MBUNGE wa Jimbo la Mbulu Mkoani
Manyara,Mustapher Akonaay (Chadema) amesema mfuko wa maendeleo wa jimbo
hauusiani na bajeti ya halmashauri wilaya ya wilaya kwani mfuko huo unasaidia
miradi iliyoibuliwa na jamii.
Akonaay aliyasema hayo kwenye Baraza
la madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo lililofanyika juzi mjini Mbulu baada
ya diwani wa viti maalum Agatha Tsuha (CCM) kuulizia kwa nini mfuko huo
hausaidii ujenzi wa shule kwenye kata yao.
Mbunge huyo alisema mfuko wa
maendeleo wa jimbo kazi yake kubwa ni kuchochea maendeleo ya jamii katika
miradi mbalimbali iliyoibuliwa hivyo haishirikiani na bajeti inayopitishwa na
madiwani wa halmashauri ya wilaya.
“Kama kuna diwani anataka kusimamia
mfuko huu agombee ubunge kwani kazi yake ni kuchochea maendeleo iliyobuniwa na
jamii na kuongezewa uwezo na hausimamiwi na madiwani kama mnavyofikiri,”
alisema Akonaay.
Alisema kupitia mfuko huo kata
mbalimbali alizozitembelea za wilaya hiyo zimefaidika nayo ikiwemo kupatiwa
mabati ya kuezekea shule za msingi na sekondari na ataendelea kuzisaidia kata
hizo kupitia mfuko huo.
Alisema lengo la mfuko huo ni
kuzijengea uwezo zaidi kata ambazo zimeibua miradi yao na kuonana na ofisi ya
mbunge wakiorodhesha mahitaji yao ambayo kwa namna moja au nyingine wanaweza
kunufaika nao.
Naye,Diwani wa kata ya Daudi,Paul
Sulle (Chadema) alihoji kitendo cha hospitali ya wilaya hiyo kutopatiwa dawa na
kudai kuwa hujuma zinafanyika kwa vile mbunge anatokea chama cha upinzani.
“Hatuelewi sababu ni nini hadi
kukosekana kwa dawa kwenye hospitali ya wilaya,ambayo inategemewa na watu
wengi,je kuna hujuma zinafanyika kwa sababu diwani na mbunge wanatokea Chadema
au kuna nini?” alihoji Sulle.
Hata hivyo,Makamu Mwenyekiti wa
halmashauri ya wilaya hiyo,Joseph Mandoo alisema upungufu wa dawa hospitalini
umeshapatiwa fumbuzi baada ya uongozi wa wilaya hiyo kufuatilia suala hilo
bohari kuu la dawa (MSD).
MWISHO.
No comments:
Post a Comment