BARAZA LA USALAMA LA UN KUAMUA HATMA YA KUMBUKUMBU ZA ICTR
Na GLADNESS MUSHI, Arusha
Arusha, Septemba
06,2012 (FH) – John Hocking, Msajili wa Taasisi ya Kimataifa itakayorithi kazi
za Mahakama za Kimataifa (MICT), Jumanne aliliambia Shirika la Habari la
Hirondelle kwamba hatma ya mahali pa kuhifadhi kumbukumbu za Mahakama ya
Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) iko mikononi mwa Baraza la
Usalama la Umoja wa Mataifa.
Rwanda imekuwa ikidai haki
ya kuhifadhi kumbukumbu za ICTR baada ya kuhitimisha kazi zake kwa maelezo
kwamba yenyewe ndiyo yenye haki ya kiasili ya kupokea kumbukumbu hizo kutokana
na ukweli kwamba mauaji ya kimbari yalifanyikia nchini Rwanda.
Wakati wa uzinduzi
rasmi wa MICT, tawi la Arusha, Julai 2, 2012, Mwendesha Mashitaka Mkuu wa
Rwanda, Martin Ngoga alisema wanahitaji majadiliano ya wazi katika masuala
mbalimbali likiwemo hilo la uhifadhi wa kumbukumbu.
Lakini wakati wa
mahojiano maalum na Shirika la Habari la Hirondelle,Msajiliwa MICT, John
Hocking alisema ‘’Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa namba 1966
litafanyiwa tathmini baada ya miaka minne ijayo na siwezi kujua nini kitatokea
baada ya miaka minne. Ni wazi kwamba sina mwelekeo kamili juu ya hili lakini
kwa hivi sasa ninachokifanyia kazi ni azimio la Baraza la Usalama, ambalo
limeelekeza kwamba, kumbukumbu hizo zihifadhiwe mahali zilizopo mahakama hizo
za Umoja wa Mataifa.’’
Kwa mujibu wa azimio
hilo la Baraza la Usalama lililoidhinishwa mwishoni mwa mwaka 2010, kuanzishwa
kwa MICT ni kwa ajili ya kurithi kazi zitakazoachwa na ICTR, yenye makao yake
makuu, Arusha, Tanzania na mahakama nyingine ya Umoja wa Mataifa ya Uhalifu wa
Kivita Katika Yugoslavia ya zamani (ICTY) iliyopo The Hague, Uholanzi.
‘’Katika azimio hilo, Baraza la Usalama
lilieleza kwamba, kumbukumbu za ICTR zihifadhiwe Arusha na zile za ICTY
zihifadhiwe The Hague,’’ alisisitiza Hocking.
Msajili huyo
aliendelea kufafanua kwamba tawi la MICT la Arusha lilipoanza kazi Julai 1,
mwaka huu shughuli mbalimbali za ICTR zilihamishiwa kwa taasisi hiyo mpya ikiwa
ni pamoja na kumbukumbu za baadhi ya kesi zilizokwishahitimishwa na ulinzi wa
watu waliotoa ushahidi katika kesi hizo.
Shughuli nyingine
zilizohamishiwa kwenye taasisi hiyo mpya ni pamoja na kusaidia juhudi za
mataifa yanayofanya uchunguzi dhidi ya watuhumiwa wa mauaji hayo nchini mwao na
kuendelea kuwasaka watuhumiwa tisa ambao bado hawajatiwa mbaroni.
Kwa mujibu wa Hocking
pia jukumu la kusimamia adhabu walizopewa wafungwa waliopo katika nchi za
Mali na Benin pia
lilihamishiwa kwenye taasisi hiyo kuanzia tarehe hiyo.
Alipoulizwa juu ya
usalama wa wafungwa wanaotumikia adhabu zao nchini Mali
kutokana na tishio la hali ya usalama nchini humo, Hocking alijibu kuwa Idara
ya Ulinzi na Usalama ya Umoja wa Mataifa na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa
nchini Mali
wamemhakikishia kwamba wafungwa wote wako salama.
Hivi sasa wako
wafungwa 19 wanaotumikia adhabu zao nchini Mali.
No comments:
Post a Comment