja na matumizi mabaya ya maziwa

Akiongea na Waandishi wa habari wiki hii wilayani humo mtaalamu wa
maziwa wa wilaya hiyo ambaye ni Care Elias alisema kuwa changamoto
hiyo inasababisha madhara makubwa sana kwa wafugaji

Alifafanua kuwa hapo awali walikuwa wanapata maziwa machache sana
kutoka kwa wafugaji lakini kwa sasa maziwa ni mengi sana katika wilaya
hiyo ya Karatu ingawaje sehemu nyingi sana zenye maziwa bado zipo
mbali na eneo la mji hali ambayo inasababisha maziwa yashindwe kufika
katika kiwanda hich

Kutokana na changamoto hiyo alidai kuwa maziwa yanayopatikana kwa
ajili ya matumizi ya kiwanda ni machache sana ingawaje kwa huko
viijijini zaidi maziwa yanazalisha lakini yanashindwa kufika kiwandani


Akiongelea hali ya uzalishaji wa maziwa katika Wilaya hiyo ya Karatu
alidai kuwa uzalishaji wa maziwa umeongezeka sana tofauti na Miaka ya
nyuma ambapo Wilaya hiyo ilikuwa inapata maziwa kidogo sana

Alisema kuwa kwa sasa kiasi cha lita zaidi ya elfu nne kinazalishwa na
wafugaji wa Wilaya hiyo ya Karatu lakini hapo awali kiasi cha lita
elfu moja pekee ndicho kilichokuwa kinazalishwa hali ambayo wakati
mwingine ilikuwa inasababisha uhaba wa maziwa

Alimalizia kwa kusema kuwa pia kituo hicho kilijengwa kwa ufadhili wa
Mamlaka ya Ngorongoro hivyo basi ili kuweza kuokoa kiasi kikubwa cha
maziwa ambacho kinapotea kila siku ni vema kama mamlaka hiyo ingeweza
kuangalia upya tena namna ya kuwapa gari ambalo litaweza kubeba maziwa
hayo kutoka Vijijini zaidi na kuleta katika kiwanda hicho cha Ayalabe

Mwisho

NGORONGORO YATOA NGOMBE 20 ZENYE THAMANI YA MILIONI 20 KWA WANACHI WA WILAYA YA KARATU



Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro(NCAA)imefanikiwa kutoa Ngombe 20 wa
kisasa wenye thamani ya zaidi ya milioni 20 kwa vijiji vinne vya
Wilaya ya Karatu kwa madhumuni ya kuendeleza Uhifadhi wa maliasili
ndani ya Vijiji hivyo.

Akiongea na waandishi wa habari mapema wiki hii Afisa Ugani wa Mamlaka
hiyo ambaye ni Bw Salustin Hallu alisema kuwa huo ni moja ya miradi
inayotekelezwa na mamlaka hiyo

Alisema kuwa mradi huo ambao hapo awali ulianza rasmi na Ngombe wa
kisasa 20 uliweza kuwa na manufaa makubwa sana kwa Vijiji vya Troma,
Ayalabe, lositete,na Upperutele ambapo hapo awali baadhi ya wafugaji
kwenye vijiji hivyo walikuwa wanalazimika kuchunga ndani ya hifadhi

Alifaafanua kuwa mpaka sasa zaidi ya familia 98 kwenye mradi huo
tayari wameshanufaika kwa kuwa kila familia moja sasa ina ngombe wa
kisasa mmoja na lengo halisi likiwa ni kuhakikisha kuwa kila familia
inajijengea uwezo wa kuchunga ndani na wala sio kutoa mifugo kwenda
kutafuta malisho nje

“Ngorongoro inalinda sana ujirani mwema na wananchi wake na ndio maana
tukaona kuwa badala ya kuwakataza tu wananchi wasiingie kwenye pori
ambapo ni hatari kwa maisha yao wao pamoja na mifugo lakini pia tuwape
mbinu mbadala za kuhakikisha kuwa wanajikomboa ndio maana tukaanzisha
huu mpango ambao umeonekana kuwasaida sana wananchi wa hivi
vijiji”aliongeza bw Hallu

