Wednesday, November 14, 2012

WANANCHI TOENI MAONI YENU KWENYE MCHAKATO WA KATIBA-WAJUMBE MANYARA


 JOSEPH LYIMO,MANYARA
WANANCHI wametakiwa kutoa maoni yao kwenye mchakato wa uanzishwaji wa katiba mpya ili waandishi wa habari waweze kutambulika kwenye katiba mpya na kuwa mhimili wa nne wa Nchi.
Hayo yameelezwa jana na wajumbe wa Serikali ya kijiji cha Magugu Wilaya ya Babati Mkoani Manyara walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari wa mkoa huo waliokuwa kwenye mafunzo ya kuandika habari za vijijini.
Waandishi hao walitembelea kijiji hicho wakiwa na mwenzeshaji wa mafunzo hayo,Frank Sanga Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mwanaspoti linalotolewa na kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) na kuandaliwa na Umoja wa Vilabu vya waandishi wa habari nchini (UTPC).
Wajumbe hao walisema wananchi wanapaswa kutambua mchango wa waandishi wa habari kwani wamekuwa watetezi wa jamii katika masuala mbalimbali yanayowakabili hivyo watoe maoni yao ili wawe mhimili wa nne.
Mmoja kati ya wajumbe hao Nyange Swalehe alisema waandishi wa habari wakipatiwa nafasi ya kuwa mhimili wa nne wa nchi watakuwa na uwezo zaidi wa kufanya kazi zao hivyo jamii itainuka kiuchumi na kutetewa kila wakati. 
Naye,Aron Macha alisema waandishi wa habari mara nyingi wamekuwa watetezi wa wanyonge hivyo wanawashukuru waandishi wa habari wa mkoa wa Manyara ambao wamewatembelea ili kusikiliza maoni yao.
“Tunawashukuru waandishi kuja kijiji kwetu kuandika changamoto na kero zinazotukabili kwani kila mara mnakuwa mpo mjini sasa tumeona kuwa hamli nyama ya kuku tu mmekuja kwetu kula na mboga za majani,” alisema Macha.
Kwa upande wake,Mwenyekiti wa kijiji cha Magugu Omary Mazinde alisema waandishi wa habari ni daraja baina ya wananchi na viongozi kwani kupitia kalamu zao changamoto na matatizo yaliyopo vijijini yanatambulika.
“Wananchi wa vijijini wanakosa fursa ya kusikika kutokana na kutokuwa na sauti za kuwafikishia kilio chao hivyo mara nyingi wanabaki kulalamika tu ila sisi tunawashukuru waandishi wa Manyara kwa kututembelea,” alisema Mazinde.
MWISHO.

No comments:

Post a Comment