KAMISHENI YA AFRIKA KUSIMAMIA USIKILIZAJI WA KESI ZA MAUAJI YA
KIMBARI RWANDA
Na Nicodemus Ikonko, Hirondelle, Arusha
Arusha, September 25, 2012(FH) – Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya
Kimbari ya Rwanda (ICTR) imehitimisha majadiliano na Kamisheni ya Afrika ya
Haki za Binadamu na Watu (ACHPR) ili kusimamia usikilizaji wa kesi za mauaji ya
kimbari zinazopelekwa kusikilizwa nchini Rwanda.
‘’Hali iliyopo sasa ni kwamba ICTR kupitia ofisi ya Msajili imeshahitimisha
majadiliano na ACHPR kusimamia usikilizaji wa kesi,’’ Msemaji wa Mahakama hiyo
ya Umoja wa Mataifa, Roland Amossouga aliliambia Shirika la Habari la
Hirondelle Jumanne.
Aliongeza kwamba,’’Hati ya makubaliano hayo itatiwa saini hivi karibuni
na baada ya hapo ACHPR ndipo itaanza rasmi kazi yake ya kusimamia kesi ya
(Jean) Uwinkindi nchini Rwanda.’’
Wafanyakazi wawili wa ICTR waliteuliwa Aprili mwaka huu kama wasimamizi wa muda wa kesi ya Uwinkindi, huku ACHPR
ikisubiriwa kukamilisha makubaliano na ICTR kufanya kazi hiyo. ACHPR ina
majukumu ya kulinda na kukuza haki za binadamu ikiwa ni miongoni mwa kazi
zake.
Wakati ukitolewa uamuzi wa kuhamishia kesi ya Uwinkindi kwenda Rwanda
Juni 2011, Majaji walimwelekeza Msajili wa Mahakama ICTR kuingia katika mkataba
wa maandishi na ACHPR ambao utaeleza wazi maslahi, fedha zinazohitajika na
mambo mengine muhimu ambayo yatafanya taasisi hiyo kuweza kutekeleza majukumu
yake ipasavyo.
Kwa mujibu wa majaji ‘’ACHPR itatakiwa kuwasilisha ripoti ya mara kwa
mara kila baada ya miezi mitatu juu ya hali ya mwenendo wa kesi kwa Rais wa
ICTR kupitia kwa Msajili wake, wakati kesi itakapoanza kusikilizwa hadi hapo
itakapohitimishwa ikiwa ni pamoja na hatua ya rufaa kwa mshitakiwa na pia
katika hatua ya kusimamia adhabu itakayotolewa, kama
itakuwepo.’’
Majaji waliridhika kuwa hatua ya Kamisheni hiyo kusimamia mwendendo
mzima wa kesi utatoa hakikisho kwamba ukiukwaji wowote wa haki ya mshitakiwa
katika mwenendo wa kesi yake utapelekwa mbele ya Rais wa ICTR mara moja ili hatua
za kurekebisha zichukuliwe ikiwa ni pamoja na kufikiria kuiondoa kesi hiyo
kusikilizwa mbele ya mahakama za Rwanda.
ICTR tayari imeridhia kesi nane kwenda kusikilizwa nchini Rwanda.
Uwinkindi, ambaye ni mchungaji alihamishiwa nchini Rwanda Aprili 19, 2012,
akiwa ni mshitakiwa wa kwanza wa ICTR kesi yake kwenda kusikilizwa nchini humo.
Nje ya Uwinkindi, kesi nyingine zilizohamishiwa nchini Rwanda ni pomoja
na mtuhumiwa ambaye bado anashikiliwa na ICTR na kiongozi wa zamani wa
wanamgambo wa Interahamwe, watuhumiwa sita ambao bado wanasakwa, wakiwemo
mameya watatu, polisi mmoja, afisa wa zamani wa jeshi na meneja mmoja wa
mgahawa. Hata hivyo kesi nyingine mbili bado zipo mbele ya Mahakama ya Rufaa
zikisubiri uamuzi.
No comments:
Post a Comment