Na Hirondelle, Arusha
Arusha,
Septemba 11, 2012 (FH) – Mahakama ya Rufaa ya Mahakama ya Kimataifa ya
Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) Oktoba 9, 2012 itatoa hukumu ya kesi
ya rufaa ya afisa mwandamizi wa zamani wa serikali ya Rwanda,
Jean-Baptiste Gatete, kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Mahakama hiyo.
Katika
kesi hiyo, pande zote mbili, za mwendesha mashitaka na utetezi zimekata
rufaa dhidi ya hukumu iliyotolewa na mahakama ya awali Machi 29, 2011.
Gatete,
ambaye ni Mkurugenzi wa zamani katika Wizara ya Wanawake na Masuala ya
Familia alitiwa hatiani kwa mauaji ya kimbari na kutekekteza kizazi kama
uhalifu dhidi ya binadamu na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela.
Majaji
walisikiliza rufaa hiyo Mei 7, mwaka huu huku upande wa mwendesha
mashitaka ukiomba mtu huyo atiwe hatianin pia kwa kosa la kula njama.
Kwa mujibu wa mwendesha mashitaka, mahakama ya awali imedaiwa kukosea
kwa kutomtia hatiani Gatete kwa shitaka hilo kwa sababu karibu vigezo
vyote vimefikiwa.
Lakini
kwa upande wake, mawakili wa utetezi wameomba mteja wao aachiwe huru
kwa mashitaka yote aliyotiwa nayo hatiani kwa madai kwamba
hayakuthibitishwa. Upande wa utetezi pia umeomba kwamba iwapo ombi lao
la awali halitakubali basi mteja wao apunguziwe adhabu.
Katika
mahakama ya awali, Gatete ilionekana na hatia pasipo mashaka yoyote kwa
kuhusika na vifo vya mamia au hata maelfu ya Watutsi katika maeneo
matatu yalikofanyikia mauaji hayo, Mashariki mwa Rwanda kati ya Aprili 7
na 12, 1994.
Maeneo
yalikotokea umwagaji damu mkubwa ni pamoja na yale ya kata ya Rwankuba
na parokia ya Kiziguro kwenye wilaya ya Murambi katika mkoa wa Byumba na
maeneo ya parokia ya Mukarange katika wilaya ya Kayonza, mkoa wa
Kibungo.
Gatete
(59) alitiwa mbaroni nchini Congo-Brazzaville Septemba 11, 2002 na
kisha kuhamishiwa makao makuu ya ICTR, Arusha nchini Tanzania. Kesi yake
ilianza kusikilizwa Oktoba 20, 2009.
No comments:
Post a Comment