Joseph
Lyimo,Babati
WAGONJWA
wanaopata matibabu kituo cha Afya Magugu Wilayani Babati Mkoani Manyara
wameulalalamikia uongozi wa kituo hicho kutoweka mazingira safi kwani uchafu umekithiri hadi kusababisha
kunguni kuenea vitandani.
Kutokana
na hali hiyo wagonjwa hao walidai kuwa wanafika kwenye kituo hicho wakiwa wana
maradhi tofauti na wana rudi majumbani wakiwa na magonjwa tofauti
yanayosababishwa na kunguni hao walioenea kwenye kituo hicho.
Wagonjwa
hao waliyasema hayo walipotembelewa na waandishi wa habari wa mkoani Manyara
waliokuwa kwenye mafunzo ya kuandika habari za vijijini yaliyoandaliwa na Umoja
wa Vilabu vya Waandishi nchini UTPC.
Wagonjwa
hao waliwaeleza waandishi walioongozana na mwezeshaji wa mafunzo hayo Mhariri
Mtendaji wa gazeti la Mwanaspoti linalotolewa na kampuni ya Mwananchi (MCL)
Frank Sanga kuwa Serikali iangalie hali hiyo.
Mmoja
kati ya wagonjwa hao Amina Juma alisema kila wakati wanapopata maradhi na
kulazwa kwenye kituo hicho wanapata wakati mgumu kutokana na kung’atwa na
kunguni wanaoenea katika vitanda wanavyovilalia.
“Pamoja
na hayo pia tuna kero kubwa ya ukosefu wa vitanda kwani tunalala watu wawili
katika kitanda kimoja hivyo tunaumia sana na kupata maumivu kutokana na kubanana
wakati wa kulala,”alisema Juma.
Naye,Zulfa
Shaban mkazi wa Gichameda alisema kutokana na hali ya uchafu kukithiri baadhi
ya wagonjwa wanahofu ya kufika katika kituo hicho ili kupatiwa huduma ya afya
wakizikumbuka kunguni zilizopo eneo hilo.
Hata
hivyo,Mganga kiongozi wa kituo hicho cha afya Magugu Dk Abdalah Abasi alisema
kunguni hizo zinaletwa na wagonjwa wenyewe kutoka majumbani mwao na
kuzihamishia kwenye wodi za kulaza wagonjwa.
“Kwa
kweli kunguni zinaletwa na wagonjwa wenyewe na wasiwasingizie wafugaji wa
kibarbaig kuwa wanaleta kunguni kwani tumekuwa tunapiga dawa wodini baada ya
wiki kunguni wanaletwa tena na wagonjwa,” alisema Dk Abasi.
Pia,alisema
wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa fedha na wanashindwa kuongeza vitanda
na kununua dawa za kutosha bohari kuu (MSD) hivyo jamii inatakiwa ijiunge na
mfuko wa afya CHF ili waletewe dawa nyingi zaidi.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment