Friday, October 5, 2012

WANAFUNZI WASHINDWA KUHUDHURIA MASOMO KWA KUHOFIA KUTEMBEA UMBALI MREFU WA MAJI


Na Queen Lema, MERU


IMEELEZWA kuwa kutokana na uhaba wa maji katika shule ya Sekondari Malula iliopo Wilayani Meru mkoani Arusha zaidi ya wanafunzi ishirini kwa kila siku wanashindwa kuhudhuria masomo kwa kuhofia kutembea umbali wa kilomita zaidi ya nne kwa ajili ya kutafuta maji

Akiongea na waandishi wa habari jana mkuu wa shule hiyo Bi Rehema Mroso alisema kuwa changamoto hali hiyo imedumu kwa miaka minne sasa

Bi Rehema alisema kuwa hali hiyo imekuwa ni kero kubwa sana kw wanafunzi wa shule hiyo kwani mara nyingine imekuwa ikisababisha wanafunzi kutumia muda mwingi sana kufikiria zaidi maji kuliko masomo ya kila siku.

Alifafanua kuwa wanafunzi hao wanalazimika hata kutembea umbali wa kilomita zaidi ya nne ili kutafuta maji wakati wa muda wa masomo hali ambayo ni chanzo kikubwa sana cha utoro wa wanafunzi shuleni hapo.

“kwa kweli wanafunzi kwa sasa wapo katika hali mbaya sana kwa kuwa wanshindwa kuwaza masomo na wanawaza umbali mrefu sana ambao wanatembea ili kutafuta maji ambapo ni kutoka hapa hadi katika uwanja wa ndege wa Kilimanjaro sasa hali hii kama haitaweza kudhibitiwa kwa haraka sana basi itachangia sana wanafunzi kukumbwa na mdororo wa elimu hasa katika maeneo haya ya Kingori, na Malula”aliongeza Bi Rehema.

Pia alisema mbali na kukabiliwa na changamoto wanafunzi kushindwa kuhudhuria masomo kutokana na kuhofia kubeba maji umbali mrefu pia shule hiyo inakabiliwa na changamoto kubwa sana ya uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi hali ambayo imeifanya shule hiyo kuweza kuajiri walimu ambao ni wanafunzi ili kuweza kuwasadia wanafunzi hao

Bi Rehema alisema kuwa wamelazimika kuajiri walimu wawili ambao ni wahitimu wa kidato cha sita waweze kuwafundisha wanafunzi hao masomo hasa ya Sayansi hali ambayo bado nayo ni changamoto kubwa sana ya wanafunzi kushindwa kufanya vema zaidi katika masomo yao hasa masomo ya hesabu na phizikia ambayo ndiyo kipaumbele kikubwa sana cha Serikali kwa sasa.

‘sasa hivi Serikali inakazia sana masomo ya Sayansi yaweze kupewa kipaumbele lakini kitu cha kushangaza ni kuwa hapa kwetu hatuna kabisa walimu na hawa walimu tulionao ni wanafunzi tu tena wa kidato cha sita sasa hili nalo linachangia sana kuweza kuwafanya wanafunzi wengi kukata tamaa na kushindwa kuyapa haya masomo kipaumbele kikubwa kama ilivyo kwa shule nyingine hasa kwenye masomo hayo”aliongeza Bi Rehema.

Alimalizia kwa kusema kuwa Serikali inatakiwa kutatua kwa haraka sana kero ambazo zinaikabili shule hiyo kwa kuwa shule hiyo ni moja ya shule ambayo inatumiwa na wakazi wengi hasa wa mpaka wa wilaya ya Meru na mkoa wa Kilimanjaro

MWISHO



No comments:

Post a Comment