Wednesday, November 14, 2012

Tume ya Mabadiliko ya Katiba yaendelea na Awamu ya Nne ya kukusanya maoni

Tume ya Mabadiliko ya Katiba yaendelea na Awamu ya Nne ya kukusanya maoni

Tume ya Mabadiliko ya Katiba inatarajia kuendelea na awamu ya nne na ya mwisho ya mikutano yake na wananchi wa mikoa sita kuanzia siku ya Jumatatu, Novemba 19, 2012 hadi Jumatatu, Desema 19, 2012 kwa lengo la kukusanya maoni yao kuhusu Katiba Mpya.

 Mikoa hiyo ni Dar es Salaam, Arusha, Simiyu, Geita, Mara na Mjini Magharibi na kila siku kutafanyika mikutano miwili, wa kwanza utaanza saa 3:00 asubuhi – saa 6:00 mchana na kufuatia na mwingine utakaoanza saa 8:00 alasiri – saa 11:00 jioni.

 Taratibu zote za kuanza kazi ya kukusanya maoni katika mikoa iliyotajwa zimekamilika zikiwemo kuandaa ratiba na kuisambaza katika ofisi za mikoa, wilaya na Halmashauri za Manispaa na Wilaya husika. Wajumbe wa Tume na watumishi wa Sekretarieti wamejigawa katika makundi saba. Kila mkoa utakuwa na kundi moja isipokuwa Dar es Salaam ambao utakuwa na makundi mawili.

 Katika mkoa wa Dar es Salaam Tume imejigawa katika makundi mawili na siku hiyo ya Jumatatu itaanza na Wilaya za Temeke na Ilala. Katika wilaya ya Temeke, Tume itaanza na eneo la Keko wakati katika wilaya ya Ilala itaanza na eneo la Jangwani kwa mikutano itakayoanza saa 3:00 asubuhi. Kwa mikutano ya alasiri, wilayani Temeke mkutano huo utafanyika Chang’ombe na ule wa Ilala utafanyika Tabata.

 Kwa upande wa mkoa wa Arusha, Tume itaanza na Wilaya ya Karatu eneo la Mbulumbulu wakati mkoani Mara Tume itaanza katika Wilaya ya Tarime eneo la Bumera. Kwa mkoa wa Simiyu, Tume itaanza na Wilaya ya Busega eneo la Lamadi na mkoani Geita, Tume itaanza na Wilaya ya Chato eneo la Kachwamba. Kwa mkoa wa Mjini Magharibi, Tume itaanza katika Wilaya ya Magharibi.

No comments:

Post a Comment