Thursday, December 6, 2012

MEYA WA JIJI AWAONYA WAFANYABISHARA

Na Dotto Mnzava, Arusha.

MEYA wa jiji la Arusha, Gaudensi Lyimo amewaonya wafanyabiashara wote
wenye mabanda ya kuuzia bidhaa mbalimbali katika eneo la soko kuu
kuacha tabia hiyo ya kukodisha vibanda hivyo kwani kwa kufanya hivyo
ni kuwakandamiza watu wa kipato cha chini pamoja na kuipotezea
manispaa mapato.

Lyimo aliyasema hayo jana wakati akizungumza katika kikao cha siku
moja kilichowashirikisha wafanyabiashara hao pamoja na uongozi wa jiji
la Arusha kilichofanyika ukumbi wa halmashauri ya jiji la Arusha.

Alisema kuwa , hivi sasa uongozi wa jiji la Arusha watafanya ziara
katika soko hilo ili kubaini wamiliki halali wa vibanda hivyo, na
endapo watagundua kuwa vimekodishwa na wamiliki hawapo basi hatua kali
za kisheria zitachukuliwa na jiji hilo.

Aidha kikao hicho kililenga kujadili mbinu mbalimbali za kuboresha
soko hilo ikiwemo kubadilika kwa bei waliyokuwa wakilipia
wafanyabiashara hao zamani ya shs 6,000 kwa mwezi kwa kibanda hali
ambayo ilikuwa ikichangia jiji hilo kupata mapato kidogo kutoka kwenye
vibanda hivyo.

Hata hivyo alisema, baada ya kufanya uchunguzi wamebaini kuwa
wafanyabiashara wenye vibanda hivyo wamekuwa wakilipa manispaa kiasi
kidogo cha fedha huku wenyewe wakitoza kiasi kikubwa cha fedha kwa
wale ambao wamewakodishia vibanda hivyo, na kupata faida mara mbili.

Lyimo alisema kuwa, hivi sasa uongozi wa manispaa kwa kushirikiana na
wafanyabiashara hao wamekubaliana kulipa kiasi cha shs 30,000 kwa
mwezi kwa vibanda vya matunda na shs 42,000 kwa mwezi kwa vibanda vya
maduka katika vilivyopo katika soko hilo.


“ tumetangaza rasmi bei hizo mpya za kulipia mabanda katika soko kuu
na tumewashirikisha wafanyabishara hao na wamekubali , hivyo gharama
hizo zitaanza kutumika rasmi mwakani kwani bei ya zamani ilikuwa ni
kidogo sana”alisema Lyimo.

Pamoja na mambo mengine alitumia fursa hiyo kuwataka wafanyabiashara
hao kuhakikisha wao wenyewe wanatunza jiji la Arusha katika
kuhakikisha kuwa sheria zozote hazikiukwi badala ya kuwaachia manispaa
na mgambo wenyewe kwani wao pia ni walinzi katika maeneo yao ya kazi.



MWISHO.

No comments:

Post a Comment