Monday, December 10, 2012

ASKOFU ISANGYA AITAKA JAMII KUTUMIA ZAIDI UZAZI WA MPANGO

 Na Joseph Ngilisho,MERU
 
ASKOFU mkuu wa kanisa la  International Evangelism Center lililopo kijiji cha Sakila wilayani Arumeru mkoani hapa,Elihud Issangya ameitaka jamii kuacha tabia ya kuzaliana hovyo kama kuku,badala yake ifuate mpango wa uzazi wa majira,ili kuipunguzia mzigo serikali kukabii changamoto ya ajira na baa la njaa linalolinyemelea Taifa.
 
Isangya ametoa kauli hiyo leo katika mahafali ya 60 ya wahitimu wa masomo ya thiolojia ngazi ya diploma, katika chuo cha bibilia kilichopo Sakila ,ambapo jumla ya wahitimu 87 kutoka nchi mbalimbali za Afrika walihitimu masomo ya miezi 6 na kutunukiwa vyeti.
Askofu huyo alikemea tabia iliyozoeleka kwa jamii  kuzaa bila mpango, huku 
akitofautiana na maandiko matakatifu yaliyopo  kwenye bibilia yanayosema enendeni mkazaliane muijaze dunia,na kusema kuwa kadili hali inavyokuwa maandiko hayo yanapitwa na wakati, kwani idadi kubwa ya watu imeongeza umasikini wa familia na taifa kwa ujumla ukiwemo uharibifu wa mazingira unaosababsihwa na watu.
 
‘’watu wanashindwa kufahamu maana halisi ya maandiko ya bibilia yanayosema kuwa , nendeni mkaijaze dunia badala yake jamii imejenga tabia ya kuzaliana hovyo na halimaye kushindwa kuimudu familia huku watoto wakiteseka kwa kukosa chakula na elimu’’alisema
 
Askofu Isangya ambaye ni mwanzilishi wa makanisa ya kipentekoste wilayani humo,alisema kuwa taifa kwa sasa linakabiliwa sana na changamoto ya umaskini na ajira kwa wananchi wake na hivyo akaitaka jamii kuisaidia serikali kwa kupunguza idadi kuzaliana ili iweze kumudu watu wake.
 
‘’ jamani tusipende kuilaumu sana serikali kwa suala  ya ajira ,lazima na sisi tupunguze idadi ya kuzaa watoto wengi kwani kwa  kufanya hivyo serikali itaweza kukabili masuala ya njaa ,ajira na umaskini’’alisema Askofu.
 
Aidha aliwataka wahitimu hao kuzingatia yale yote waliojifunza na kwenda kuyatangaza kote duniani,waelimishe jamii kimwili na kiroho iweze kuishi kwa amani ,hata hivyo Askofu Isangya alijivunia chuo hicho kilichoanzishwa mwaka 1983 kwa kuhitimisha wanafunzi zaidi ya 6000 hadi kufikia mwaka huu ambao wamesaidia sana kutangaza amani hapa nchini na nchi za nje.
 
Kwa upande wao wahitimu hao wakisoma risala yao walisema kuwa wanakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo ya kukatika katika kwa umeme mara kwa mara hali inayowafanya kutotimiza ma`lengo yao.
 
Aidha walitaja changamoto ingine inayowakabili kuwa ni pamoja na ubovu wa miundo mbinu hasa bara bara ya kutoka maji ya chai hadi sakila hali inayowafanya kutopata huaduma zao za msingi pindi wanapozihitaji.
 
Hata hivyo walitaja mafanikio waliyowanayo tangu kuanzishwa kwa chuo hicho kuwa ni pamoja na kufanikiwa kuwachimba wananchi  visima 52 vya maji kwa ajili ya kukabiliana na upungufu wa maji pamoja na kuwa na mpango wa kuanzisha vyuo vingine  afrika ili viweze kuhudumia jamii nzima.
 
Mwisho

No comments:

Post a Comment