Wednesday, November 14, 2012

DIWANI WA KATA YA BASHNET AKANUSHA UVUMI


 NA JOSEPH LYIMO MANYARA
DIWANI wa Kata ya Bashnet Wilayani Babati Mkoani Manyara,Laurent Surumbu Tara (NCCR Mageuzi) amekanusha vikali uvumi ulioenea wiki iliyopita kuwa amejiuzulu udiwani baada ya kuhama chama hicho na kujiunga na Chadema.
Wiki iliyopita katika Tarafa ya Bashnet na mji wa Babati kulienea habari kuwa Diwani huyo ambaye pia aligombea ubunge mwaka 2010 na kubwagwa na Vrajilal Jitu Son (CCM) ameondoka NCCR Mageuzi na kuhamia Chadema.
Akizungumza jana na Mwananchi,Tara alisema hata yeye alisikia hizo tetesi kuwa amejiuzulu nafasi hiyo ya udiwani baada ya kuondoka NCCR Mageuzi na kujiunga Chadema jambo ambalo siyo kweli.
Alisema huo ni mtazamo wa baadhi ya watu kuwa amehama chama chake na kujiunga na Chadema hivyo kupoteza sifa ya kuwa diwani kitendo ambacho alidai kuwa hakijafanyika.
“Hata mimi nimesikia kwa watu wakisema kuwa nimejiuzulu udiwani kata ya Bashnet baada ya kuondoka NCCR Mageuzi na kujiunga na Chadema,hayo ni maoni na mtazamo wao hivyo nimeshawishika kukanusha hilo,” alisema Tara.
Alisema kuwa bado anashikilia nafasi ya udiwani na hajafanya jambo hilo kwani endapo akifanya hivyo atatoa taarifa rasmi na kutamka hadharani kuwa amejiuzulu nafasi ya udiwani wa kata ya Bashnet kwa tiketi ya NCCR Mageuzi.
Mwaka 2010 Tara aligombea nafasi ya udiwani na ubunge wa Jimbo la Babati Vijijini ambapo aliangushwa na mbunge wa sasa Jituson lakini alikata rufaa Mahakama kuu akipinga kushindwa nafasi hiyo.
Pia,baada ya kupeleka kesi hiyo Mahakamani,Jaji Fatuma Massengi aliisikiliza na kutupa vipingamizi vyote alivyovitoa kwenye ushahidi wake ili Jituson afutiwe ubunge lakini alifikisha kesi hiyo Mahakama ya rufaa kupinga maamuzi hayo.
Hata hivyo,Majaji watatu waliosikiliza rufaa yake waliipinga na kudai kuwa Jituson alishinda ubunge kihalali hivyo ataendelea kuwa mbunge wa jimbo hilo hadi mwaka 2015 na Tara anatakiwa alipe gharama za uendeshaji kesi hiyo.
MWISHO.

No comments:

Post a Comment