Awali alisema Mamlaka pia bado ina mkakati mbalimbali wa kuhakikisha
kuwa wanaweza kufikia familia zote sanjari na kuwapa elimu mbalimbali
juu ya umuhimu wa kufuga ndani laki ni pia kuwapa mbinu imara ambazo
zinatakiwa kutumiwa na wafugaji wa kisasa zaidi

Akiongea kwa niaba ya familia 98 ambazo zimenufaika na mradi huo wa
ngombe wa kisasa kutoka Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro bi Emirita
Martin alidai kuwa pamoja na kuwa wamepata Ngombe lakini bado Mradi
huo unapaswa kuongezewa ngombe ambao wataweza kuwanufaisha wanawake

Bi Emirita alibainisha kuwa kama kila Boma na familia zitapa Ngombe
mmoja ambaye atazaliana basi wakina mama wataondokana na dhana ya kuwa
tegemezi kwenye maisha ya kifamilia kwani ufugaji unabadilisha maisha
duni na maskini ambayo wanayo baadhi ya wanawake katika Wilaya hiyo ya
Karatu

MWISHO

MWANDRI AWATAKA WAKRISTO KUSOMA VITABU VYA MUNGU KULIKO VENYE SIMULIZI ZISIZOJENGA JAMII

Na Bety Alex, Arusha



Waziri Agrey Mwandri amewataka wakristo kuachana na tabia ya kukwepa kujisomea vitabu mbalimbali ambavyo vinaongeza maarifa ya kiroho na kimwili kwani kwa njia ya vitabu hata maarifa juu ya ufalme wa Mungu nayo yanaongezeka sana

Mwandri aliyasema hayo wiki iliyopita katika kanisa la Winner Chapel Intrenational Arusha lililopo maeneo ya Kaloleni Mjini hapa wakati akizindua rasmi Kitabu kilichoandaliwa na Muinjilisti Paul Dickson kijulikanacho kama Ufalmwe wa Mungu hutekwa na wenye nguvu.

Alisema,kwa sasa wapo baadhi ya wakristo ambao wanapenda kujisomea vitabu ambavuyo havina maslahi na Mungu na badala yake vitabu hivyo vinahamsisha dhambi jambo ambalo kwa sasa wanatakiwa kulikataa

Alifafanua kuwa kama kila mkristo atahakikisha kuwa hapotezi muda wake mwingi kwenye vitabu hivyo a,mbavyo havijengi basi ni wazi kuwa hta dhambi ndani ya mkoa wa Arusha lakini Tanzania kwa ujmla nazo zitapungua kwa kiwango

Alibainisha kuwa kwa kusoma vitabu ambavyo vina madharai ya mwenendo wa Kimungu kunasaidia sana kuhimiza hata nguvu za Mungu kushuka na kuongoza katika mambo mbalimbali.

“jamani jiwekeeni utaratibu wa kuhakikisha kuwa mnasoma vitabu venye madhari ya Kimungu msinione hapa napambana kweli kule Bungeni lakini niwaambieni kuwa muda wangu mimi natumia hivi hivi vitabu vya mungu kujisomea na kuhakikisha kuwa naktafuta hata suluhu kule Bungeni hivyo basi igeni mfano huu “aliongeza Mwandri

Katika hatua nyingine Mwandishi wa kitabu hicho ambaye ni Muinjilisti Paul Dickson alisema kuwa lengo na maudhui ya kitabu hicho kijulikanacho kama Ufalme wa Mungu hutekwa na wenye nguvu, kina malengo ya kuhakikisha kuwa kinawakomboa baadhi ya watu katika ufalme wa Mungu

Muinjlisti huyo alidai kuwa kwa sasa wapo baadhi ya watu ambao wanatamani sana kuwa na falme wa Mungu lakini bado hawajaju hata siri za kuweza kuuteka ufalme huo hali ambayo wakati mwingine inasababisha waone kama ni wakosaji

