PICHANI NI KAMANDA WA POLISI MKOA WA ARUSHA,PICHA NA MAKTABA YA MALKIA WA HABARI.
WATAKIWA
KUFAHAMIANA ILI WAWEZE KUSAIDIANA KATIKA
KUKOMESHA UHALIFU
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha,
Mkuu wa Jeshi
la polisi Wilaya ya Arusha Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Gilles Muroto amewataka
wakazi wa Kata ya Sokoni One kila mmoja ajitahidi kufahamiana na jirani yake
ili waweze kusaidana pindi uhalifu unapotokea katika eneo lao.
Hayo aliyasema
juzi katika mkutano kati ya Jeshi la polisi, viongozi wa kata hiyo na askari wa
vikundi vya ulinzi shirikishi ambao ulifanyika katika shule ya Msingi Sokoni
One iliyopo Jijini hapa.
Muroto alisema
kwamba, kuishi katika nyumba yenye “geti” kubwa ambayo inakuwa na mlinzi pamoja
na mbwa si sababu ya kutovamiwa na wahalifu kwani wapo wengi ambao wanaishi
maisha kama hayo lakini wanavamiwa na wezi au
majambazi.
Alisema si
vizuri kwa majirani kuishi kwa kujitenga kwani jirani ndio mtu wa kwanza kukupa
msaada pindi uvamizi unapotokea
ikizingatiwa kwamba maeneo mengi yana matatizo ya miundo mbinu kama vile
ufinyu wa barabara ya magari hivyo ni vigumu kwa askari wa Jeshi la polisi
kuyafikia kwa uharaka.
Akitolea
ufafanuzi tatizo la msiri kujulikana Mrakibu huyo Mwandamizi wa Jeshi la Polisi
alisema kwamba, kwa sasa Jeshi la Polisi limeweka utaratibu mzuri wa kupokea
taarifa toka kwa wasiri ambapo uwa wanakwenda moja kwa moja katika ofisi za
viongozi wa Jeshi hilo na kuwapa taarifa ambayo nayo inafanyiwa kazi kwa
usiri, lakini akaonya baadhi ya watoa
siri wengine uwa wanawasimulia watu wao wa karibu hali inayochangia kujulikana
na wale wanaowafichua.
Katika kuboresha
utendaji kazi wa vikundi hivyo, alisema kwamba ni vyema askari hao wakawa na
sare maalum badala ya kufanya doria wakiwa wamevaa kiraia hali ambayo ni hatari
kwao na pia inawatia wasiwasi hata wanaohojiwa.
Naye Mkuu wa
Kitengo cha Polisi Jamii mkoa wa Arusha Mrakibu wa Polisi Mary Lugola aliwataka
wananchi watoe ushirikiano kwa vikundi hivyo vya ulinzi shirikishi pamoja na
Jeshi la Polisi katika kutoa kutoa taarifa zinazohusu uhalifu na wahalifu
wenyewe.
Alisema ana
imani na vikundi hivyo kwa kuwa vijana wanaochaguliwa uwa tabia zao zinakuwa
zimetathminiwa kwa undani kupitia viongozi wa mitaa hadi kata.
Aliwataka askari
hao waendeleze ari ya Utendaji kazi waliyonayo na uaminifu pamoja na
kutojichukulia sheria mkononi hali ambayo itasababisha jamii izidi kuwaamini
zaidi.
Alimalizia
kuwaelimisha askari hao kwa kuwaahidi kuwatembelea mara kwa mara katika eneo hilo na maeneo mengine
ili mafunzo hayo yasambae kwa kila mwananchi hali ambayo itasaidia kujenga
ushiriano mkubwa baina ya wananchi, Jeshi la polisi na vikundi vya ulinzi
shirikishi.
Mpango wa uundaji
wa vikundi vya ulinzi shirikishi ulianzishwa Mwaka 2006 na Jeshi la Polisi
nchini, ambao kwa kiasi kikubwa unasaidia kuwashirikisha moja kwa moja wananchi
kushiriki katika suala nzima la ulinzi wa wao wenyewe pamoja na mali zao badala
ya kuliachia Jeshi hilo pekee.
No comments:
Post a Comment