Sunday, December 23, 2012

WAZIRI WA ZAMANI WA MIPANGO WA RWANDA AHUKUMIWA MIAKA 35 JELA

WAZIRI WA ZAMANI WA MIPANGO WA RWANDA AHUKUMIWA MIAKA 35 JELA
 
Na Nicodemus Ikonko, Hirondelle, Arusha

 Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda(ICTR) imemhukumu kifungo cha mika 35 jela Waziri wa zamani wa Mipango wa Rwanda,Augustin Ngirabatwara baada ya kumtia hatiani kwa mashitaka matatu ya mauaji ya kimbari.

Mahakama iliyokuwa inaongozwa na Jaji William Sekule kwa kauli moja imemtia hatiani ngirabatware kwa mashitaka ya mauaji ya kimbari, uchochezi na ubakaji kama uhalifu dhidi ya binadamu.

‘’Augustin Ngirabatware, mahakama imekuona una hatia kwa mauaji ya kimbari, uchochezi na ubakaji kama uhalifu dhidi ya binadamu,’’ Jaji Sekule alisema huku Ngirabatware akielekeza uso wake chini.
‘’Kwa uhalifu huu na kwa kuzingatia mazingira yote ya kesi hii, mahakama inakuhukumu kifungo cha miaka 35 jela,’’ alitamka Jaji Sekule.

Katika hukumu yake,mahakama imemtia hatiani Waziri huyo wa zamani kwa mauaji ya kimbari kutokana na ukweli kwamba alichochea, kusaidia na kuunga mkono mashambulizi na mauaji dhidi ya Watutsi katika wilaya yake ya Nyanyumba, mkoa wa Gisenyi, Kaskazini mwa Rwanda alikozaliwa. Alitekeleza uhalifu huo kwa kwa kupitia hotuba na vitendo vyake kwa kugawa silaha Aprili 7, 1994.

Mahakama ilibaini kwamba baadhi ya silaha zilizogawanywa kwa wanamgambo wa interahamwe zilitumika katika mashambulizi na mauaji na kwamba maneno yake na vitendo vyote kwa pamoja vilitoa hamasi kwa wanamgambo hao kufanya uhalifu huo katika wilaya ya Nyamnyumba.

Ngirabatware ambaye ni mkwe wa mtuhumiwa wa mauaji ya kimbari ambaye bado anasakwa vikali na ICTR alijitetea kwa kudai kwamba wakati mauaji hayo yanafanyika yeye hakuwepo wilayani kwake, utetezi ambao ulitupwa na mahakama.

Mfungwa huyo, ambaye kitaaluma ni daktari wa uchumi alitiwa mbaroni nchini Ujerumani Septemba 17,2007 na kisha kuhamishiwa Arusha, makao makuu ya ICTR Oktoba 8, 2008. Kesi yake ilianza kusikilizwa Septemba 29, 2009.

No comments:

Post a Comment