Sunday, October 7, 2012

MWENDESHA MASHITAKA, MAWAKILI WA UTETEZI WAKATA RUFAA KESI YA LUBANGA

MWENDESHA MASHITAKA, MAWAKILI WA UTETEZI WAKATA RUFAA KESI YA LUBANGA
 
Na Hirondelle,Arusha
 
Arusha, Oktoba 05, 2012 (FH) – Pande zote mbili, za utetezi na mwandesha mashitaka katika kesi ya kiongozi wa zamani wa wanamgambo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Thomas Lubanga, zimekata rufaa kupinga adhabu aliyopewa mshitakiwa huyo ya kifungo cha miaka 14 jela.
Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) iliyopo The Hague Uholanzi, Julai 10, 2012 ilimtia  hatiani Lubanga kwa uhalifu wa kivita kwa kuwasajili na kuwatumia watoto katika mapigano eneo la Ituri, Mashariki mwa DRC kati ya Septemba 1, 2002 na Augosti 13,2003. Wakati huo Lubanga alikuwa kiongozi wa kundi la waasi la UPC.
Wakati mwendesha mashitaka anapinga adhabu ya kifungo cha miaka 14 jela akitaka iongezwe, upande wa utetezi unapinga vyote viwili, kutiwa hatiani na adhabu aliyopewa.
Lubanga alitiwa mbaroni Kinshasa mwaka 2005 na kisha kuhamishiwa ICC, The Hague March 2006. Kesi yake ilianza kusikilizwa Januari 26, 2009.
ICC, ambayo ni mahakama pekee ya kudumu duniani ya kushughulikia kesi za mauaji ya kimbari, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu imeshotoa hati kadhaa za kukamatwa kwa wahalifu wa makosa kama hayo nchini DRC.
Nje ya Lubanga, wengine walioshitakiwa pia mbele ya mahakama hiyo ni pamoja na viongozi wengine wawili wa wanamgambo, Germain Katanga na Mathieu Ngudjolo ambao wanasubiri kutolewa kwa hukumu za kesi dhidi yao.

No comments:

Post a Comment