Tuesday, March 26, 2013

UGONJWA WA MAHINDI KUTOKA KENYA WAWAATHIRI WANANCHI KATA YA KIKWE MERU


UGONJWA WA MAHINDI KUTOKA KENYA WAWAATHIRI WANANCHI KATA YA KIKWE MERU

ZAIDI ya Hekari 300 kutoka katika kata ya Kikwe Wilayani Meru mkoania Arusha zimeharibiwa vibaya na ugonjwa mahindi kutoka Nchini Kenya unaojulikana kama ugonjwa wa kusinyaa kwa mahindi hali ambayo itafanya wakulima washindwe kupata mahindi wakati wa mavuno

Akiongea na “patapata”mapema jana diwani wa kata hiyo bw Emanuel Silayo alisema kuwa hali hiyo ya ugonjwa ambayo imekumba kata hiyo ya Kikwe inaashiria njaa kubwa sana kwa kuwa mazao ya mahindi shambani hakuna huku wakulima wakiwa wameshapanda

Silayo alisema kuwa Miezi michache iliyopita wakulima waliweza kupanda mazao ya nafaka hasa mahindi lakini baada ya mahindi kuchomoza yalianza kushambuliwa na ugonjwa hadi kufa

Alisema kuwa pamoja na kuwa mahindi hayo yamekufa wakati wakulimna wengi wamepanda kwa ajili ya mategemeo ya chakula katika eneo hilo la Kikwe lakini mahindi machache sana yameweza kusalia hali ambayo bado ni kiashirio kikubwa sana cha Njaa


Alifafanua kuwa kama tahadhari haitaweza kuchukuliwa kwa haraka sana basi huenda wakati wa mavuno ndani ya mwaka huu kusiwe na mavuno kabisa hivyo baa la njaa kuweza kutawala katika Wilaya hiyo ya Meru.

Akiongelea Ugonjwa huo wa mahindi kutoka nchini Kenya Afisa Kilimo Wilaya ya Meru,Grace Solomoni alisema kuwa ugonjwa huo ni hatari sana kwa kuwa unashambulia zao la mahindi hadi kufa lakini bado mkulima anaweza kupata angalau kiasi kidogo

Grace alisema kuwa kwa mujibu wa taararibui za kilimo mara baada ya shamba kuathiriwa na ugonjwa huo shamba linapswa kupumzishwa kwa kipindi cha miaka mitatu ili vijidudu vife lakini kama wakulima wataendelea kulima basi watasababisha  vijidudu hivyo kuzaliana kwa wingi sana

MKAPA FOUNDATION YATOA MAFUNZO KWA TIMU ZA USIMAMIZI WA AFYA KUTOKA KATIKA WILAYA 132 HAPA NCHINI

NA MWANDISHI WETU,ARUSHA

MKAPA FOUNDATION YATOA MAFUNZO KWA TIMU ZA USIMAMIZI WA AFYA  KUTOKA KATIKA WILAYA 132 HAPA NCHINI

TAASISI ya Mkapa Foundation imefanikiwa kutoa mafunzo timu za usimamizi wa afya kwenye Wilaya 132  hapa nchini huku  mafunzo hayo yakiwa na malengi ya kuwajengea uwezo wa rasilimali watu ili waweze kutoa huduma bora zaidi za afya katika maeneo yao ya kazi.

Hayo yamebainishwa na Afisa Mpango kitengo cha uwezehsaji katika taasisi hiyo,Bi Pamela Chiwa wakati akiongea na wataalamu wa afya kutoka katika vituo vya afya ndani ya kanda ya kaskazini mapema jana

Aidha Pamela alisema kuwa timu hizo za usimamizi wa afya katika ngazi ya Wilaya ziliweza kupatiwa mafunzo hayo ya rasilimali watu  yaliweza kudumu hapa nchini kwa muda wa mwaka mmoja ambapo mpaka sasa mafanikio  makubwa sana yameshonekana katika sekta hiyo ya Afya

Alifafanua kuwa mbali na kuweza kuwajengea uwezo wataalamu hao wa afya ambao ni timu za usimamizi wa afya lakini sasa wanashuka zaidi ambapo wanalenga pia kuwapa mafunzo kama hayo hayo wataalamu wa afya kutoka katika vituo vya afya.

