Saturday, November 17, 2012

MADEREVA TOYO SEKEI WAPEWA MBINU ZA KUKABILIANA NA AJALI ZA BARABARANI






WAENDESHA “BODABODA” WAPEWA MBINU ZA KUDHIBITI UHALIFU
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha

Waendesha Pikipiki za abiria maarufu kama “bodaboda” kata ya Sekei wilayani Arusha wamepewa mbinu mbalimbali za kujikinga na wahalifu pindi wanapokuwa katika kazi zao.

Akiongea na Madereva hao katika Mkutano wa Ulinzi Shirikishi uliofanyika leo asubuhi  katika ofisi ya Afisa Mtendaji wa kata ya Sekei ambao uliwajumuisha Jeshi la Polisi, Viongozi wa kata hiyo na madereva wa Pikipiki za abiria Mkuu wa Polisi Wilaya ya Arusha, Mrakibu Mwandamizi wa polisi Gilles Muroto aliwafundisha mbinu mbalimbali ambazo madereva hao wanapaswa wazitumie.

 Alisema kwanza wanatakiwa wawe karibu na Jeshi la Polisi kimawasiliano ili waweze kupata msaada pindi wanapoona kuna mazingira hatarishi ikizingatiwa kwamba, uwa wanafanya kazi hadi usiku wa manane kauli ambayo ilizaa matunda baada ya madereva hao kila mmoja kuchukua namba ya simu ya Mkuu huyo wa Polisi.

 Pili alisema matukio ya wizi wa Pikipiki pamoja na uvamizi unasababishwa na baadhi  ya madereva ambao si waaminifu miongoni mwao wenyewe na wanaofanya vitendo hivyo wanajulikana hivyo aliwataka wanaowafahamu wahalifu hao kulisaidia Jeshi la polisi kwa njia ya taarifa ambazo zitafanyiwa kazi mara moja tena kwa njia ya usiri.

Aliwashauri waanze kuwa na ushirikiano wao wenyewe kupitia vikundi vyao hasa katika mawasiliano hali ambayo itasaidia kupata msaada pindi wanapopata tatizo.

Alisema madereva hao wanapaswa kuwa waangalifu kabla ya kumbeba abiria kwa kuangalia muonekano wake kuanzia nguo na alama nyingine ambazo zinaweza kulisaidia Jeshi la polisi katika upelelezi wa awali hasa pale inapotokea mwenzao kapatwa na tatizo la kihalifu.

Aliongeza kwa kusema kwamba,  pindi mwenzao anapombeba abiria, madereva wenzake anaowaacha wanatakiwa wamuangalie kwa umakini abiria huyo hali ambayo itasaidia mara baada ya mwenzao kusikia amekumbwa na tatizo iliyotokana na safari yake ya mwisho.

“Inatakiwa mpendane, mwezenu anapopata mteja wengine mliobaki mnatakiwa kumuangalia kwa umakini abiria huyo na kama inatokea mwenzenu amepata matatizo maelezo yenu yanapata pa kuanzia , kwamba yule mtu aliyeondoka naye muonekano wake upo vipi”. Alisisitiza Muroto.

Mbali na elimu hiyo kuhusiana na udhibiti wa uhalifu pia aliwataka madereva hao kuheshimu sheria za usalama barabarani ikiwa ni pamoja na kuvaa kofia ngumu “Helmet”na kuwa wastahimilivu katika vivuko kwani ajali nyingi zinazotokea zinasababishwa na wao wenyewe pindi wanapojaribu kuyapita magari yaliyo mbele yao wakati yakiwa yamesimama.

Mkuu huyo wa polisi Wilaya aliwataka madereva hao wa boda boda kutojichukulia sheria mkononi pindi mwenzao anapogongwa na gari na badala yake wanatakiwa watoe taarifa Polisi ili taratibu za kisheria zifuatwe.
Naye Mkuu wa Dawati la Jinsia na watoto mkoa wa Arusha Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Maria Maswa aliwashauri madereva hao kupitia vipato vya kazi yao kuwekeza katika maeneo mengine kama vile kilimo na biashara hali ambayo itawasaidia kujikwamua kiuchumi.

Alisema ajira walioipata inatakiwa wazidi kuiheshimu ili kipato kinachopatikana kiweze kutoa huduma bora kama vile elimu bora kwa watoto na hatimaye kujenga familia yenye ustawi hali ambayo kwa kiasi kikubwa itasaidia kuepusha ongezeko la watoto wa mitaani.

Kwa upande wake PC Rajabu kutoka kitengo cha Polisi Jamii mkoa wa Arusha, alimalizia kwa kuwashauri madereva hao kukagua kabla hawajaanza safari mizigo wanayokabidhiwa na abiria kwani wakati mwingine wanaweza wakakabidhiwa mzigo haramu kama vile madawa ya kulevya na kadhalika na kusababisha kuingia katika matatizo.
 
MWISHO

No comments:

Post a Comment