Na Joseph Lyimo,MANYARA
KAMPUNI ya Ujenzi ya China ya Chico imejitolea
kutumia sh50 milioni kwa ajili ya ukarabati wa kituo cha magari ya kubeba abiria
kilichopo mjini Babati Mkoani Manyara ili kumaliza kero iliyopo kituoni hapo mvua
zinaponyesha.
Akizungumza juzi mjini Babati mbele ya viongozi
wa halmashauri ya wilaya hiyo wakati wakuanza kukarabatiwa kituo hicho,msemaji
wa kampuni ya Chico,Yan Wangting alisema lengo lao ni kutoa msaada kwa jamii
inayotumia kituo hicho.
Wangting alisema Mwenyekiti wa halmashauri ya
mji wa Babati,Mohamed Farah alizungumza naye na kuomba msaada wa kukarabatiwa
kituo hicho ambacho wakati mvua zikinyesha kunakuwa na kero ya madimbwi ya
maji.
Alisema kuwa ili kushiriki shughuli za
maendeleo,kampuni ya Chico imejitolea kufanya kazi hiyo bure ili kuondoa adha
ya wasafiri na magari yanayotumia kituo hicho hasa kero ya maji wakati mvua
zinaponyesha.
“Lengo la kampuni ya Chico kukarabati kituo
hiki ni kutoa mchango wetu kwa jamii ambapo tunatarajia kutumia siku tatu hadi
nne katika kuhakikisha kuwa kazi hii imekamilika na kituo kinaendelea
kutumika,” alisema Wangting.
Kwa upande wake,Mwenyekiti wa halmashauri ya
mji huo,Mohamed Farah aliipongeza kampuni hiyo kwa kujitolea kukarabati kituo
hicho cha mabasi cha mjini Babati ili kiweze kutoa huduma ipasayo ya usafiri
mjini hapo.
“Tunaishukuru kampuni ya Chico kwa kuamua
kutukarabatia stendi yetu na wananchi wasiwe na wasiwasi wala hofu ya kuona
ukarabati ukiendelea ila mnapaswa kutambua huu ni msaada tu na siyo
vinginevyo,” alisema Farah.
Alisema hivi sasa magari ya usafiri ya mji huo
yanatoa huduma hiyo kwenye uwanja wa mpira wa miguu wa Kwaraa kwa muda wote
ambapo ukarabati wa kituo ukiendelea hivi sasa.
Naye,Kaimu Mkurugenzi wa mji wa Babati,Winnie
Kijazi alisema ili kuunga mkono msaada huo uliotolewa na kampuni ya Chico,jamii
inapaswa kutunza mradi huo pindi utakapokamilika.
“Tunaishukuru sana kampuni ya Chico kwa kutukarabatia
kituo hiki na tunapaswa kuuenzi msaada huu kwa kuitunza miundombinu yetu ya
kituo chetu ili kiweze kutunufaisha kwa muda mrefu zaidi,” alisema Kijazi.
Kampuni ya Chico ndiyo iliyojenga barabara ya
Minjingu-Babati ambapo mwanzoni mwa mwezi huu,Rais Jakaya Kikwete aliizindua
barabara hiyo ambayo imerahisisha usafiri wa kutoka mkoani Manyara hadi Arusha.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment