Na ROSE JACKOSON , Arusha
SERIKALI imeombwa kutoa elimu zaidi hasa kwa mabalozi wa
nyumba kumi kumi maeneo ya Vijijini hasa kwa upande wa walemavu kwani baadhi ya
wananchi wa vijijini bado wana uelewa mdogo kwa walemavu na hali hiyo huenda
ikasababisha wasishirikishwe katika zoezi la Sensa ya watu na makazi.
Hayo yameelezwa na Bi Yunisi Urasa ambaye ni Katibu wa
shirikisho la vyama wenye ulemavu(SHIVYAWATA) mapema jana wakati akiongea na
wakufunzi ambao watashirikishi katika zoezi la Sensa.
Aidha bi Yunisi alisema kuwa ni vema kama zoezi hilo liweze kuwafikia watu wote kama
sheria inavyosema lakini wapo baadhi ya watu ambao hawataweza kufikiwa kutokana
na uelewa mdogo , pamoja na Imani mbaya dhidi ya walemavu.
Aliongeza kuwa endapo kama Serikali kwa sasa ikiwashirikisha
viongozi wa nyumba kumi kumi katika zoezi hilo la Sensa itachangia kwa kiwango
kikubwa sana watu wenye ulemavu hasa watoto wa maeneo ya vijijini kuweza kushiriki katika zoezi hilo la Sensa.
“kama tunavyoona ni
kuwa zoezi hili linasonga mbele zaidi hasa hapa mijini lakini sisi tunajiuliza
kuwa je Kijijini itakuwaje na kwa maana hiyo basi kama hawa mabalozi wa nyumba
kumi kumi watahamasisha watu hasa wenye ulemavu watakuwa ni kichocheo
kikubwa sana hasa kwa Serikali hasa kufikia kwenye malengo yake ya Sensa
na watu kwa kipindi hiki”aliongeza Bi Yunisi.
Pia alisema kuwa mbali na Mabalozi kuhamasisha watu juu ya
umuhimu wa Sensa ya watu na makazi hasa maeneo ya Vijijini nao wanawake wana nafasi kubwa sana ya
kusaidia na kuraisisha zoezi hilo kwa
kuachana na mila potofu za watoto walemavu kwa kuwa nao wana haki ya msingi
kabisa.
“Wanawake wa Vijijini wanatakiwa kujua na kutambua kuwa
Sensa ina umuhimu mkubwa sana
kwa maendeleo ya jamii ambapo kupitia hata Sensa hiyo itaweza kusaidia Jamii
hizo za Walemavu katika mahitaji muhimu ikiwemo huduma za Msingi kwenye maisha
ya kila siku”aliongeza Bi Yunisi
Awali Mratibu wa zoezi hilo la Sensa kwa Mkoa wa Arusha Bi
Magret Martin alisema kuwa mpaka wamejipanga kuhakikisha kuwa makundi yote
kwenye jamii yanafikiwa katika zoezi hilo la Sensa kwa kuwa Sensa ina umuhimu
mkubwa sana kwa maslahi ya Taifa la Tanzania.
Bi Magret aliongeza kuwa ndani ya mafunzo yanayoendelea
mjini hapa wamejipanga kuhakikisha makundi maalumu katika jamii nayo yanafikiwa
na jamii kwa kuwa nayo yana nafasi kubwa sana
katika kuraisisha zoezi hilo
ndani ya jamii ya Kitanzania.
MWISHO
No comments:
Post a Comment