Alibainisha kuwa yote  hayo ambayo yanafanyika chini ya Taasisi ya Mkapa Foundation yanalenga kuhakikisha kuwa kila watanzania wanapata huduma bora na kwa wakati ili kuokoa maisha ya watu wengi zaidi ambao ndio nguvu kazi ya taifa la leo


Katika hatua nyingine alisema kuwa nao wataalamu wa afya wanatakiwa kuhakikisha kuwa wanaachana na dhana inayosema kuwa wataalamu wa afya ni wachache katika vituo,na hata hospitali bali wanatakiwa kuhakikisha kuwa wanafanya kazi tena kwa ubora wa hali ya juu hata kama wapo wachache

Hataivyo alisema kuwa kama wataalamu hao watafanya kazi kwa ubora ambao unatakiwa basi watachangia sana huduma za afya kuweza kuboreka zaidi ya sasa huku hali hiyo pia itachangia kwa kiwango kikubwa maendeleo ya Nchi  hivyo hata malengo ya Taaasisi hiyo ya Benjamini Mkapa nayo yataweza kufanikiwa kwa kiwango cha hali ya juu sana.

MWISHO

Thursday, March 14, 2013

WANAWAKE 33 WAPEWA ELIMU ILI WAJIKOMBOE


WANAWAKE wapatao 33 kutoka tarafa ya Manyara, wilayani Monduli, mkoa wa Arusha wamenufaika na elimu ya ujasiliamali, Afya ya uzazi, stadi za maisha na ukimwi iliyotolewa na shirika lisilo la kiserikali kutoka nchini Ujerumani liitwalo DSW.

Mafunzo hayo ya siku tano yalifanyika kwenye eneo la Mto-wa-Mbu, na kuwashirikisha wataalam kutoka Mradi wa Kuwawezesha Wanawake na Wasichana (WOGE)

Akizungumza juzi, mmoja wa wakufunzi kutoka mradi wa WOGE, Daudi Tano alisema: “Lengo la mafunzo hayo ni kumjengea uwezo mwanamke ili aweze kujitambua yeye kama yeye,mambo muhimu ya kufanya kwenye jamii,pamoja na jinsi ya kujikinga na maambukizi ya Ukimwi


Mtaalam huyo alisema mafunzo hayo yalilenga kumkomboa mwanamke kutokana na changamoto nyingi anazakabiliana nazo katika maisha yake ya kila siku.

Alifanunua kuwa WOGE ni mradi wa kikanda ambao unatekelezwa kwenye nchi za Tanzania, Kenya, Uganda na Ethiopia ukilenga zaidi kuwakwamua wanawake na wasichana walioko pembezoni hasa wale wa vijijini. Nchini Tanzania

“Mradi unawalenga zaidi wanawake wa vijijini walio na umri kati ya miaka 16 na 55, ambao wapo kwenye ajira isiyo rasmi na ambao hawapo shuleni ama hawana ajira,” alisema,

Pia aliongeza  kuwa madhumuni ya mradi huo ni kutoa mchango katika jitihada za kupambana na umaskini kwa kuwawezesha wanawake na wasichana ili waweze kusimama wao wenyewe kichumi na kutokuwa wategemezi.


Naye Afisa ustawi wa jamii Tarafa ya Manyara, Denis Magiye alilishukuru shirika la DSW kwa elimu hiyo na kuyataka mashirika mashirika mengine kuiga mfano huo ili kumkomboa mwanamke na msichana wa Kitanzania.

Alisema elimu ya uzazi inahitajika sana katika nyakati hizi kwani uzazi wa mpango humpatia mwanamke uhuru wa kufanya shughuli zake za kuinua kipato cha familia.

“Kuzifahamu njia za uzazi wa mpango kutawasaidia hata kupunguza idadi idadi ya watoto ambao hawajatarajia kuwapata na pia kupunguza vifo vinavyotokana na masuala ya uzazi,” alisema.

MWISHO

Saturday, March 9, 2013

UKOSEFU WA NYUMBA ZA POLISI MERERANI CHANZO CHA UTENDAJI HAFIFU WA POLISI


UKOSEFU WA NYUMBA ZA POLISI MERERANI CHANZO CHA UTENDAJI HAFIFU WA POLISI


IMEELEZWA kuwa ukosefu wa nyumba za askari polisi wa kituo cha Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara unachangia kuchelewesha utendaji kazi wao kwani inawabidi watoke majumbani kwao na kwenda kituoni ndipo wafike kwenye eneo la tukio.

Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Mirerani,Albert Siloli kwenye kikao cha siku ya familia ya polisi na wadau wa mji huo cha kujadili tathmini ya utendaji kazi wake kwa mwaka uliopita.

Siloli alisema ukosefu wa nyumba za askari polisi unachangia kwa kiasi kikubwa kudhoofisha utendaji kazi wao kwani unawachelewesha kufika kwenye tukio husika na kuchukua hatua stahili ikiwemo kuthibiti uhalifu.

Alisema Serikali inapaswa kulipatia ufumbuzi tatizo hilo kwa kuwajengea nyumba karibu na kituo cha polisi askari hao ili waweze kutimiza wajibu wao kwa jamii ipasavyo kwani hivi sasa mji huo unazidi kupanuka kwa haraka.

Hata hivyo,kwa niaba ya wenyeviti wengine wa mitaa ya mji mdogo wa Mirerani,Siloli alitoa pongezi kwa askari hao kwani uhalifu hivi sasa umepungua kwa kiasi kikubwa kwenye mji wa Mireraani hivyo jamii inaishi kwa amani ya kutosha.   

Pia,Mwenyekiti huyo alimpongeza Mkuu wa kituo cha polisi Mirerani,Mrakibu Msaidizi wa polisi Ally Mohamed Mkalipa kwa kuandaa hafla kwani haijawahi kufanyika tangu kituo hicho kianzishwe mwaka 1998 na utendaji kazi wao ni wa asilimia 100.

Pamoja na hayo alisema baadhi ya askari wa usalama barabarani wanakabiliwa na changamoto ya kudaiwa kupokea rushwa kwenye kazi zao hivyo kulitia doa jeshi hilo kwani jamii inalalamika mno kuhusiana na jambo hilo.

Kwa upande wake,Mkuu wa kituo cha Polisi Mirerani Mrakibu Msaidizi wa polisi (ASP) Ally Mohamed Mkalipa aliwashukuru wenyeviti wa mitaa hao kwa kutambua kuwa uhalifu hivi sasa umepungua kwenye mji huo.

Mkalipa ameeleza kuwa jamii inatakiwa kuongeza ushirikiano kwao kwani ni dhahiri shahiri uhalifu umepungua kwa kiasi kikubwa na watajitahidi kuondokana na changamoto zinazowakabili

Kuhusu suala la baadhi ya askari polisi kuhusishwa na upokeaji rushwa amesema watalifuatilia jambo hilo kwani maadili yanawataka askari  wasijihusishe na vitendo.

Alisema kisingizio cha kudai kuwa mshahara mdogo unachangia polisi kupokea rushwa siyo sahihi kwani upo utafiti umebaini kuwa hata wanaopokea mshahara mkubwa wana kawaida ya kupokea rushwa hivyo watawachunguza na wakiwabaini watawachukulia hatua ikiwemo kuwashitaki kijeshi,kuwafukuza kazi na kwenye mahakama za kawaida.

MWISHO.

ARUSHA YAKAMILISHA MPANGO MKAKATI WA UENDELEZAJI WA MAENEO MBALIMBALI YA MIJI


ARUSHA YAKAMILISHA  MPANGO MKAKATI WA UENDELEZAJI WA MAENEO MBALIMBALI YA MIJI


MKOA wa Arusha, umekamilisha mpango mkakati wa kuyaboresha na kuyaendeleza maeneo yote ya miji midogo ambayo hayajaharibiwa kutokana na ujenzi holela ili yawe ni ya mfano.

Hayo yamo katika taarifa ya Utafiti iliyotolewa na mtaalam wa mipango miji kutoka Taasisi ya kimataifa ya maendeleo ya miji, (IIUD) inayoongozwa na Profesa mstaafu wa Chuo kikuu cha Havad, nchini Marekani, Mona Serageldin kutoka nchini Misri ,aliyoiwasilisha kwenye kikao cha pamoja cha watendaji wa jiji la Arusha, Halmashauri ya Meru na halmashauri ya Arusha DC,mwishoni mwa wiki.

Profesa huyo amesema kuwa mpango huo unafadhiliwa naChuo kikuu chaAghakhan, una lengo la kuondoa tatizo la ujenzi holela ambalo halizingatii  ramani ya mipango miji na imesababisha miji mingi duniani kuwa na makazi holela hali ambayo inaharaisha usalama na amani ya wananchi .

ProfesaMuna amesema kupitia taasisi hiyo maeneo mengi ambayo ameshayafanyia utafiti na kukuta hayajaharibiwa hayataharibiwa tena kwa sababu sasa yatajengwa majengo ya mfano .

Amesema anasikitishwa na kushangazwa  na ujenzi holela ambao unaendelea kushika kasi katika maeneo mbalimbali hasa katika miji inayokua huku mamlaka husika zikishindwa kuzuia na kukomesha hali hiyo

Ameongeza  kuwa tayari taasisi hiyo imeshakamilisha kazi hiyo ya utafiti kwa Asilimia 70 kuhusu ujenzi na uboreshaji wa miji inayokuwa bila kuzingatia  mipango mipango miji na matokeo yake ni kuwepo uyoga wa nyumba  ambazo hazikupangiliwa.

Alifafanua kuwa kupitia mpango huo ujenzi holela utakwisha na wananchi watajenga kwa kuzingatia taratibu lengo ni kuwepo na miji iliyopangiliwa ambayo itakuwa ni kivutio.

Kwa upande wake Kaimu mkuu wa mkoa wa Arusha, Nyerembe Mnasa, amesema mara baada ya kukamilika kwa hatua hiyo ya mpango huo itafuatiwa na hatua ya kuwepo na Mapango mkakati (MasterPlan) ya jiji la Arusha na miji mingine mifdogo iliyopo halmashauri za Meru na Arusha Vijijini ambazo zitakuwa na maeneo ya mfano.

Nyerembe, amesema watendaji hawana budi kuunga mkono mpango huo ambao unakusudia kuondoa tatizo la ujenzi holela katika miji mingi nchini ambalo limekuwa ni sugu na kero ya muda mrefu .
 MWISHO

WAMILIKI WA SHULE BINAFSI WATAKIWA KUWAANGALIA YATIMA NA WALE WANAOTOKEA KATIKA MAZINGIRA MAGUMU


Na Queen Lema,Arusha

WAMILIKI WA SHULE BINAFSI WATAKIWA KUWAANGALIA YATIMA NA WALE WANAOTOKEA KATIKA MAZINGIRA MAGUMU

IMEELEZWA kuwa endapo kama Wamkiliki wa shule binafsi  wataweza kusaidia jamii za watoto yatima na wanaotokea katika mazingira magumu katika shule zao basi watachangia kwa kiwango kikubwa sana kupunguza tatizo la watoto wa mitaani.

Asilimia kubwa ya watoto wanaokimbilia mitaani wanakwena huko kwa kuwa baadhi ya familia zao hazina uwezo wa kuwasaidia katika masuala ya elimu hali ambayo nayo kwa wakati mwingine inasababisha wimbi la watoto hao.

Kauli hiyo imetolewa na  Bi  Isabela Daniel ambaye ni  Mkurugenzi wa Shule ya Upendo Friends iliopo Matevesi Jijini hapa mapema jana wakati akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea shule hiyo kwa malengo ya kutambua nafasi ya Watoto Yatima ndani ya shule Binafsi.

Isabela alisema kuwa kwa sasa kutokana na hali ya Maisha sio wanafunzi wote ambao wana uwezo wa kwenda shule hasa za binafsi na hata zile za Serikali hivyo basi kama wamiliki wa shule watakuwa wanaaacha kuliangalia suala hilo kwa undani ongezeko la watoto wa mitaani litakuwa ni kubwa sana.

Alifafanua kuwa wamiliki wanatakiwa kujiwekea utaratibu wa kuhakikisha kuwa kila mara wanaweka utaratibu wa kuwachukua japo kidogo na  kuwapa elimu wanafunzi ambao wanatokea katika makundi maalumu japo kwa uchache ambapo pia hali hiyo itachangia sana nafasi ya maendeleo katika taifa la Tanzania.


Awali Mkurugenzi huyo alisema kuwa nayo Serikali kwa kushirikiana na Shule Binafsi zinatakiwa kuhakikisha kuwa zinaweka utaratibu wa kutambua vipaji vya baadhi ya watoto kwani kwa sasa wapo baadhi ya watoto ambao wanavipaji lakini wanashindwa kuendelezwa

Alisema kuwa hali hiyo ya kuendeleza vipaji vya watoto itafanya baadhi yao waweze kujiimarisha zaidi hivyo hata kwa nyakati zijazo pia watachangia sana kupunguza tatizo la wataalamu ambalo kwa sasa linaikabili sana Nchi ya Tanzania.

MWISHO

IELIMISHENI JAMIII KUHUSU UMUHIMU WA MPANGO WA MKUHUMI- MUNASA NYIREMBE


IELIMISHENI JAMIII KUHUSU UMUHIMU WA MPANGO WA MKUHUMI- MUNASA NYIREMBE

Na Queen Lema,Arusha


VIONGOZI wa idara mbalimbali zinazohusika na Misitu hapa Nchini wametakiwa kuhakikisha kuwa wanatumia na wanaelimisha jamii kuhusu umuhimu wa mpango mkakati wa kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa itokanayo na ufyekaji  na uharibifu wa misitu(MKUHUMI) ambapo mpango huo unalengo lakuokoa tani nyingi zaidi za  misitu

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru,Munasa Nyirembe wakati akifungua warsha ya wadau wa mpango huo jijini hapa mapema juzi

Munasa alisema kuwa mpango huo ni muhimu sana kwa ajili ya maendeleo ya nchi ya Tanzania pamoja na mkoa wa Arusha ingawaje kwa sasa Changamoto ni kubwa sana  hasa maeneo ya vijijini ambapo asilimia kubwa ya jamii wanafyeka misitu kwa ajili ya matumizi mbalimbali

Alisema kuwa endapo kama Kiongozi wa idara atasimama vema katika nafasi yake na kuhamisisha umma juu ya umuhimu wa mradi huu basi atachangia kwa kiwango kikubwa sana kuokoa tani nyingi za misitu ambazo zinafyekwa na watu kwa maslahi yao

Alifafanua kuwa mpango huo wa MKUHUMI ni muhimu sana kwa maendeleo ya Nchi hivyo kinachoitajika kwa sasa ni suala zima la uhamasishaji baina ya watendaji wa mpango huo pamoja na wananchi ambao wakati mwingine wanaharibu misitu bila kujua umuhimu wake.

“huu mpango ni muhimu sana na kwa hali hiyo  napenda kuwasihi wananchi waupokee kwa kuwa una manufaa sana na kama utatumika vema utaweza kuhamisisha suala zima la upandaji wa miti  pamoja na misitu ambayo kwa sasa kwenye baadhi ya maeneo misitu hakuna huku hata iliyopo wakati mwingine inafyekwa kwa ajili ya maslahi ya watu wachache”aliongeza Nyirembe

Katika hatua nyingine Mratibu wa mradi  huo wa MKUHUMI wilaya ya Kilosa,Hassani Chikira alisema kuwa mpango huo ni muhimu sana kwa Nchi ya Tanzania hususani kwenye suala la Mabadiliko ya Tabia Nchi kwa kuwa unawahimiza wananchi walime na kuhifadhi Misitu ili waweze kupata fedha mbalimbali ambazo zinatumika kwa ajili ya masuala mengine ya kijamii

Akielezea mradi huo hapa nchini kwa sasa alisema kuwa umeshafanyiwa  uhamasishaji katika kanda  mbili ambapo viijiji kumi na nane kutoka kanda ya kati ambayo inajumuisha mikoa ya Manyara,Singida,na Dodoma, huku kwa upande wa kanda ya Mashariki ikiwa ni mikoa ya Pwani,Morogoro,na Dar es saalam

Aliongeza kuwa Wilaya ambazo nazo zimefanikiwa kufikiwa na mradi huo ndani ya kanda hizo mbili ni wilaya ya Babati pamoja na Wilaya ya Kongwa huku mpaka sasa mafanikio ya mpango huo yakiwa yameanza kuonekana  hali ambayo nayo itachangia sana kupunguza tatizo la uharibifu wa misitu.

MWISHO

Monday, March 4, 2013

VIONGOZI WA DINI WAKUTANA ARUSHA KWA AJILI YA KUOMBA AMANI KWA NCHI ZA EAC


VIONGOZI WA DINI WAKUTANA ARUSHA KWA AJILI YA KUOMBA AMANI  KWA NCHI ZA EAC

Na Queen Lema,Arusha


Viongozi wa dini wakiwemo wachungaji zaidi ya 400 kutoka katika nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki wamekutana Jijini Arusha katika Kongamano  kwa ajili ya kujadili mambo mbalimbali ya uongozi wao pamoja na kuombea nchi hizo amani hasa ya Nchi ya Kenya na Tanzania.

Akiongea na “Majira”jana mratibu wa kongamano hilo ambalo limeandaliwa na mtandao wa wachungaji mkoa wa Arusha,Bw Geofrey Ayo alisema kuwa kongamano hilo lina manufaa makubwa sana kwa Nchi hizo

Ayo alisema kuwa amani ya nchi inatakiwa ipite hata kwa viongozi wa dini kwa kuwa wao wana nafasin kubwa sana ya kuweza kuhubiri amani tofauti na viongozi wengine wowote hivyo basi mtandao huo umechukua nafasi hiyo kwa ajili ya kuhakikisha kuwa nchi hizo zinakuwa na amani

Alisema kuwa wachungaji hao zaidi ya 400 ambao wamekutana Jijini Arusha wameweza kujadili mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na hata jinsi ya kulinda amani ambayo baadhi ya Nchi imepotea kwa sababu mbalimbali hivyo kupitia kwa waumini wao wataweza kuwafanya wananchi walinde amani

“tumekutana hapa kuhakikisha kuwa tunajadili mambo mbalimbali ya msingi lakini pia kuhakikisha kuwa kila Kiongozi anakuwa balozi wa kulinda amani na wala sio kwenye serikali kwani sisi Viongozi wa dini tuna nafasi kubwa sana ya kutekeleza suala hilo ambalo wakati mwingine tunaachia Serikali pekee’aliongeza Ayo

Mbali na hayo aliwataka Viongozi wa dini kuhakikisha kuwa wanajiwekea utaratibu wa kuhakikisha kuwa mbali na kuomba amani kwa nchi husika lakini watumie nafasi mbalimbali ambazo wanazo kwa kuwataka waumini wao waweze kufanya kazi kwa bidii na kisha kupambana na Umaskini

Alifafanua kuwa kama Viongozi wa dini wataweza kufanya hivyo basi wataweza kuondoa Mataifa ya jumuiya ya Afrika ya Mashariki hususan Tanzania kutoka katika  hali ya umaskini ambayo ipo na kufika katika viwango vya hali ya juu ambapo hata hali ya ugumu wa maisha wakati mwingine inachangia sana uharibifu wa amani, pamoja na umaskini.

“kwa sasa kuna changamoto kubwa sana za masuala ya kimaisha lakini viongozi wa dini wanatakiwa kuhakikisha kuwa wanaweka utaratibu wa kusisisitiza watu wahakikishe kuwa wanafanya kazi na waache kukaa kaaa ovyo mitaani na pindi wanapokaa mitaani ndipo wanapofanya na kuwaza hata mbinu za kuharibu amani’aliongeza Ayo

MWISHO.

KESI YA MWANDISHI WA HABARI ZA UCHUNGUZI ALIYEUWAWA BURKINAFASO KUANZA KUSIKILIZWA KATIKA MAHAKAMA YA AFRIKA


KESI YA MWANDISHI WA HABARI ZA UCHUNGUZI ALIYEUWAWA BURKINAFASO KUANZA KUSIKILIZWA KATIKA MAHAKAMA YA AFRIKA

Na Queen Lema,Arusha.

Mahakama ya  juu ya haki za binadamu inatarajia kuanza kusikiliza rasmi kesi iyaokabili Serikali ya bukinafaso juu ya mauaji ya Mwandishi wa habari za Uchunguzi Nobert Zongo pamoja na  wenzake watatu wakati wakiwa kazini December 13 mwaka 1998


Akiongea na Vyombo  vya habari mapema jana jijini hapa Afisa habari wa mahakama hiyo Bw jean Pierre alisema kuwa Kesi hiyo itaanza kusikilizwa kuanzia March saba na nane mwaka huu

Jean alisema kuwa kesi hiyo ambayo inaikabili Serikali ya burkinafaso itaweza kusikilizwa na Majaji 11 wa mahakama hiyo huku upande  kwa Upande wa wanasheria  wakitoka katika Nchi za Nigeria na Burkifaso ambao wanasimama kama wanasheria wa walalamikaji

“kesi hii itaendeshwa kisasa zaidi ambapo jopo la majaji wetu watasikiliza na kisha kuharisha kwa mujibu wa sheria za mahakama yetu  hivyo mara baada ya kuhairisha kesi hiyo basi watataja siku nyingine ya kusikilizwa tena’aliongeza Jean

Katika hatua nyingine alisema kuwa pia mahakama hiyo kupitia kwa Raisi wake Sophia Akufye inatarajia kumuapisha jaji Aba Kimelabaou kutoka Burkinafaso kama Jaji wa mahakama hiyo mara baada ya jaji Nyamihala Mulenga wa nchini Uganda kufariki dunia

Alisema kuwa Raisi wa Mahakama hiyo atapisha jaji huyo March 4 katika mahakama hiyo na kisha kuhudhuriwa na majaji 10 kutoka nchi mbalimbali duniani huku lengo likiwa ni kuongezea nguvu mahakama hiyo.

“March 4 mwaka huu tutamuapisha jaji huyu rasmi kama jaji halali kwa ajili ya shuguli mbalimbali za mahakama yetu hivyo pia wadau mbalimbali wa mahakama hii nao watakuwepo pamoja na viongozi wengine ili kuweza kushuhudia kitu ambacho kinaendelea siku hiyo”aliongeza Jean

MWISHO

HAKIKISHENI KUWA HAMUINGILII HAMUHARIBU KAZI ZA WAFADHILI- OLE MEDEYE


HAKIKISHENI KUWA HAMUINGILII HAMUHARIBU KAZI ZA WAFADHILI- OLE MEDEYE

Na Queen Lema,Arusha


Naibu waziri wa nyumba,ardhi na makazi ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Arumeru Magharibi,Goodlucky Ole Medeye amezitaka Serikali za Mitaa ukiwemo Uongozi wa Vijiji Mbalimbali ndani ya jimbo hilo kuhakikisha kuwa kamwe hawaangilii shuguli au miradi mbalimbali ya Wafadhili ambayo ina malengo ya kuwasaidia wananchi

Medeye aliyasema hayo Jimboni humo wakati akizundua zahanati  ya Ester iliopo katika Kijiji cha Ngaramtoni ambayo ilijengwa kwa nguvu za wafadhili kutoka nchini Uingereza kwa malengo ya kudumisha sekta ya afya hasa afya ya mama na mtoto

Medeye alisema kuwa kuwa endapo kama Vijiji vitakuwa vinaingilia masuala ya Miradi ambayo imetolewa na wafadhili kwa malengo mbalimbali ni wazi kuwa malengo hayo yatakwama na badala yake umaskini ndio utakaokirhiri huku jamii ikibaki na mateso mengi

Aliongeza kuwa kazi ya Serikali ya Kijiji ni kuhakikisha kuwa miradi hiyo inafanya kazi kwenye viwango vya hali ya juu kama yalivyokuwa malengo ya wafadhili  hivyo kama Serikali za kijiji zitafanya hivyo basi zitachangia sana mabadiliko tena ya hali ya juu huku mabadiliko hayo yakichangia kupungua kwa umaskini


Awali wanawake ambao ndio walengwa wakubwa sana wa mradi huo walisema kuwa zahanati hiyo itaweza kuwasaidia kwa kuokoa afya zao kwani walikuwa wanalazimika kutembea Umbali wa zaidi ya Kilomita Kumi kwa ajili ya kutafuta huduma za afya hali ambayo wakati mwingine husababisha vifo

“kabla hii zahanati ya ester haijaja tulikuwa tunatoka hapa mpaka Selian au mara nyingine tunaenda mpaka Mjini au Kaloleni sasa wakati huo kama unaumwa sana unaweza kupoteza maisha kutokana na umbali ila kwa sasa tuna uhakika wa kupata huduma bora tena za afya ya mama na mtoto’waliongeza wanawake hao

Mwisho

FANYENI KAZI KWA BIDII ILI MUONGEZE UFANISI WA BENKI YETU-MKURUGENZI ACB


FANYENI KAZI KWA BIDII ILI MUONGEZE UFANISI WA BENKI YETU-MKURUGENZI ACB

Na MWANDISHI WETU,ARUSHA

IMEELEZWA  kuwa endapo kama watendaji wa Benki ya Akiba watafanya kazi kwa bidii basi wataweza kuruhusu ushindani wa kibenki hivyo kuweza kutoa ruhusa hasa kwa wateja wake kunufaika na huduma mbalimbali zikwemo huduma za Mikopo


Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya Akiba hapa nchini John Lwande,wakati akiongea na wafanyakazi wa benki hiyo kutoka katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro mapema wiki hii

Aidha Lwande alisema kuwa  ipo haja ya wafanyakazi wa Benki kuhakikisha kuwa kamwe hawasababishi dosari zozote za kibenki kwa kuwa kwa sasa kuna wimbi kubwa sana la huduma hizo na badala yake wanatakiwa kuwafanya wateja waridhike na huduma za kibenki hasa kwenye Mikopo

Alifafanua kuwa endapo kama watafanya hivyo basi watakuwa ni miongoni mwa chanzo kikubwa sana cha kufanya mabadiliko ndani ya Nchi ya Tanzania kwa kuwa asilimia kubwa ya watanzania wataendelea kutumia huduma hizo za Kibenki kwa ajili ya maslahi ya Jamii zao


Akiongelea Suala la Mikopo kwa watanzania alisema kuwa  kwa sasa wanajiopanga kuhakikisha kuwa wanaongeza kiasi cha Mikopo ili kuweza kuwafikia watanzania walio wengi zaidi tena hasa wa Mikoa ya Dodoma na Mwanza ambapo wanatarajia kufungua matawi  mengi zaidi kwa maslahi ya shuguli za kibenki kwa wananchi wa  mikoa hiyo.

Alimalizia kwa kusema kuwa pamoja na kuweka mikakati ya kufungua matawi ambayo yataweza kuwasaidia wananchi kwenye masuala ya Kifedha lakini pia Benki hiyo kwa Mkoa wa Arusha na Kilimanjaro  kwa kipindi cha mwaka 2012 waliweza kuvuka malengo hali ambayo imeweza kuinua mapato ya Benki hiyo.

MWISHO