NA MWANDISHI MAALUM NEW YORK
Rais Jakaya Mrisho Kikwete amesema, vifo vya akina mama vitokanavyo na
matatizo wakati wakujifungua havipaswi kutokea na havikubaliki.
Na kwa sababu hiyo, anasema juhudi zaidi zinahitajika katika kubabiliana
na hali hiyo na hasa ikizingatia kwamba sababu zinazosabisha kutokea
kwa vifo hivyo zinazuilika.
“ Vifo vya wanawake wajawazito havikubaliki” akasema na kuongeza “ na
ndiyo kwasababu tunahitaji kuongeza juhudi zaidi kuokoa maisha ya
wanawake, kwa sababu si haki na si jambo jema kwa mwanamke kufa wakati
wa kujifungua , si haki afe wakati akimleta kiumbe mwingine duniani, na
cha kusikitisha zaidi wanakufa kwa sababu ambazo zinaweza kuzuilika”.
Akasisitiza Rais Kikwete.
Ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa awamu ya pili ya mpango wa
ubunifu wa uboreshaji wa huduma ya afya ya mama na mtoto katika maeneo
ambayo huduma hiyo haipatikani kwa urahisi nchini Tanzania.
Uzinduzi wa mpango huo umefanyika mbele ya waandishi wa habari siku ya
jumanne hapa Makao Uakuu ya Umoja wa Mataifa na kuhudhuriwa na Katibu
Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, Rais Jakaya kikwete na
wafadhili wakuu wa mpango huo ambao ni Meya wa Jiji la New York na
philanthropist Michael Bloomberg na Dkt. Helen Agerup, Mkuu wa Mfuko wa
H&B Agerup.
Wafadhili hao wawili wametoa dola za kimarekani milioni 15 kufadhili
huduma za uboreshaji wa vituo vya afya, na mafunzo ya huduma za
upasuaji wa dhararu kwa waganga, wakunga na manesi lengo likiwa ni
kuokoa maisha ya wanawake wanapojifungua na kupunguza umbali wa
kuifuata huduma hiyo.
Rais Kikwete amesema kwamba, uboreshaji wa huduma za afya ya mama na
mtoto na afya kwa ujumla ni moja ya vipa umbele vyake muhimu na ni
jambo lililo ndani ya moyo wake.
“Tumefanya mengi na tunaendelea kufanya, lakini tunahitaji kuongeza kasi
ya juhudi hizi, uboreshaji wa huduma ya afya ya mama na mtoto ni
kupaumbele changu ni jambo lililo moyoni mwangu na tunapopata wafadhilli
kama nyinyi kuchangia juhudi zetu tunafarijika zaidi na kutiwa moyo na
tunawashukuru” akasema Rais.
Naye katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, ambaye amekuwa
mstari wa mbele katika kupigania nakutetea haki za wanawake na watoto,
amesisitiza haja na umuhimu wa ushirikiano kati ya sekta za umma na
sekta binafsi kuokoa maisha ya wanawake na watoto kwa kuboresha huduma
zao.
“Tunahitaji marais, mameya ,wanaharakatiwa kuboresha huduma za afya
na wafanyakazi wa afya hadi ngazi ya chini kabisa. Leo tunashuhudia
matokeo ya ushirikiano huu ambapo kwa ushirikiano wa viongozi watatu
tumeweza katika kipindi cha miaka miwili kupunguza kwa asilimia kubwa
vifo vya wanawake wajawazito katika maeneo ya mikoa ya Kigoma,
Morogoro na Pwani ambako mpango huu wa ubunifu umekuwa ukitekelezwa”
akabainisha Ban ki Moon
Aidha Ban Ki Moon amemuelezea Rais Jakaya kikwete kama mmoja wa
viongozi wa kwanza duniani kuungua mkono mkakati wa Kimataifa kuhusu
Afya ya mama wajawazito na watoto, mpango uliozinduliwa mwaka 2010
ambapo kiasi cha dola milioni 400 zitaelekezwa katika uboreshaiji wa
huduma hizo. Na ni mpango unaokwenda sambamba na utekelezaji wa
Malengo ya Maendeleo Millenia ( MDGs).
Kwa upande wake Meya na philanthropies Michael Bloomberg akizungumza
kwenye uzinduzi huo anasema aliamua kuichagua Tanzania kufadhili
uboreshaji wa huduma za afya ya mama na mtoto kutokana na kuvutiwa
kwake na juhudi za Rais Jakaya Kikwete katika kukabiliana na vifo
vitokanavyo na uzazi.
“Mwaka 2006 niliamua kuwekeza Tanzania kwa kubuni mpango huu wa
kuboresha huduma ya dharura ya uzazi hasa katika maeneo ambayo
hayafikiki na hakuna huduma za afya. Niliamua hivi kwa sababu nilivutiwa
sana na juhudi za Rais Kikwete, ni kiongozi makini, imara na ambaye
amekuwa mstari wa mbele katika suala hili, Tanzania inabahati ya kuwa na
kiongozi kama huyo” akasisitiza
Na kuongeza kwamba mpango wake huo ambao amesema ni wa aina yake na wa
kwanza kufanyika na umeanza katika maeneo machache kwa lengo la kuona
maendeleo na mafaniko yake ili baadaye uweze kusambazwa katika maeneo
mengine ya nchi.
Naye Dkt. Helen Agerup, yeye amesema ameamua kuugana na Meya Bloomberg
kufadhili mpango huo kutokana kuvutiwa na kazi nzuri inayofanywa na
Meya na kubwa zaidi baada ya kujionea kwa macho yake kile ambacho
kimekuwa kikifanyika nchini Tanzania.
“Nilikwenda Tanzania mimi na binti yangu na mume wangu, tukajionea kazi
nzuri ya ubunifu huu na namna ilivyoweza kuokoka maisha ya wanawake
wajawazito. Tumeamua kuwekeza kwa sababu kile tulichokiona Tanzania
kimekidhi malengo ya mfuko wetu, kwa sababu tunahitaji kufanya jambo
ambalo matokeo yanapimika, yanaonekana na yanazaa matunda na haya yote
tumeyashuhudia Tanzania”. Akabainisha Dkt. Hellen
Uzinduzi wa mpango huo ulikwenda sambamba na onesho la video fupi
iliyoonyesha kile kilichokuwa kikifanyika nchini Tanzania, kwa maana ya
uokoaji wa vifo vya wanawake wajawazito kwa utoaji wa huduma za dharura
za upasuaji baada ya waganga na wakunga kupewa mafunzo ya upasuaji wa
dharura.
Aidha video hiyo imeonyesha wanawake wakipoteza maisha aidha kutokana na
kupoteza damu nyingi wakati wa kujifungua au kupata maambukizo wakati
wa kijifungua. Lakini imeonyesha pia jinsi ya wataalamu hao wakitoa
huduma hiyo kwa uhodari na uadilifu mkubwa na nyuso zao zikiwa zimejaa
faraja hasa baada ya kupewa mafunzo kupitia mpango huo.
No comments:
Post a Comment