RWANDA YAKANA KUKOSA FEDHA KUGHARIMIA KESI YA UWINKINDI
Na Hirondelle, Arusha
Arusha,
Oktoba 16, 2012 (FH) – Rwanda, Jumanne imekanusha ripoti kwamba timu ya
utetezi ya mshitakiwa wa mauaji ya kimbari, Mchungaji Jean Uwinkindi
imekosa fedha za kuwawezesha kufanya upelelezi na kuwatafuta mashahidi
wa kumtetea mteja wao.
Uwinkindi
ni mshitakiwa wa kwanza wa Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari
ya Rwanda (ICTR) kesi yake kuhamishiwa nchini Rwanda,kusikilizwa katika
mahakama ya nchi hiyo.
Gatera
Gashabana,Wakili wa utetezi wa Uwinkindi alitoa malalamiko ya
kukosekana kwa fedha, kwa mujibu wa msimamizi wa mwenendo wa kesi hiyo
wa ICTR, Anees Ahmed. Lakini kwa upande wake, Mwendesha Mashitaka Mkuu
wa Rwanda, Martin Ngoga alisema Jumanne kwamba hakuna uhaba wa fedha
kugharimia kesi hiyo.
‘’Serikali
inajua majukumu yake ya kuwezesha upande wa utetezi chini ya mfumo wa
msaada wa kisheria,’’ Ngoga aliliambia Shirika la Habari la Hirondelle
kwa simu. ‘’Shughuli yoyote ya upande wa utetezi inayoruhusiwa na
mahakama italipwa.Hakuna uhaba wa fedha kwa ajili hiyo.’’
‘’Kama
upande wa utetezi unataka kufanya shughuli yoyote, hawana budi kuiomba
mahakama,’’ Ngoga aliiambia Hirondelle. Alisema hakuna ombi la aina hiyo
mbele ya jaji na kwamba ‘’hakuna haja ya kupiga kelele kwa jambo ambalo
halijafikishwa mbele ya mamlaka husika.’’
Alipokuwa
chini ya kizuizi cha ICTR, Mchungaji Uwinkindi kama mtu asiyekuwa na
uwezo wa kujilipia huduma za kisheria, alikuwa anapewa huduma hiyo na
mahakama hiyo ya Umoja wa Mataifa.Lakini Mbele ya mahakama ya Rwanda,
gharama za msaada wa kisheria zinatakiwa kulipwa na serikali ya Rwanda.
Kwa
mujibu wa ripoti ya msimamizi wa mwenendo wa kesi hiyo, msaada wa
kisheria unaotolewa kwa Wakili Kiongozi na Msaidizi wake unagharimia
huduma tu na hauruhusu kulipia gharama za kukodisha wapelelezi wa kesi
au gharama za kuwatafuta mashahidi watarajiwa, kuchukua maelezo yao na
kuhakikisha kuwepo mbele ya mahakama wanapohitajika.
ICTR
iliamuru kuhamishwa kwa kesi ya Uwinkindi kwenda kusikilizwa nchini
Rwanda Juni mwaka jana na Mahakama ya Rufaa ilithibitisha uamuzi huo
Desemba, 2011. Uwinkindi alihamishiwa nchini Rwanda Aprili 19, 2012.
Wafanyakazi
wawili wa ICTR waliteuliwa kuwa wasimamizi wa muda wa mwenendo wa kesi
hadi hapo makubaliano yatakapokamilishwa ya kupata wasimamizi kutoka
Kamisheni ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu(ACHPR).
Mchungaji
Uwinkindi anashitakiwa kwa mauaji ya kimbari na kuteketeza kizazi. Kwa
mujibu wa Msimamizi wa ICTR, upande wa mwendesha mashitaka uko tayari
kuanza kusikilizwa kwa kesi hiyo.
No comments:
Post a Comment