“hiki kitabu kina siri nyingi sana za uponyaji na jinsi ya kuuteka ufalme wa Mungu hivyo basi natamani kuona kuwa watuw a sasa hususani mkoa wa Arusha na Tanzania wanaweza kuinuka  na kutoka katika hali Fulani hata za umaskini kwa kuwa ufalme wa Mungu kuuteka ni bure kabisa’aliongeza muinjilisti huyo

Alimalizia kwa kusema kuwa pamoja na kuwa vitabu vya Mungu vinaweza hata kuokoa lakini bado ipo changamoto kubwa sana kwa waaandishi wa vitabu kwa kuwa baadhi yao huandika zaidi vitabu ambavyo vinahusu mapenzi na kusahau vitabu vya kuwakomboa watu jambo ambalo si jema kwa maendeleo ya watu

MWISHO

UHAMIAJI YATARAJIA KUKUSANYA BILIONI 85



Na mwandishi wetu Arusha

Idara ya Uhamiaji hapa nchini inatrajia kukusanya kiasi cha zaidi ya
Bilioni 85 kwa kipindi cha mwaka 2013/2014 ambapo makusanyo hayo
yanatokana na mapato mbalimbali ya idara hiyo ambayo ipo chini ya
Wizara ya mambo ya ndani.

Hayo yameelezwa na Kamishana wa utawala na fedha katika idara hiyo
ambaye ni Bw Piniel Mgonja wakati akiongea  katika mkutano wa
tathimini wa utendaji kazi kwa wahasibu wa idara wa uhamiaji
unaondelea Jijini hapa

Piniel alisema kuwa kiasi hicho cha fedha kinaweza kupatikana na
kuvuka malengo kutokana na ukusanyaji wa Madhuhuli kuboreshwa zaidi
tofauti na miaka ya nyuma hali ambayo mpaka sasa itasaidia sana
kuongezeka kwa mapato ya idara hiyo.


Mbali na hayo alisema kuwa  hata kwa sasa vipo  baadhi ya vyanzo
vingine ambavyo  navyo vimechangia sana kuongeza mapato katika idara
hiyo ambapo vyanzo hivyo ni pamoja  vyanzo vya vibali vya kuishi
Nchini, huduma za Pasipoti, Hati za kusafiria,huduma ya uraia ,Viza
kwa wageni wanaoishi hapa Nchini

Kutokana na hali hiyo alisema kuwa bado idara ya uhamiaji hapa nchini
inakabiliwa na  changamoto kubwa ambayo ni ukosefu wa huduma za
kibenki katika baadhi ya vituo vya uhamiaji hapa nchini hali ambayo
wakati mwingine inasababisha upotevu na umanifu wa kifedha kwa
wafanyakazi pamoja na wadau wa uhamiaji

Alisema kuwa hali hiyo  si nzuri sana kwani nayo inachangia sana
kupunguza hata mapato ya Serikali kwani baadhi ya mapato huwa
yanapungua au kupotea kabisa kutokana na ukosefu wa huduma za kibenki.

Awali Akifungua mkutano huo Katibu Mkuu wa wizara ya mambo ya ndani
Nchi, bw Mbarak Abdulwakil alisema kuwa wahasibu katika wizara hiyo
wanatakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia sheria,Kanuni , na taratibu
zilizopo kwani usimamizi wa fedha unataka usimamizi wa hali ya juu
sana kwani fedha zinaushawishi mwingi sana

Alisistiza huduma ya malipo ya fedha inatakiwa kufanyika kwa njia ya
benki na kwa wakati na kwamba katika ukusanyaji wa maduhuli au katika
matumizi ya fedha na rasilimali nyingine benki ndio mahala sahihi pa
kuweka fedha hizo ili kuondo kasoro zinazoweza kujitokeza.

