Wednesday, November 14, 2012

WANANCHI WALALAMIKIA MATIBABU YA KITUO CHA AFYA



Joseph Lyimo,Babati
WAGONJWA wanaopata matibabu kituo cha Afya Magugu Wilayani Babati Mkoani Manyara wameulalalamikia uongozi wa kituo hicho kutoweka mazingira safi kwani uchafu umekithiri hadi kusababisha kunguni kuenea vitandani.
Kutokana na hali hiyo wagonjwa hao walidai kuwa wanafika kwenye kituo hicho wakiwa wana maradhi tofauti na wana rudi majumbani wakiwa na magonjwa tofauti yanayosababishwa na kunguni hao walioenea kwenye kituo hicho.
Wagonjwa hao waliyasema hayo walipotembelewa na waandishi wa habari wa mkoani Manyara waliokuwa kwenye mafunzo ya kuandika habari za vijijini yaliyoandaliwa na Umoja wa Vilabu vya Waandishi nchini UTPC.
Wagonjwa hao waliwaeleza waandishi walioongozana na mwezeshaji wa mafunzo hayo Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mwanaspoti linalotolewa na kampuni ya Mwananchi (MCL) Frank Sanga kuwa Serikali iangalie hali hiyo.
Mmoja kati ya wagonjwa hao Amina Juma alisema kila wakati wanapopata maradhi na kulazwa kwenye kituo hicho wanapata wakati mgumu kutokana na kung’atwa na kunguni wanaoenea katika vitanda wanavyovilalia.
“Pamoja na hayo pia tuna kero kubwa ya ukosefu wa vitanda kwani tunalala watu wawili katika kitanda kimoja hivyo tunaumia sana na kupata maumivu kutokana na kubanana wakati wa kulala,”alisema Juma.
Naye,Zulfa Shaban mkazi wa Gichameda alisema kutokana na hali ya uchafu kukithiri baadhi ya wagonjwa wanahofu ya kufika katika kituo hicho ili kupatiwa huduma ya afya wakizikumbuka kunguni zilizopo eneo hilo.
Hata hivyo,Mganga kiongozi wa kituo hicho cha afya Magugu Dk Abdalah Abasi alisema kunguni hizo zinaletwa na wagonjwa wenyewe kutoka majumbani mwao na kuzihamishia kwenye wodi za kulaza wagonjwa.
“Kwa kweli kunguni zinaletwa na wagonjwa wenyewe na wasiwasingizie wafugaji wa kibarbaig kuwa wanaleta kunguni kwani tumekuwa tunapiga dawa wodini baada ya wiki kunguni wanaletwa tena na wagonjwa,” alisema Dk Abasi.
Pia,alisema wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa fedha na wanashindwa kuongeza vitanda na kununua dawa za kutosha bohari kuu (MSD) hivyo jamii inatakiwa ijiunge na mfuko wa afya CHF ili waletewe dawa nyingi zaidi.
MWISHO.

No comments:

Post a Comment