Halmashauri ya Meru yawapimia wananchi viwanja zaidi ya
4000 .
GLADNESS MUSHI, Arusha.
HALMASHURI ya Meru wilayani Arumeru mkoani Arusha imewapimia wananchi
zaidi ya viwanja 4000 katika maeneo mbalimbali pamoja na kuwapatia
michoro, ramani na hati za ardhi kwa lengo la kuwawezesha wananchi kuwa na
usalama na mali
zao.
Hayo yalisemwa hivi karibuni na Mwenyekiti wa halmashauri
ya wilaya ya Meru, Godson Majola wakati akizungumza katika ufunguzi wa baraza
la madiwani lililofanyika katika halmashauri hiyo.
Majola alisema kuwa , halmashauri hiyo wameandaa mikakati mbalimbali
ya kuanza kuwapimia wananchi maeneo yao kwa
lengo la kuwapatia hati miliki ili kuwawezesha kupata mikopo na hata kuendeleza
shughuli mbalimbali za maendeleo katika maeneo yao.
Alisema kuwa, lengo la kuwapimia wananchi maeneo yao ni ili
kuwawezesha kwa urahisi kuaminika katika taasisi mbalimbali za fedha na
kuweza kupata mikopo , kwani changamoto kubwa iliyokuwa ikiwakabili ni
kutokuwa na hati miliki za ardhi ambazo zinawawezesha kuchukua mikopo.
Alifafanua zaidi kuwa, upimaji huo wa ardhi za wananchi utafanyika
kata zote za halmashauri hiyo ambapo mchakato huo tayari unaendelea na
zoezi zima linaedelea vizuri katika maeneo mbalimbali.
Aidha aliwataka madiwani kuhakikisha wanashiriki kikamilifu
katika kutoa ushirikiano katika upimaji wa maeneo hayo ya wananchi ikiwa ni
pamoja na kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika zoezi hilo.
Hata hivyo alitoa wito kwa viongozi mbalimbali ambao hawajawapimia
wananchi maeneo yao
kuhakikisha wanaanza mchakato huo mapema ili kuwawezesha wananchi hao kupata
hati miliki ambazo zitawezesha kuchangia shughuli mbalimbali za maendeleo.
‘Jamani madiwani katika upimaji wa maeneo ya wananchi kunakuwepo
na changamoto mbalimbali ndani yake lakini nyie ndio mtakaowezesha
kutatuliwa kwa changamoto hizo kwa wakati, hivyo wahusika wanapowafikia katika
ameneo yenu tafadhali mtoe ushirikiano wa kutosha ili kila mwananchi
aweze kupata haki yake ya msingi’alisema Majola.
Naye Mkurugenzi wa halmashauri ya Meru,Trisias Kagenzi alisema kuwa,
upimaji huo utawezesha kwa kiasi kikubwa sana kuondokana na ujenzi holela
unaofanyika katika maeneo mengi ya mji wa Usa river kwani kumekuwepo na
wimbi kubwa sana la ujenzi holela katika maeneo mbalimbali.
Aidha alitumia fursa hiyo kuwataka madiwani wanasimamia kikamilifu
miundombinu ya barabara hususani katika upanuzi wa barabara katika kata zao kwa
lengo la kuhakikisha maendeleo yanakuwepo katika kata zao na kuweza kutatua
changamoto mbalimbali za wanachi.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment