Monday, December 3, 2012

Mbunge Nassari wa CHADEMA Meru asusia Baraza la Madiwani

MBUNGE WA JIMBO LA ARUMERU MASHARIKI AKIAPA KUTUMIKIA WANANCHI WA JIMBO LAKE DODOMA,BUNGENI


Mbunge Nassari wa CHADEMA Meru asusia Baraza la Madiwani


Na Mary Mwita ,Arumeru .

MBUNGE wa Jimbo la Arumeru Mashariki  kupitia tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo Joshua Nasari  amesusia kikao cha Baraza la Madiwani  la  Halmashauri ya Meru ,baada ya kamati ya Uchumi ,Ujenzi  na Mazingira ,kuelezea nia ya kuwagawa viwanja kwa Vijana na wananchi  kupitia kata zao katika eneo la Soko la Tengeru.

Mbunge huyo alishangaza Baraza hilo ,baada ya kudai kuwa eneo hilo linapaswa kujengwa vitega uchumi na wawekezaji na siyo kupewa wananchi na Vijana   kama kamati ya uchumi ilivyoazimia na kukubaliwa na Baraza kuendelea na maamuzi hayo kwa kugawa viwanja kupitia kata.

Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani Frida Kaaya akielezea sakata hilo aliliambia Baraza hilo kuwa ameshangazwa na maamuzi ya Mbunge huyo ambaye alisema ni Diwani akiwa katika Baraza hilo ,kuwa alipaswa kukubali maamuzi ya Madiwani wenzake .

Alisema kuwa viwanja vinavyotarajiwa kugawanywa ni Viwanja 118 ,vitakavyojengwa kuzunguka soko na hivyo kufanikiwa kuwaondoa wafanyabiashara wanaopanga bidhaa chini .

Alifafanua kuwa kwa sasa Halmashauri hiyo imeanza kujikita kusaidia Vijana ,na kuwa kugawanywa viwanja hivyo kutalenga vikundi vya vijana ,ili waweze kufungua miradi ya maendeleo  kupitia vikundi,hatimaye kuweza kujikwamua katika uchumi na kuongeza kipato chao .

Diwani wa Kata ya Nkwarusambo akizungumza katika kikao hicho alimtaka Diwani Nassari kuheshimu maamuzi ya vikao  vya baraza na kushirikiana na madiwani wenzake kulewatea wananchi maendeleo na siyo kupinga kila kitu hata kama ni jambo jema .

Alisema kuwa Halmashauri hiyo ,inasifiwa kuwa na ushirikiano mzuri na wananchi ,na kuwa Mbunge huyo anatakiwa kuepuka migogoro isiyokuwa na na lazima .

Kwa upande wake Mbunge Nassari aliwaambia waandishi wa habari kuwa ,hakubaliani na kamati ya Uchumi na Baraza hilo ,kwa kuwa wamekiuka makubaliano ya awali ya kujenga vitega uchumi katika eneo ,na kudai kuwa anahisi kuna mchezo unataka kufanyika .


‘Mimi nina historia ndefu ,siku zote ,kuwa Viwanja vikitolewa wanaokuja kununua ni watu wa Arusha mjini ,watu wa Moshi na watu wa Meru hawaambulii chochote ,kwa hiyo ,ni mara kumi vikajengwa vitega uchumi ,ili wananchi waje wafanyie biashara badala ya kugawa kama Kamati ya Uchumi ilivyopendekeza “ anasema Nassari

No comments:

Post a Comment