Thursday, September 20, 2012

DKT ASHA MIGIRO KUWA MGENI RASMI BARAZA LA VIONGOZI WA SERIKALI ZA MITAA

Na Queen Lema ,Arusha

ALIYEKUWA naibu katibu mkuu wa umoja wa mataifa Dkt Asha Rose Migiro
anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kuzindua baraza la viongozi wakuu wa
serikali za mitaa la Afrika Mashariki linalotarajiwa kuzinduliwa mjini
arusha kuanzia septembaer 24 ambapo mkutano huo utaudhuriwa na mawaziri
wa serikali za mitaa na viongozi wa juu wa serikali za mitaa kutoka nchi zinazounda
jumuiya ya afrika mashariki.

Hayo yalielezwa na mkuu wa kitengo cha mawasiliano kutoka Ofisi ya Waziri
Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) bi Rebecca Kwandu
alipokuwa akiongea na waandishi wa habari mjini hapa.



Alisema kuwa kupitia mkutano huo utaweza kuwawezesha viongozi wakuu wa
serikali za mitaa wa nchi wananchama kuzindua baraza la viongozi wakuu wa
serikali za mitaa la Afrika Mashariki yaani “The East African Local
Government Forum” ambapo kupitia baraza hilo wataimarisha utendaji wa
serikali za mitaa na utekelezaji wa dhana ya ugatuaji wa madaraka kwa umma
kwa lengo la kuleta maendeleo endelevu katika kanda ya afrika mashariki



“tunatarajia kukutana mjini hapa kwa lengo la kuwawezesha viongozi wakuu
kuzindua baraza la viongozi wakuu wa serikali za mitaa la afrika mashariki
ili kuwawezesha kufanya kazi kwa pamoja katika kuimarisha utendaji wa
serikali za mitaa hii itawasaidia kwa kiwango kikubwa kudumisha umoja
katika hata utendaji wa kazi zao”alisema bi Rebecca.



Aidha alieleza kuwa kupitia mkutano huu viongozi wa Serikali za Mitaa
watapata nafasi nzuri ya kubadilishana uzoefu kuhusu namna ya uwakilishi wa
wananchi unavyofanyika kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa kama vyombo vya
Uwakilishi wa wananchi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.



Alisema kuwa mkutano huo utazihusisha nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki za Burundi, Kenya, Rwanda, Tanzania na Uganda. ambapo pia nchi
za Visiwa vya Comoro na Sudan ya Kusini zimealikwa kushiriki.

Aidha aliwataja washiriki wengine wa mkutano huo ni wadau wa maendeleo
ambao ni Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Mfuko wa
Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNCDF) na Shirika la Maendeleo la
Ujerumani(GIZ).


MWISHO

No comments:

Post a Comment