Sunday, October 7, 2012

WAZINDUA MRADI MKUBWA WA MAJI


WAKAZI wa Kijiji cha Naisinyai Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara ambao baadhi ya watoto wao waliathirika kwa kupata ulemavu kutokana na kutumia maji yenye florine,wamezinduliwa mradi mkubwa wa maji na Mkuu wa mkoa huo.
Mradi huo wa maji ya kisima kirefu ambao umefadhiliwa na Kampuni ya TanzaniteOne umezinduliwa juzi na mkuu wa mkoa huo Elaston Mbwilo alipofanya ziara ya kuzindua miradi ya maendeleo kwenye kata ya Naisinyai.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo wa maji,Mbwilo aliwataka wakazi wa eneo hilo kuulinda mradi huo ambao utakuwa na manufaa makubwa kwa jamii na mifugo iliyopo kwenye eneo hilo. 
“Mradi huo unatakiwa kutunzwa kwani kupata mradi ni jambo linguine lakini kuutumia na kuutunza ni jambo lingine hivyo utunzeni na pia wapande miti na maua kwa ajili ya kutunza mazingira,” alisema Mbwilo.
Kwa upande wake,Ofisa Uhusiano msaidizi wa kampuni ya TanzaniteOne Halfan Hayeshi alisema mradi huo umedhamini na kampuni yao kwa gharama ya sh milioni 45 na una uwezo wa kutoa lita 30,000 kwa kila siku.
Hayeshi alisema wameweka mtambo kwenye mradi huo ambao hutengeneza maji safi na salama yafaayo kwa matumizi ya binadamu na watauhudumia kwa muda wa mwaka mmoja kisha wataukabishi uongozi wa kijiji uendeleze.    
Naye,Mwenyekiti wa Kijiji cha Naisinyai Taiko Kurian alisema watautunza mradi huo wa maji ambao una manufaa makubwa kwa jamii tofauti na awali ambapo maji yaliyokuwa yanatumiwa eneo hilo yaliwapa ulemavu baadhi ya watoto.
Kurian alisema kuwa kupitia mradi huo jamii itanufaika kwani baadhi ya watoto kabla ya kuanzishwa kwa mradi huo waliathirika kwa miguu yao kupinda,vichwa kuwa vikubwa na meno kuwa na rangi.

No comments:

Post a Comment