Monday, November 12, 2012

Kesi ya madai dhidi ya ACU na raia wa ugiriki kusikilizwa 23 january mwakani.


Kesi ya madai dhidi ya ACU na raia wa ugiriki kusikilizwa  23 january mwakani.
Joseph Ngilisho, Arusha.
 
KESI ya madai iliyofunguliwa mwaka 2007 na mamlaka ya kahawa ACU mkoa wa Arusha dhidi ya raia wa Ugiriki anayeishi nchini Tanzania katika eneo la Usa river Sotiris Sotirades (87) imehairisha hadi january  23 mwakani.
HAKIMU wa  baraza la ardhi na nyumba mkoa wa Arusha,Maiko Makombe  amesema kuwa siku ya  kesi hiyo pande zote mbili zitapaswa kuleta mashaidi wao ili kesi hiyo iweze  kuanza  kusikilizwa na haki iweze kutendeka kwa haraka.
Akizungumza mahakamani hapo, Hakimu Makombe alisema kuwa, kesi hiyo ya madai namba 209 ya mwaka 2007 ameirithi mwaka 2009,kutoka kwa hakimu mwingine aliyekuwa anaisikiliza ambaye kwa sasa amehamia jijini Dar es salaam.
Makombe alisema kuwa, kesi hiyo ambayo kwa sasa ipo katika hatua ya kusikilizwa imeshindwa kuendelea kwa wakati kutokana na upande wa mashtaka kutoa udhuru kila wanapofika mahakamani ama kutofika kabisa hivyo,ifikapo january mwakani wawe wamejipanga na kuleta mashaidi wao kwa ajili ya kuendelea kwa kesi hiyo. 

Alisema kuwa,kesi hiyo imedumu kwa muda mrefu sasa na uchelewashaji huo umekuwa hauwatendei haki upande wa mdaiwa kwani wao wamekuwa wakihudhuria mahakamani hapo mara kwa mara na kesi kuendelea kupigwa tarehe,kitendo ambacho kinawapa usumbufu usio na tija .
‘’Kwa kweli kitendo hiki hakitendi haki hata kidogo mahakama zimekuwa zikilaumiwa sana kwa kuchelewesha kesi za watu ,lakini kwa hali hii utailaumu mahakama,na mimi leo nasisitiza awamu nyingine msipofika naifuta kesi hii’’alisema Makombe.
Hata hivyo hakimu alimtaka Mwakilishi wa ACU kuhakikisha kuwa siku ya kesi wawe tayari wamejiandaa kwa kutoa ushaidi ili kesi hiyo iweze kuendelea kwani imedumu kwa muda mrefu sasa .

Akizungumza kwa masikitiko mahakamani hapo, mgiriki huyo alisema kuwa alimweleza Hakimu Makombe kuwa , upande wa madai wamekuwa wakifanya makusudi kuahirisha kesi hiyo ili kuvuta muda mzee huyo aweze kufa na hatimaye kesi yake ya msingi iweze kupotea.
Alisema kuwa,pamoja na kuwa amekuwa akihudhuria mahakamani hapo kila kesi inapotajwa lakini cha ajabu hakuna lolote linaloendelea ,na kuwa kwa sasa hivi anaumwa sana hivyo anahofia  pindi atakapokufa  haki yake ya msingi inaweza  ikapotea.
Hivyo  aliiomba mahakama kuharakisha kesi hiyo ili iweze kumalizika kwa haraka kwani imedumu kwa muda mrefu na amekuwa akitumia gharama kubwa  ya uendeshaji wa kesi hiyo ikiwa ni pamoja na kuwalipa mawakili na usafiri wa kwenda na kurudi kila kesi inapotajwa.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment