Friday, October 19, 2012

TUME YA TAIFA YA KUDHIBITI UKIMWI YATAKIWA KUANGALIA MAKUNDI MAALUMU

TUME YA TAIFA YA KUDHIBITI UKIMWI YATAKIWA KUANGALIA MAKUNDI MAALUMU

Na Queen Lema,ARUSHA

TUME ya taifa ya kudhibiti ukimwi, TACAIDS, imetakiwa  kuangalia makundi maalumu ya kijamii  kwa kuyafuata huko yaliko ili kuyapatia elimu ya kuepukana na ukimwi badala ya kuyaacha yakiendelea   kusambaza  na kuueneza na hivyo kufanya mapambano ya kuudhibiti na kupunguza ukimwi kuwa ngumu.

Rai hiyo imetolewa jana na Mkuu wa mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, katika hotuba ya ufunguzi ya warsha ya siku tatu iliyosomwa na Mkuu wa wilaya ya Arumeru, Deus mnasa,kuhusu  mpango mkakati wa awamu ya tatu wa mpango wa taifa wa miaka mitano ,2008/ 2012 na 2013 hadi 2017 .

Warsha hiyo inashirikisha wadau mbalimbali ambao ni wawakilishi wa Sekta ya Utalii, wafugaji , mashirika yasiyo ya kiserikali, wachimbaji madini, waishio na virusi vya ukimwi, asasi za kijamii, maafisa maendeleo ya jamii,maafisa mipango wa wilaya, na afisa uchumi kutoka Sekretariet ya mkoa wa Arusha , waratibu wa ukimwi wa halmashauri za wilaya  kutoka mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara .

Mkuu wa mkoa, amesema kwa kuwa semina hiyo inalenga utambuzi  wa mahitaji ya watu walioko katika hatari ya kupata maambukizi mapya  ya virusi, tume inatakiwa kuwafuata wale wote wanaojihusisha na ngono kwenye madanguro ,sanjari na vijana na kuwapatia elimu ya kujikinga na ukimwi kwa sababu ni makundi muhimu ya nguvu kazi.

“Maambukizi yatapungua iwapo tu makundi maalumu yakiwemo ya vijana na wasichana wanaofanya ngono katika madanguro watapatiwe elimu badala ya kuwaacha pembeni bila ya kuwasaidia”alisema magesa..

Magesa, ameitaka ,Tacaids, kutafuta  utaratibu mzuri wa  kuliandalia program maalum kundi linalofanya biashara ya ngono kwenye madanguro ili kuzuia ngono za hovyo ambazo zimeenea katika miji mbalimbali nchini   ili kuliepusha lisipate maambukizi  na kusambaza ukimwi kwa wengine kutokana na kutokuwa na elimu ya kujikinga na kuchukua tahadhari.

Tacaids ianzishe mpango wa kuwawezesha walioathirika na ukimwi kuanzisha miradi ya kiuchumi ili waweze kujiajiri  na kuachana na  utegemezi na omba omba hali ambayo inasababisha vifo vya haraka..

Pia Tacaisd, ihakikishe fedha za misaada zinazotolewa kwa waathirika na wagonjwa kupitia mashirika na asasi za kijamii zinawafikia walengwa ,badala ya watoa huduma ambao wanajinufaisha kwa  kununua magari ya kifahari na kujenga nyumba  huku walengwa wakiwa hawanufaiki .

Magesa, ameitaka Tacaids, kutumia tafiti za kitaalam  kuhusu ukimwi ziweze kusaidia kupunguza kiwango cha maambukizi badala ya tafiti hizo kubakia kwenye makabati bila kufanyiwa kazi na hilo ni jambo la kusikitisha na kushangaza.

Amesema iwapo Tacaids itatumia tafiti hizo  maambukizi mapya ya ukimwi ,ni wazi kuwa maambukizi yatapungua  na hivyo kuondoa unyanyapaa na vifo  tatizo ambalo limekuwa  likizikabili jamii mbalimbali hapa nchini.

“Umefika wakati Tacaids, kuaandaa utaratibu utakaowawezesha  waathirika na wagonjwa wa ukimwi kupata hati miliki ya mali zao ili kuepuka kunyang’anywa pindi wenza wao wanapofariki kutokana na mila potofu ambazo ni kandamizi zimekuwa zikiwanyima haki wajane badala ya kuwaacha waendelee kuishi kwa matumaini” alisema magesa.

Amezitaka  Kamati za ukimwi katika halmashauri    zishirikiane kikamilifu ili kupunguza maambukizi ya ukimwi ,kwa kuwa ukimwi ni vita  ya kibailojia iliyoletwa  kwa ajili ya kudhoofisha ukuaji wa uchumi katika mataifa yanayoeendelea.

Amesema serikali inataka kuwepo thamani halisi ya utekelezaji wa mpango wa mkakati wa mapamano ya ukimwi
Magesa,ameitaka tacaids, kutambua kwa nini maambukizi ya ukimwi yanaendelea kusambazwa  kutokana na vijana kujiingiza kwenye mapenzi wakiwa katika umri mdogo ,umaskini wa familia na  kutokulelewa kimaadili .

Amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika mapambano ya Ukimwi kutokana na kuwa na sera nzuri na mkakati wa makusudi hivyo Tacaids iongeze kasi zaidi na iangalie uwezekano wa kutoa elimu ya ukimwi kwenye vyuo vikuu ambako maambukizi yapo juu na kuliokoa kundi hilo ambalo limeaachwa .


Amesema kushuka kwa kiwango cha maambukizi kutawezesha taifa kupiga hatua ya mafanikio  kutokana na hatua ya kupunguza vichocheo na Tanzania bila ukimwi inawezekana

No comments:

Post a Comment