Monday, December 31, 2012

TUMIENI FURSA IPASAVYO


 NA MWANDISHI WETU MANYARA

JAMII nchini imeaswa kutumia ipasavyo fursa zilizopo na zinazotolewa na Serikali au mashirika mengine ya ndani na nje ya nchi hususani shirika la kazi duniani (ILO) kwa kuwa wabunifu na kujituma ili waweze kujiendeleza kimaisha.

Hayo yameelezwa juzi mjini Kateshi wilayani Hanang’ mkoani Manyara na Ofisa Maendeleo ya mifugo na uvuvi wa wilaya hiyo Dk Tom Maeda,kwenye uzinduzi wa mpango wa ukuzaji wa ujasiriamali kwa vijana wenye kauli mbiu moto wa nyika.

Katika uzinduzi huo ulioandaliwa na asasi ya Disabled and Orphans Hope Centre (Dohoce) ya wilayani Hanang’ kupitia shirika la kazi duniani (ILO) Dk Maeda alisema huu ni wakati wa wajasiriamali nchini kuchangamikia fursa zilizopo.

Alisema wilaya hiyo ni sehemu ya jumuiya ya watanzania wenye kuwajibika kutekeleza malengo ya milennia na dira ya Taifa ya mwaka 2025 na mkakati wa kukuza uchumi na kuondoa umasikini (Mkukuta) namba mbili.

“Haya yote yanategemea kwa kiwango kikubwa utashi wa jamii hasa vijana kujituma,kuwa wabunifu na kupenda kujiajiri wenyewe kwa kutumia fursa zilizopo na zinazotolewa na Serikali na asasi za kijamii,” alisema Dk Maeda.

Naye,Mratibu wa Dohoce,Kianga Mdundo alisema takwimu zilizotolewa na Waziri wa kazi na ajira Dk Makongoro Mahanga,zinaonyesha kuwa watanzania walioajiriwa kwenye sekta rasmi ni asilimia 30,ajira Serikali asilimia tano,sekta zisizo rasmi asilimia 35 na wasio na ajira asilimia 30.

Mdundo alisema Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya mahesabu ya mashirika ya umma,Zitto Kabwe alisema wahitimu wa vyuo vyote nchini kwa mwaka ni 650,000 na wanaopata ajira ni 40,000 na 610,000 waliobaki wanakosa ajira.

“Kwa hiyo soko la ajira isiyo rasmi ndiyo inayotegemewa kuwa mkombozi wa vijana katika kujiletea maisha bora kwa kila mtanzania hivyo Dohoce imeamua kuwajengea uwezo jamii iliyopo wilayani Hanang’,” alisema Mdundo.

Kwa upande wake,mwezeshaji wa mafunzo hayo Julius Slaa alisema kada zilizopatiwa mafunzo hayo na kupatiwa cheti ni mafundi wa ushonaji,seremala, magari,pikipiki,waashi,mamalishe,wakulima,wafugaji na wasindikaji vyakula.

Slaa aliwataja wengine ni wakuzaji miche ya miti,wadau wa sokoni,wana harakati wa mazingira,wafugaji wa nyuki,taasisi za fedha,wasimamizi na waandaji wa mipango,wakuzaji miche ya miti,wana michezo na wana habari.

MWISHO.

No comments:

Post a Comment