Friday, December 14, 2012

WAZAZI WAUKATAA UONGOZI WA SHULE YA MWANDETI


Joseph Ngilisho,Arumeru.
 
WAZAZI katika shule ya msingi ya Mwandeti iliyopo wilayani Arumeru,mkoani Arusha,wameukataa uongozi wa shule hiyo pamoja na kamati yake kwa madai ya ubadhilifu wa mali za shule na kueleza kuwa hawatoshiriki shughuli za maendeleo ya shule hiyo  hadi mkuu wa shule hiyo,Elibariki Laizer aondolewe.
 
Aidha wamemtuhumu mkuu huyo washule,kwenda kinyume na taratibu za uongozi wa shule hiyo kwa kuiendesha  kama mali yake,kujimilikisha mashamba ya shule na kuingia ubia wa shambe la shule lenye ukubwa ekari 6  na wafanyabishara bila kufuata utaratibu,kuchangisha michango hovyo kwa wanafunzi ikiwemo kuwalipisha faini wanapochelewa kufika shuleni ama kutofika kabisa.
 
Wakizungumza kwenye kikao cha shule kilichofanyika shuleni hapo jana,wazazi hao wa jamii ya wafugaji wamemtaka mwalimu huyo kuondoka shuleni hapo kwani pamoja na mambo mengine, kiwango cha taaluma kwa wanafunzi kimeshuka.
 
Mmoja wa wazazi hao,Lugion Leshiloi amesema kuwa mwalimu Laizer tangu ahamishiwe kwenye shule hiyo mwaka 2007 shule hiyo ambayo ilijengwa kwa msaada wa wazazi na mashirika mbalimbali, kwa sasa imechakaa,majengo yamepasuka na kuhatarisha maisha ya wanafunzi ,milango na vioo vya madirisha vimeibwa bila kuwemo uangalizi.
 
Alisema kuwa kwa sasa hawana imani na mwalimu huyo, kwani kuendelea kuwepo shuleni hapo kutaifanya shule hiyo ifilisike zaidi huku wanafunzi wakiumia kwa michango mbalimbali ambayo mara nyingi haina hata risiti,na kwamba wengi wa wanafunzi wameshindwa kuendelea na masomo kutokana na kero mbalimbali za mkuu huyo wa shule na kujikuta idadi ya wanafunzi kwa sasa  ikifikia 700 kutoka wanafunzi 1000 waliokuwepo.
 
‘’shule imekufa haina uangalizi ,majengo yamepasuka kila kona ,tunachotaka ni mwalimu mkuu na kamati yake waondoke,bila hivyo hatutatoa ushirikiano na shule hii’’alisem mzazi Samwel Mseyeke ambaye ni mwenyekiti mstaafu wa kijiji
 
Naye mzazi ,Jonas Klasian alimtuhumu mkuu huyo wa shule kwa kuwachangisha wanafunzi michango nya shilingi 1000 kila wiki huku wanaochelewa kufika shuleni hulipishwa shilingi 500 hadi 1000 na wale wanaoshindwa kufika kabisa shuleni kwa siku moja huwalazimu kulipa shilingi 2000 hadi 2500 huku akiwasisitiza wazazi ambao hawatoi michango ya watoto wao ,kuwaondoa watoto wao shuleni hapo.
 
Wazazi hao wamesusia taarifa ya mapato na matumizi ya mwaka 2011/12 iliyoandaliwa na mkuu huyo wa shule na kusomwa katika mkutano huo wakidai kwamba imechakachuliwa na imejaa ubabaishaji kwani idadi ya fedha zilizosomwa kutumika zimepandikiziwa na wanawasiwasi hazikutumika kwa matumizi hayo yaliyotajwa.
 
Akijibu tuhuma hizo mkuu wa shule huyo,Elibariki Laizer alisema kuwa tuhuma hizo  ni majungu ya wananchi hao zenye lengo la kumchafua huku akifafanua kwamba utaratibu kuingia ubia wa mashamba ya shule upo wazi kwani walifanya hivyo kwa lengo la kuwapunguzia mzigo wanafunzi wa kulima mashamba hayo muda wa masomo.
 
Akizungumzia suala la wazazi kukataa taarifa ya mapato na matumizi alisema kuwa fedha zote zilizoingia shuleni hapo zimetumika kama ipasavyo na hakukuwa na taarifa iliyopotoshwa na kwamba suala na shule kuchakaa ni wazazi ndio wameitelekeza na sio jukumu lake.
 
Mwisho.

No comments:

Post a Comment