Thursday, October 11, 2012

MURUNYA AIBUKA KIDEDEA MWENYEKITI WA WAZAZI

CHAMA cha mapinduzi mkoa wa arusha  kimemchagua mbunge  wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki (EAC), Bernard Murunya,  kuwa Mwenyekiti wa Wazazi ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Arusha.

Aidha  uchaguzi huo uliofanyika kwenye ukumbi wa makao makuu ya CCM
Mkoa wa Arusha jana, Murunya aliwashinda wenzake watatu kwa kupata
kura 169 kati ya kura 334 zilizopigwa.

Msimamizi wa uchaguzi huo, Mary Chatanda, ambaye ni Katibu wa CCM Mkoa
wa Arusha na Mbunge wa Viti Maalum, aliwataja wagombea wengine katika
nafasi hiyo na kura walizopata kwenye mabano kuwa ni Edwin Seneu (1),
Mohammed Festo (68) na Musa Mkanga (69).

Kwa upande wa  nafasi ya Baraza Kuu la Taifa Wazazi/Mkutano Mkuu wa
CCM Taifa, aliyechaguliwa kuchukua nafasi hiyo ni John Pallangyo kwa
kupata kura 211 na kuwashinda Mbunge wa Viti Maalum, Namelok Sokoine
(112), Harun Matagane (6) na Baltazar Lymo (4).

Aidha nafasi ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa ilikwenda kwa
Fatuma Ngairo aliyepata kura 312 dhidi ya Mohammed Said Hassan (21) na
Jonas Lubulu (6) na kwa upande wa Baraza la Wazazi la Mkoa
ilinyakuliwa na Lucy Bongole (239) dhidi ya Mariam Athman Majengo (78)
na Filemon Amo (7).

Akizungumza baada ya kuchaguliwa kwake, Murunya alisema Jumuiya ya
Wazazi Mkoa wa Arusha, inakabiliwa na tatizo la ukata ambapo
ulisababisha ugumu kuwasafirisha wajumbe kutoka maeneo mbali mbali
wilayani kuhudhuria uchaguzi huo muhimu.

Hata hivyo, alisema chini ya uongozi wake atahakikisha kwamba
analitafutia ufumbuzi tatizo hilo ndani ya kipindi cha miaka miwili.

“Tutafanya mikakati kuhakikisha Jumuiya inaondokana na ukata, tutabuni
miradi ya kupata fedha na ndani ya miaka miwili mtakuja hapa mkiwa
kifua mbele,” alitamba.

MWISHO

No comments:

Post a Comment