ELIMU YA MAZINGIRA IANZIE KUANZIA NGAZI YA CHEKECHEA ILI KUOKOA JAMII DHIDI YA UHARIBIFU WA MAZINGIRA
Na MWANDISHI WETU, ARUSHA
IMEELEZWA kuwa endapo kama wanafunzi kuanzia ngazi ya
madarasa ya awaali watafundishwa na kupewa mbinu za kutunza mazingira
yanayowazunguka basi wanafunzi hao
watakuwa ni wataalamu wazuri wa kutunza
na kuthamini mazingira tofauti na sasa ambapo bado wapo baadhi ya wananchi wa
maeneo mbalimbali ambao wanaharibu vibaya vyanzo vya mazingira kwa kushirikiana
na watoto wao kwa kuwa hawana elimu ya kutosha huku watoto hao wakiona kuwa
uharibifu wa mazingira ni jambo la
kawaida sana.
Wito huo umetolewa mjini Arusha na Mratibu wa shirika la
Roots and Shoots,Bw Japhet Mwanangombe mapema wiki hii wakati akiongea na
wanafunzi ambao ni wadau wa mazingira (waelimishaji
rika) zaidi ya 190 kutoka katika shule mbalimbali za msingi na Sekondari kwa mkoa wa Arusha
Bw Mwanangombe alisema kuwa
kwa sasa ni vema kama somo la
elimu ya mazingira likafanywa kama somo lenye umuhimu mkubwa sana kwa wanafunzi
kuanzia wale wa madarasa ya awali kwa
kuwa kama wanafunzi hao wataweza kupata vema elimu hiyo basi watakuwa ni
mabalozi wazuri sana wa mazingira tofauti na sasa ambapo kwa somo hilo linatolewa na wadau mbalimbali huku
hata baadhi ya wazazi na wakuu wa shule wakiona kuwa ni moja ya elimu ambayo
haina tija sana kwenye Jamii
Alisema kuwa elimu hiyo inapoanzia kuanzia ngazi ya chini
kabisa itaweza kuwafanya watoto hata kuweza kuyapenda na kuyathamini mazingira
ya Nchi na hivyo kukemea vikali sana
suala zima la uharibifu wa mazingira ambapo mara nyingine unafanywa na wazazi
au walezi wao kwa kuwa hawana elimu ya kutosha juu ya madhara ya uharibifu huo.
“tuseme tusemavyo tuende tuendako hii elimu ni ya muhimu sana kwenye Nchi yetu
tena hususani Vijijini lakini kama tutakuwa tunaendelea kusema kuwa tuyapende
mazingira huku hiki kizazi kikiwa hakiambiwi madhara ya uharibifu bado
hatusaidii Jamii ila hawa watoto wetu wanatakiwa wapewe elimu hii ili kama hata
wazazi wao hawana elimu ya kutosha basi
watawafundisha wazazi wao na hapo mazingira yataweza kuhifadhika tena
hasa yale ya Vijijini,Aliongeza Bw Mwanangombe.
Mbali na hayo Mratibu huyo alisema kuwa nao wakuu wa shule
wanatakiwa kuhakikisha kuwa wanatoa vipaumbele sanjari na uanzishwaji wa vitalu
vya miti ndani ya shule zao na kuachana na tabia ya kuwakataza baadhi ya
wanafunzi ambao wanamsukumo na suala zima la mazingira kwani kwa hali hiyo
wanachangia sana uharibifu wa mazingira ambapo madhara kwa sasa yametanda sana
ndani ya uso wa dunia.
Aliwataka wadau hao wa elimu ambao ni wakuu wa shule
kuhakikisha kuwa kila shule inakuwa hata na mashindano ya kimazingira ambayo
yataweza kuwapa wanafunzi fursa ya kuyapenda na kuthamini mazingira hasa kwa
njia ya upandaji wa miti hali ambayo nayo itafanya jamii kuepukana na ukame
ambao kwa sasa upo kwenye baadhi ya vijiji
na kutokana na ukame huo unasababisha hata vifo vya wanyama na mimea
kukauka.
Nao wanafunzi hao walisema kuwa pamoja na kuwa Shirika hilo linawawezesha katika masuala mbalimbali hasa ya
utunzaji wa mazingira basi jamii nayo hasa kupitia kwenye Familia zao na
Serikali za mitaa zinatakiwa kuwapokea na kuacha tabia ya kuwadharau kutokana
na kuwa na umri mdogo kwani kupitia kwao wanaweza kufanya mabadiliko makubwa sana katika sekta hiyo ya
mazingira.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment