Wednesday, January 9, 2013

MERU WAPATA HASARA YA MILIONI 30 KUTOKANA NA WAWEKEZAJI KUKIMBILIA KWENYE MPANGO WA EPZ


MERU WAPATA HASARA YA MILIONI 30 KUTOKANA NA WAWEKEZAJI KUKIMBILIA KWENYE MPANGO WA EPZ

Na Queen Lema,MERU

HALMASHAURI ya Meru Mkoani Arusha imepata hasara ya zaidi milioni 30 kwa kipindi cha miaka miwili mara baada ya kukosa kodi katika mashamba makubwa mawili yaliopo ndani ya halmashauri ambapo mashamba hayo yameingia katika mpango rasmi wa maendeleo ya uchumi na viwanda(EPZ)

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Trasias Kagenzi wakati akiongea na Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo katika kikao cha kupitisha bajeti ya Halmashauri hiyo mapema jana.

Kagenzi  alisema kuwa Halmashauri  hiyo imepata hasara ya ukosefu wa kodi kutoka kwa wawekezaji wawili ambao wameingia katika mpango huo wa EPZ ambao walikuwa wanachangia kodi kwa kiasi cha Milioni kumi na tano kwa mwaka.

Aliongeza kuwa  Wawekezaji  wa mashamba hayo  ambao wamehamia katika mpango huo ni pamoja na Doll Esatate, huku Mwekezaji mwingine akiwa ni Delka Bruine ambapo walikuwa wanchangia kiwango kikubwa sana cha kodi hali ambayo imesababisha mapungufu makubwa sana.

Alisema kuwa  hasara hiyo ya Mamilioni ya fedha inachangia sana Halmashauri hiyo kushindwa kufikia malengo yake mbalimbali ambayo wamejiwekea lakini pia mpaka sasa wameshabuni chanzo mbadala ambacho kitaweza kufuta kwa kiwango hasara hiyo kubwa ambayo imetokana na wawekezaji kujiunga na mpango wa EPZ

“hapo awali tulikuwa tunachukua kiasi cha Milioni 15 kwa wawekezaji hawa wawili lakini kwa miaka miwili tumekosa kodi zao kwa kweli hii ni hasara kubwa sana nah ii pia tutaitumia kama changamoto hata kwa hawa wengine ambao nao wanampango wa kujiunga na EPZ kwani kama tusipokuwa wajanja na tukabuni aina mpya ya vyanzo vya mapato basi halmashauri itakuwa katika hali tete”aliongeza Kagenzi

Katika hatua nyingine alisema kuwa mbali na kukosa Milioni 30 kama kodi lakini mpango huo utaweza kuwanufaisha watu wengi hususani Vijana ambapo kwa awali utatoa ajira kwa Vijana zaidi ya 5000 huku hali hiyo ikichangia kwa  kiwango kikubwa sana hata Ukuaji wa Uchumi wa  Meru

Kagenzi alifafanua kuwa wananchi wa Meru wanatakiwa kutumia vema fursa ambazo zipo na wahakikishe kuwa kupitia fursa hizo  na wao wanakuwa wabunifu kwa kuweza kujiandaa hata kuanzia sasa kuboresha bidhaa ili ziweze kuendana na soko la Nchi jirani

MWISHO

No comments:

Post a Comment