Friday, October 19, 2012

MGOGORO MKUBWA UNAFUKUTA

Joseph Lyimo,Arumeru

MGOGORO mkubwa unafukuta baina ya wakazi wa kitongoji cha Msikitini Kijiji cha Mikungani wilayani Arumeru na Mwenyekiti wa Kitongoji hicho wakimtuhumu kuruhusu kituo cha kulea watoto yatima kujengwa kwenye barabara wanayoitumia hivyo kuwa kikwazo cha maendeleo.

Wakizungumza jana kwenye kikao kilichoitishwa na Ofisa Tarafa wa Mbuguni Japhet Moirana wakazi hao walisema hawapingi maendeleo ya kituo hicho ila wanapinga uongozi wa kitongoji kuruhusu ujenzi huo na kufunga barabara yao.

Mmoja kati ya wakazi hao Hamad Ngoya alisema uongozi wa kitongoji hicho ulifanya makosa kuruhusu ujenzi wa kituo hicho kwenye barabara inayotumika tangu mwaka 1975 hivyo jengo hilo limejengwa hivi karibuni kwa makosa.

“Barabara ni maendeleo kwani hata nyumba ya mama wa Rais Jakaya Kikwete iliyopo Msoga Bagamoyo ilijengwa barabarani na akaruhusu ibomolewe na Tanroads hivyo siyo busara kujenga kituo hicho barabarani,” alisema Ngoya.

Naye,Lewis Msaiyo alisema hata kama kituo hicho kinataka kuziba barabara kwa sababu ya usalama wa watoto kugongwa na gari au pikipiki wangepaswa waweke matuta au ukuta kuliko kuziba barabara hiyo inayosaidia watu wengi.

Kwa upande wake,Tareto Dau alidai kuwa barabara hiyo ilitolewa bure mwaka 1975 na Mzee Tareto na Bakary Ngoya ili jamii ipite kwenye njia hiyo na kufuata huduma mbalimbali ikiwemo kununua bidhaa kwa duka la Fakhii na Ally Mnaro.

Zawadi Amiry alisema uongozi wa kituo hicho haukupanga mipango yake kwa ukamilifu kwani endapo wangetambua kuwa eneo la ekari moja walilonalo ni dogo wangejenga ghorofa kuliko kujenga kituo chao pembeni ya barabara.

Hata hivyo,Kiongozi wa kituo hicho Mchungaji Frank Lema alisema yeye hana ugomvi na mtu yeyote ila uamuzi wowote utakaochukuliwa na wakazi hao wenyewe wataukubali kwani awali walielezwa kuwa barabara hiyo haitumiki.

Naye,Ofisa Tarafa wa Mbuguni Japhet Moirana alisema sakata hilo linarudishwa kwenye mkutano mkuu kijiji cha Mikungani ndiyo wenye uamuzi wa mwisho na kudai kuwa awali alielezwa Serikali ya kijiji imekubali ujenzi huo eneo hilo.

Moirana alisema barabara hiyo iendelee kutumiwa na jamii hadi hapo itakapoamriwa vinginevyo na pia aliiasa jamii hiyo ikubali barababara hiyo iondolewe eneo hilo wazo lililopingwa vikali na wakazi hao.  

MWISHO.

No comments:

Post a Comment