Tuesday, September 25, 2012

wanafunzi wa ilboru waandamana



Joseph Ngilisho,Arusha


WANAFUNZI wa shule ya Sekondari Ilboru iliyopo Arumeru mkoani Arusha,wameandamana katika ofisi ya mkuu wa mkoa wa Arusha,wakishinikiza mkuu wao wa shule ,Jovinas Mutabuzi aondolewe kwa madai kwamba amekuwa akichangia kudorora kwa elimu shuleni hapo.

Wakitoa madai yao leo mbele ya mkuu wa mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo,majira ya saa 2 asubuhi ,wamemtuhumu Mutabuzi kwenda kinyume na utaratibu wa shule hiyo ikiwemo kuwatimua ovyo walimu wao wanaodai walikuwa wakiwafundisha vizuri,kuwanyanyasa na matumizi mabaya ya fedha za shule.

Aidha wamebainisha kuwa mkuu huyo ameshiriki kuwagawa wanafunzi  kiitikadi za kidini  na kisiasa, kuwatoza faidi ya shilingi 150,00 hadi 190,000 pindi wanapotenda kosa ikiwemo kuchelewa wanapokuwa likizo ama wanapo kuwa na ruhusa ya kwenda kanisani ama msikitini.

Madai  mengine ni ufujaji wa fedha za umma zinazotolewa na wahisani ama wadau wa elimu wakishirikiana na mhasibu wa shule hiyo,ukarabati duni wa shule,miundo mbinu mibovu,wizi wa mali za umma,bodi ya shule isiyoeleweka,kudorora kwa taaluma,matumuzi mabaya ya fedha  na wanafunzi kudhalilishwa.

Akiongea kwa niaba ya wenzake kiongozi wa serikali ya wanafunzi hao(HP),Didas Mselle alimtaka mkuu huyo wa mkoa kuwapatia jibu la mara moja juu ya utekelezaji wa madai yao ikiwemo kumwondoa  mkuu wa shule hiyo kwani hawamtaki.

Alisema  wamekuja katika ofisi hiyo ya mkuu wa mkoa kwa lengo moja la kupata utatuzi wa madai yao ambayo wamedai yamekuwa ya muda mrefu bila kupatiwa ufumbuzi huku wanafunzi hao wakiendelea kunyanyasika na kusababisha baadhi yao kushuka kielimu kutokana na ufundishwaji mbovu huku idadi kubwa ya walimu wakitimuliwa mara kwa mara.

Wanafunzi hao wameenda m,bali zaidi wakimtuhumu Mutabuzi,kuiendesha shule hiyo kibabe kwa sheria zake huku akitumia simu yake ya mkononi kama M pesa ya kutumiwa fedha zinazotokana na adhabu ya wanafuzi hao.

‘’kwanza tunashangaa shule yetu inaakaunti tatu lakini mkuu wetu anaataka tumtumie fedha kwenye namba ya simu ya mhasibu wake hili suala haliwezekani kabisa kwani hata risiti hatupewe’’alisema

Akijibu hoja hizo mkuu huyo wa mkoa, aliwasihi wanafunzi hao kuacha jaziba na kurudi shuleni kuendelea na vipindi vya masomo kwani  hoja zao zitafanyiwa kazi na kwa kiasi kikubwa zimeonekana kuwa za msingi.

‘’mmekuja hapa kwa lengo la kuwasilisha kero zetu sasa tumezisikia ,tumezichukua na tunazifanyia kazi,rudini shuleni tutatuma viongozi wetu kufuatilia madai yenu na kuyapatia ufumbuzi ikiwemo kusikiliza upande mwingine’’alisema Magesa Mulongo.

Naye mkuu huyo wa shule hiyo,Jovinas Mutabuzi alipotafutwa kwa njia ya simu ya mkononi ili kujibu tuhuma hizo alisema kuwa madai hayo hayana msingi wowote na yamejaa uchochezi na kueleza kuwa wanafunzi hao wanamsukumo wa kisiasa na mara nyingi wamekuwa wakishiriki matendo maovu na  wanapokemewa ikiwemo kupewa adhabu wanasema wananyanyaswa .

Wanafunzi hao waliweza kutawanywa na askari polisi waliowaamuru warondoke na kurudi shuleni baada ya amri ya mkuu wa mkoa kuitoa ,hata hivyo hakuna vurugu yoyote iliyotokea.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment