Wednesday, November 14, 2012

MBOWE -ACHENI PROPAGANDA FEKI


MBOWE -ACHENI PROPAGANDA FEKI
 
MWENYEKITI wa Chadema,Freeman Mbowe amesema watu wanaoeneza propaganda na kupanda mbegu chafu kwa kudai kuwa Chadema ni chama cha wachaga wamepoteza dira na kuhishiwa na hoja.
Mbowe aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wakazi wa mkoa wa Manyara kwenye uwanja wa Kwaraa mjini Babati katika ziara ya Chadema ya operesheni vuguvugu la mabadiliko (M4C) mkoani humo.
Alisema wanaoeneza fikra hizo potofu zisizo na mashiko wameishiwa na hoja na aliongeza kuwa Chadema hakifungamani na kabila wala dini yoyote ile kwani viongozi wake ni wametokana na dini tofauti na makabila mbalimbali.
Alisema Makamu wake upande wa bara Said Arfi ametokea Mpanda na wa upande wa Zanzibar ametokea Wete Pemba na Katibu Mkuu Dk Wilbroad Slaa ametokea Karatu na Naibu Katibu Mkuu Zitto Kabwe ametokea Kigoma.
“Kwa vile mimi ni mchaga wanasema Chadema ni chama cha wachaga,mbona Chama kinachoitwa mapinduzi sijui walipindua nini,Mwenyekiti wake ni mkwere lakini hakiitwi chama cha wakwere,” alisema Mbowe.
Alisema hata Wenyeviti wa TLP na NCCR-Mageuzi ni wachaga lakini vyama hivyo havisemwi kuwa ni vya wachaga ila Chadema kwa vile jamii inawaunga mkono na watu wamepata mwamko kuwafuata wanadai ni chama cha wachaga.
Aliwataka wakazi wa mkoa wa Manyara wajiandae kwa ajili ya mabadiliko kwa kuitoa CCM madarakani na kuiweka Chadema kwa njia ya kura mwaka 2015 na wajitokeze kwa wingi wakati wa kujiandikisha utakapofika.
Alisema mbunge mmoja wa Chadema ni sawa na wabunge 30 wa CCM ndiyo sababu wanashiriki kutetea na kutoa hamasa kwa watanzania wote bila kubagua eneo alilochaguliwa.
“Wabunge wa Chadema ni watu makini ndiyo sababu leo Halima Mdee mmemuona hapa Manyara,japokuwa yeye ni mbunge wa Kawe na Pauline Gekul naye hata nje ya nchi huwa nakwenda naye,” alisema Mbowe.
Naye,Mbunge wa viti maalum mkoa wa Manyara (Chadema) Pauline Gekul alisema CCM imekosa dira na mwelekeo katika mkoa huo hivyo wanasubiri kwa hamu kufanyika kwa uchaguzi mkuu ili waiondoe madarakani.
“Wana wa Manyara wamechoka na CCM hivyo Kamanda Mbowe wana kuhakikishia kwa kusema CCM kwisha,kwisha,kwisha kabisa na jibu ni mwaka 2015 pale ambapo watakapoitoa madarakani kwa njia ya kura,” alisema Gekul.
MWISHO.

No comments:

Post a Comment