MWISHO

VIONGOZI WASIOWAJIBIKA CHANZO CHA NCHI KUWA MASKINI INGAWAJE INA RASILIMALI ZA KUTOSHA


Na Queen Lema, Arusha

IMEELEZWA kuwa dhana ya kutowajibika kwa baadhi ya Viongozi wa sekta mbalimbali hapa nchini imesababisha Nchi ya Tanzania kuonekana maskini ingawaje ina rasilimali nyingi sana ambazo zingeweza kuwanufaisha jamii

Hayo yameelezwa juzi na Naibu Waziri wa maliasili na utalii,Bw Lazaro Nyalandu wakati akiongea kwenye maafali ya nne ya chuo cha habari maalumu kilichopo katika eneo la Ngaramtoni Jijini hapa.

Bw Nyalandu alisema kuwa kwa sasa asilimia kubwa ya viongozi wamejisahau katika uwajibikaji wao na badala yake wanajiweka kwenye utaratibu wanaoutaka wao hali ambayo inasababisha kazi na malengo mbalimbali ya taifa kukwama huku nao wananchi wakiendelea kulaumu  Serikali.

Alisema kuwa hali hiyo ya kutowajibika kwa baadhi ya viongozi wa sekta mbalimbali ndio iliyosababisha Tanzania ya sasa kuonekana kama ni mojawapo ya nchi maskini duniani ingawaje kuna rasilimali za kutosha ambazo kama zingetumika basi zingeweza kuwanufaisha watanzania wote

Alisema ili maendeleo ya nchi ya Tanzania yaweze kuja ni lazima kila kiongozi ahakikishe kuwa anawajibika ipasavyo lakini pia ahakikishe kuwa anakuwa mbunifu wa kuweza kubuni aina mbalimbali ya njia ambazo zitasababisha nchi isionekane kama maskini lakini pia hata rasilimali nazo ziweze kuwanufaisha wazawa


Awali mkuu wa chuo hicho cha habari Maalumu BwJackson Kaluzi alisema kuwa pamoja na kuwa wamefanikiwa kutoa elimu ambayo inawasaida vijana wa kitanzania lakini bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali

Bw Jackson alitaja Changamoto hiyo kuwa ni pamoja na ukosefu wa Ardhi ya kutosha kwa ajili ya kuapanua eneo la chuo jambo ambalo mpaka sasa chuo hicho kimeshindwa kupanua eneo lake


            MWISHO

MFANYAKAZI WA TANZANITE APIGWA RISASI

MFANYAKAZI wa kampuni ya uwekezaji ya Tanzanite One inayochimba madini eneo la Mirerani, wilayani Simanjiro, Willy Mushi (), ameuawa kwa kupigwa risasi na watu wanaoaminika kuwa ni wachimbaji wadogo baada ya kukutana mgodini chini ya ardhi.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Manyara, Akili Mpwapwa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo alilosema lilitokea Saa 6:00 usiku wa kuamkia jana na tayari ametuma timu ya upelelezi unaoongozswa na Afisa upelelezi wa mkoa huo, kuchunguza zaidi tukio hilo.
Marehemu alipigwa risasi mbili kufuani upande wa kushoto alipoongozana na mfanyakazi mwenzake Kennedy Masimbaji kukikagua eneo la mgodi unaoingiliana na migodi ya wachimaji wadogo.
“Tulipofika kwenye mitobozano ambako kumepangwa mifuko ya viroba vya mchanga kutenganisha mgodi wetu na ile ya wachimbaji wadogo, ghafla tukashambuliwa kwa risasi ambazo zote zilimuingia marehemu kifuani na kufariki papo hapo,” alisema Masimbaji
Mfanyakazi mwingine wa Tanzanite One, leonard Paul alisema tukio hilo ni muendelezo wa mashambulizi yanayodaiwa kufanywa na wachimbaji wadogo dhidi ya wafanyakazi wa mwekezaji pindi wanapokutana chini ya ardhi ambapo siku kadhaa zilizopita uongozi ulilazimika kusimamisha kazi kutoa fursa ya polisi kuchunguzi migogoro ya mitobozano.
 “Serikali lazima sasa ichukue hatua kuzuia matumizi ya silaha za moto chini ya migodi,” alisema Paul
Kwa mujibu wa Mdogo wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Tumsifu Mushi, marehemu ameacha mjane na watoto wanne na taratibu za mazishi zinaendelea.
Mwisho.