Friday, November 9, 2012

Watanzania watakiwa kujenga tabia ya kucheki afya zao mara kwa mara

Watanzania watakiwa kujenga tabia ya kucheki afya zao mara kwa mara


Na Anna Nkinda – Maelezo
…………………………………………
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete ameitaka jamii kujenga mazoea ya kujichunguza afya zao mara kwa mara ili kuepuka maradhi au vifo visivyo na lazima kwani hivi sasa kuna maradhi mbalimbali yanayotokana na mazingira na aina ya mtindo wa maisha  na hivyo kurudisha nyuma maendeleo  binafsi na taifa kwa ujumla.

 Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) ameyasema hayo leo wakati wa uzinduzi wa kampeni ya utoaji huduma ya afya kwa jamii ikiwemo uchunguzi wa saratani iliyoandaliwa na Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (MEWATA) katika viwanja vya mnazi mmoja jijini Dar es Salam.

 Mama Kikwete pia aliitaka jamii kubadilisha mtazamo juu ya afya ya uzazi na mtoto kuwa inamhusu mama peke yake bali kila mmoja katika familia anahusika  ingawa hapo awali wanaume walionekana kutengwa na kutowajibika ipasavyo hivyo kusababisha kuzorota kwa afya ya uzazi na mtoto.
  “Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii pamoja na wadau wake hivi sasa wametuanzishia mchakato huu, awali huduma hii ilijulikana kama afya ya mama na mtoto lakini sasa inajulikana kama afya ya uzazi na mtoto hii ni kuonesha kwamba kila mmoja wetu ndani ya familia  anawajibika”, alisema Mama Kikwete.

No comments:

Post a Comment