Katika harakati za kuhakikisha
kwamba Afrika Mashariki inaendelea kuwa salama kwa uwekezaji, Jumuia ya
Afrika Mashariki (EAC) na Shirika la Polisi la Kimataiafa(INTERPOL)
wamekubaliana kushirikiana katika masuala ya usalama kwa manufaa ya
pande zote mbili.
Katibu Mkuu wa EAC, Dk. Richard
Sezibera alisema hayo alipokutana na kiongozi mwenzake wa INTERPOL,
Roland Noble kwenye Mkutano wake Mkuu wa 18, mjini Roma, Italia,
mwishoni mwa wiki, Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki
linaripoti.
‘’Kadiri mtangamano wa EAC
unavyozidi kujiimarisha na kupanuka, na uhuru unaopatikana kutokana na
utekelezaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja, mambo hasi ya uhalifu kama
vile madawa ya kulevya, usafirishaji haramu wa binadamu, bidhaa feki na
uhalifu wa mtandao nao unaongezeka na hivyo haunabudi kupigwa vita kwa
nguvu zote,’’ alisisitiza Dk. Sezibera.
Katibu Mkuu huyo wa EAC
aliongeza kwamba nafasi ya INTERPOL ina umuhimu wa pekee katika kusaidia
EAC kutekeleza mikakati yake ya amani na usalama.
INTERPOL na EAC zinatarajiwa kutiliana saini mkataba wa maelewano kuhusu ushirikiano huo hivi karibuni.
Kwa mujibu wa taarifa ya
Sekretariet ya EAC, majadiliano baaina ya taasisi hizo mbili juu ya
masuala ya ushirikiano yalianza tangu mwaka 2009 kwa lengo la kutumia
nafasi zilizopo kuimarisha ufanisi wa utendaji kazi katika taasisi hizo
kwa masuala ya usalama katika kanda hiyo.
Kwa sasa nchi zote tano
wanachama wa EAC; Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda na Burundi,
zinawasiliana na INTERPOL katika ngazi ya ofisi ya kanda.
Wakati huo huo Rais wa Mfuko wa
Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo(IFAD) wenye makao yake makuu mjini
Roma, Italia, Kanayo Nwanze amezihakikishia kuziunga mkono nchi
wananchama wa EAC katika juhudi zke za kupambana na njaa ili
kujitosheleza kwa chakula.
Alisema EAC itapewa kipaumbele
cha kwanza katika mipango yake kwa mwaka 2013 na kuongeza kuwa maafisa
waandamizi wa shirika lake wako tayari kujadili maeneo ya kushirikiana
ili kuongeza uzalishaji wa chakula katika kanda hiyo.
No comments:
Post a Comment