Sunday, October 7, 2012

RAIS KAGAME ADAI ICC IMEAANZISHWA KWA AJILI YA WAAFRIKA


RAIS KAGAME ADAI ICC IMEAANZISHWA KWA AJILI YA WAAFRIKA
 
Na Hirondelle,Arusha
 
Arusha, Oktoba 05, 2012 (FH) – Rais wa Rwanda, Paul Kagame, Alhamisi amedai kwamba Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) yenye mamlaka ya kuwashitaki watuhumiwa wa mauaji ya kimbari,uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu, ni fimbo ya kisiasa iliyoanzishwa kwa lengo la kuwapiga waafrika.
‘’Wanaiita mahakama ya kimataifa lakini kwa kweli ni kwa ajili ya waafrika. Waafrika siyo lazima wale ambao wamefanya makosa, bali ni wale wanaowapinga,’’ Rais Kagame alisema mjini Kigali wakati akizindua Mwaka wa Mhakama wa 2012-2013 nchini humo.
Rais huyo alifafanua ’’ Wanatuambia, ooh watawaadhibu watu wanaojihusisha katika kusajili askari watoto lakini hawawasaki wale wanaowaua.’’
Kagame aliendelea ‘’Wapo watu wanaoua,wanaobaka na wanaofanya kila uhalifu.Hunyamaza tu juu ya hayo yote labda ni kwa sababu tu ndivyo waafrika wanavyotakiwa kuwa.’’
Rais huyo pia alizungumzia mgogoro unaoendelea Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) akidai kwamba serikali ya nchi hiyo na jumuia ya kimataifa ndiyo inayostahili kushutumiwa na siyo Rwanda.
Baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO) yameiomba Rwanda kuunga mkono juhudi za kumtia mbaroni Jenerali Bosco Ntaganda, ambaye anatakiwa na ICC kwa uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita.Lakini Rais Kagame amekuwa  wakati wote akidai kwamba nchi yake haina sababu yoyote ya kufanya hivyo.
NI/FK  

No comments:

Post a Comment