Picha ya kwanza ni Makamu wa Kwanza wa Rais
wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akizindua Ripoti ya Idadi ya Watu
Duniani kwa mwaka 2012, huko Mkwajuni Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Picha ya pili ni Makamu wa Kwanza wa Rais
wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akionnyesha Ripoti ya Idadi ya Watu
Duniani kwa mwaka 2012, baada ya kuizindua rasmi huko Mkwajuni Mkoa wa
Kaskazini Unguja.
Picha ya tatu ni Makamu wa Kwanza wa Rais
wa Zanziba Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na MWakilishi Mkaazi wa
UNFPA Tanzania Mariam Khan baada ya kuzindua Ripoti ya Idadi ya Watu
Duniani kwa mwaka 2012, huko Mkwajuni Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Na picha ya Mwisho ni Waziri wa Afya Juma Duni
Haji akiungana na kikundi cha Sanaa Zanzibar kutoa burudani ya ngoma ya
Msewe wakati wa uzinduzi wa Ripoti ya Idadi ya Watu Duniani kwa mwaka
2012, huko Mkwajuni Mkoa wa Kaskazini Unguja.(Picha na Makame Mshenga
Maelezo Zanzibar)
Na-Maelezo Zanzibar
Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema kuwa jamii inahitaji kuelimishwa zaidi
juu ya umuhimu wa uzazi wa mpango kwa maendeleo ya nchi sambamba na
kutunza afya ya jamii hasa kwa akina mama na watoto.
Kauli
hiyo imetolewa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif
Sharif Hamad katika hafla ya uzinduzi wa Ripoti ya Idadi ya Watu Duniani
ya mwaka 2012 iliyofanyika katika viwanja vya skuli ya Mkwajuni Mkoa wa
Kaskazini Unguja, ambako alimuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohd Shein.
Amesema
jamii bado haijatoa umuhimu unaostahiki katika matumizi ya njia za
uzazi wa mpango, hali inayopelekea kuwepo kwa ongezeko kubwa la watu
ambalo huathiri harakati za maendeleo na afya ya jamii.
“Taarifa
zinaonesha kwamba Zanzibar hivi sasa inakadiriwa kuwa na idadi ya watu
1.3 milioni, wanaoongezeka kwa kasi ya asilimia 3.1 kwa mwaka ambapo
idadi ya watu katika kila kilomita moja ya mraba imefikia watu 496 mwaka
2011”, ilieleza sehemu ya hotuba hiyo ya Dkt. Shein iliyosomwa na
Makamu wa Kwanza wa Rais.
Amefahamisha
kuwa bado vifo vya mama wajawazito viko juu duniani lakini vimepungua
kwa upande wa Tanzania na Zanzibar hasa kwa kina mama wenye umri mdogo
na wanaokabiliwa na tatizo la umaskini.
“Kwa
Tanzania katika mwaka 2004/05 idadi ya vifo ilikuwa 578 kwa kila akina
mama waja wazito 100,000 na kupungua kidogo hadi kufikia vifo 454 mwaka
2010. Hata hivyo kwa Zanzibar vifo vya akina mama vimepungua kutoka vifo
473 mwaka 2006 hadi vifo 281 mwaka 2011, kwa kila kina mama 100,000 kwa
takwimu za hospitali”, alifafanua.
Amesema
mafanikio hayo yametokana na juhudi za serikali katika kuimarisha
huduma za afya kwa jamii ikiwa ni pamoja na kutoa chanjo za pepopunda na
shurua, sambamba na kuimarisha huduma za afya ya uzazi katika hospitali
mbali mbali.
Ametoa
wito maalum kwa Wazazi kuwaozesha watoto zao kuanzia umri wa miaka 20
na kuendelea ili wamalize masomo yao kwani elimu ni ufunguo wa Maisha.
Kwa
upande wao wawakilishi wa Umoja wa Mataifa wameipongeza Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuona umuhimu wa huduma ya uzazi na kuamua
kutoa huduma hiyo bila ya malipo.
Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Idadi ya watu (UNFPA) Tanzania bibi Mariam Khan
amesema bado suala la uzazi wa mpango linakabiliwa na changamoto nyingi
ikiwa ni pamoja na wanajamii kuona ugumu juu ya matumizi ya njia za
uzazi wa mpango.
Amesisitiza
kuwa Mashirika ya Kimataifa ya UN na UNFPA yataendelea kuziunga mkono
jitihada zinazofanywa na Serikali ya Muungano na ile ya Mapinduzi ya
Zanzibar ili kuhakikisha jamii inapata uelewa na kudumisha uzazi wa
mpango.
Amefahamisha
kuwa uzazi wa mpango ni muhimu katika kusaidia kukuza kipato cha
wanafamilia, sambamba na kuwaendeleza watoto katika makuzi bora, na wito
kwa jamii kutoa fursa zinazostahiki kwa akina mama na watoto ili
kusaidia harakati za maendeleo kwa jamii.
Kwa
upande wake Waziri wa Afya Mhe. Juma Duni Haji amesema wameamua kufanya
uzinduzi huo katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, ili kutoa uelewa zaidi
kwa wakaazi wa Mkoa huo ambao ni miongoni mwa mikoa inayofanya vibaya
katika suala la uzazi wa mpango.
Amesema
akinamama na watoto wanahitaji kulindwa kiafya, na kuwataka wazazi hasa
wa kiume kushirikiana kikamilifu katika suala la malezi na makuzi ya
watoto wao.
Mapema
akitoa muhtasari wa ripoti hiyo, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Uchumi na
Mipango ya Maendeleo Khamis Mussa amesema kimsingi ripoti hiyo
imeelezea juu ya changamoto, faida na haki za binadamu katika uzazi wa
mpango.
Amesema
uzazi wa mpango ni miongoni kwa haki za binadamu lakini imeelekezwa
zaidi kwenye haki za kifamilia, ili wanafamilia waweze kupanga juu ya
idadi na umri wa kupishana kwa watoto, ili kuepuka mimba zisizotarajiwa.
“Inakisiwa
kuwa kiasi cha mimba milioni 80 zinapatikana bila ya kutarajiwa
duniani, huku nusu ya mimba hizo zikitolewa, jambo ambalo ni hatari
katika uzazi”. Alidokeza Katibu Mkuu huyo.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Uzazi wa Mpangilio katika ukuzaji Uchumi”
No comments:
Post a Comment