Friday, October 19, 2012

MWENYEKITI WA UWT MKOA WA MANYARA AITAKA SERIKALI KUHARAKISHA MCHAKATO MZIMA WA EPZ

MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mkoa wa Manyara Dorah Mushi amesema Serikali inatakiwa kuharakisha uanzishaji wa eneo la uwekezaji wa biashara ya nje (EPZA) uliopo mji mdogo wa Mirerani.

Akizungumza juzi na wakazi wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro wakati alipopokelewa baada ya kuchaguliwa kushika nafasi hiyo Mushi alisema EPZA itakuwa tegemeo kubwa la Mirerani pamoja na madini ya Tanzanite.

“Mradi wa EPZA ni tegemeo kubwa kwa wakazi wa mji mdogo wa Mirerani na Simanjiro kwa ujumla kwani fursa za uchumi zitaongezeka na kusababisha watu wasitegemee madini ya Tanzanite peke yake,” alisema Mushi.

Alisema mradi huo ni wa muda mrefu na hatambui kikwazo kinachokwamisha kuanzishwa kwa mradi huo ambapo wakazi waliokuwa wanamiliki maeneo ya mradi huo walishakubali kuhama ili kuupisha.

“Jamii ya Mirerani na Simanjiro itanufaika kiuchumi kupitia EPZA kwani bidhaa na mazao yatakayozalishwa na wakazi hao ikiwemo madini ya Tanzanite, Tomarini ya kijani,gaineti,mifugo,ngozi yatafanya wapige hatua,” alisema Mushi.

Alisema ni muda mrefu sasa umepita bila eneo hilo kuendelezwa wakati ambapo ardhi ya kujengwa EPZA imeshatengwa na mji huo hivyo kusubiri Serikali kuanza kujenga eneo hilo.

Mwenyekiti huyo alisema kuwa watu wengi hasa wanawake wa eneo hilo watanufaika kutokana na mradi huo ambao umekuwa tegemeo kubwa lakini utekelezaji wake bado haujafanyika.

Alisema watu wamekuwa na maswali mengi kuliko majibu kuhusiana na mradi huo ambao ni tegemeo kubwa kwao lakini kupitia nafasi aliyonayo hivi saa atakuwa anawakumbusha viongozi wa Serikali juu ya hatima ya EPZA Mirerani.

MWISHO.

No comments:

Post a Comment