Tuesday, January 1, 2013

MBUNGE AKONAY ATETA KUHUSU MFUKO WA MAENDELEO


MBUNGE wa Jimbo la Mbulu Mkoani Manyara,Mustapher Akonaay (Chadema) amesema mfuko wa maendeleo wa jimbo hauusiani na bajeti ya halmashauri wilaya ya wilaya kwani mfuko huo unasaidia miradi iliyoibuliwa na jamii.

Akonaay aliyasema hayo kwenye Baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo lililofanyika juzi mjini Mbulu baada ya diwani wa viti maalum Agatha Tsuha (CCM) kuulizia kwa nini mfuko huo hausaidii ujenzi wa shule kwenye kata yao.

Mbunge huyo alisema mfuko wa maendeleo wa jimbo kazi yake kubwa ni kuchochea maendeleo ya jamii katika miradi mbalimbali iliyoibuliwa hivyo haishirikiani na bajeti inayopitishwa na madiwani wa halmashauri ya wilaya.

“Kama kuna diwani anataka kusimamia mfuko huu agombee ubunge kwani kazi yake ni kuchochea maendeleo iliyobuniwa na jamii na kuongezewa uwezo na hausimamiwi na madiwani kama mnavyofikiri,” alisema Akonaay.

Alisema kupitia mfuko huo kata mbalimbali alizozitembelea za wilaya hiyo zimefaidika nayo ikiwemo kupatiwa mabati ya kuezekea shule za msingi na sekondari na ataendelea kuzisaidia kata hizo kupitia mfuko huo.

Alisema lengo la mfuko huo ni kuzijengea uwezo zaidi kata ambazo zimeibua miradi yao na kuonana na ofisi ya mbunge wakiorodhesha mahitaji yao ambayo kwa namna moja au nyingine wanaweza kunufaika nao.

Naye,Diwani wa kata ya Daudi,Paul Sulle (Chadema) alihoji kitendo cha hospitali ya wilaya hiyo kutopatiwa dawa na kudai kuwa hujuma zinafanyika kwa vile mbunge anatokea chama cha upinzani.

“Hatuelewi sababu ni nini hadi kukosekana kwa dawa kwenye hospitali ya wilaya,ambayo inategemewa na watu wengi,je kuna hujuma zinafanyika kwa sababu diwani na mbunge wanatokea Chadema au kuna nini?” alihoji Sulle.

Hata hivyo,Makamu Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo,Joseph Mandoo alisema upungufu wa dawa hospitalini umeshapatiwa fumbuzi baada ya uongozi wa wilaya hiyo kufuatilia suala hilo bohari kuu la dawa (MSD).

MWISHO.

No comments:

Post a Comment