Wednesday, November 28, 2012

KAMPUNI YA CHINA YA CHICO IMEJITOLEA KUTUMIA MILIONI 50

Na Joseph Lyimo,MANYARA

KAMPUNI ya Ujenzi ya China ya Chico imejitolea kutumia sh50 milioni kwa ajili ya ukarabati wa kituo cha magari ya kubeba abiria kilichopo mjini Babati Mkoani Manyara ili kumaliza kero iliyopo kituoni hapo mvua zinaponyesha.

Akizungumza juzi mjini Babati mbele ya viongozi wa halmashauri ya wilaya hiyo wakati wakuanza kukarabatiwa kituo hicho,msemaji wa kampuni ya Chico,Yan Wangting alisema lengo lao ni kutoa msaada kwa jamii inayotumia kituo hicho.

Wangting alisema Mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Babati,Mohamed Farah alizungumza naye na kuomba msaada wa kukarabatiwa kituo hicho ambacho wakati mvua zikinyesha kunakuwa na kero ya madimbwi ya maji.

Alisema kuwa ili kushiriki shughuli za maendeleo,kampuni ya Chico imejitolea kufanya kazi hiyo bure ili kuondoa adha ya wasafiri na magari yanayotumia kituo hicho hasa kero ya maji wakati mvua zinaponyesha.

“Lengo la kampuni ya Chico kukarabati kituo hiki ni kutoa mchango wetu kwa jamii ambapo tunatarajia kutumia siku tatu hadi nne katika kuhakikisha kuwa kazi hii imekamilika na kituo kinaendelea kutumika,” alisema Wangting. 

Kwa upande wake,Mwenyekiti wa halmashauri ya mji huo,Mohamed Farah aliipongeza kampuni hiyo kwa kujitolea kukarabati kituo hicho cha mabasi cha mjini Babati ili kiweze kutoa huduma ipasayo ya usafiri mjini hapo.

“Tunaishukuru kampuni ya Chico kwa kuamua kutukarabatia stendi yetu na wananchi wasiwe na wasiwasi wala hofu ya kuona ukarabati ukiendelea ila mnapaswa kutambua huu ni msaada tu na siyo vinginevyo,” alisema Farah.

Alisema hivi sasa magari ya usafiri ya mji huo yanatoa huduma hiyo kwenye uwanja wa mpira wa miguu wa Kwaraa kwa muda wote ambapo ukarabati wa kituo ukiendelea hivi sasa.

Naye,Kaimu Mkurugenzi wa mji wa Babati,Winnie Kijazi alisema ili kuunga mkono msaada huo uliotolewa na kampuni ya Chico,jamii inapaswa kutunza mradi huo pindi utakapokamilika.

“Tunaishukuru sana kampuni ya Chico kwa kutukarabatia kituo hiki na tunapaswa kuuenzi msaada huu kwa kuitunza miundombinu yetu ya kituo chetu ili kiweze kutunufaisha kwa muda mrefu zaidi,” alisema Kijazi.

Kampuni ya Chico ndiyo iliyojenga barabara ya Minjingu-Babati ambapo mwanzoni mwa mwezi huu,Rais Jakaya Kikwete aliizindua barabara hiyo ambayo imerahisisha usafiri wa kutoka mkoani Manyara hadi Arusha.

MWISHO.

No comments:

Post a Comment