NHC YATAKIWA KUFUATA SHERIA YA MANUNUZI YA UMMA
…………………………………………
NA MAGRETH KINABO- MAELEZO
KAMATI ya Bunge ya Hesabu za
Mashirika ya Umma (POAC) imeliagiza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC)
kufuata Sheria ya Manunuzi ya Umma (PPRA) katika utendaji wake wa kazi.
Kauli hiyo ilitolewa leo na
Mwenyekiti wa POAC,Kabwe Zitto wakati kamati hiyo ilipokutana na baadhi
ya viongozi kuhusu kuzungumzia utendaji wa shirika hilo kwenye ukumbi
wa ofisi ndogo ya Bunge jijini Dares Salaam.
Maagizo hayo yalitolewa na
kamati hiyo kufuatia shirika hilo katika mwaka wa fedha 2010/2011
lilipanga kutumia sh.bilioni 31 lakini limetumia sh. bilioni sh.
bilioni 25 nje ya taratibu za PPRA.
Akijibu
hoja hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Nehemia Msechu alisema
suala hilo limetokana nakuwepo kwa miradi ya dharura iliyoangalia
masuala ya kibiashara. Hata hivyo alisema eneo hilo ni moja ya
changamoto wanayokabiliana nayo, hivyo wameshaanza kuifanyia kazi
kushirikiana na PPRA.
Kamati hiyo pia imelitaka shirika
hilo, kuwakilisha matumizi ya fedha ya mwaka huu unaoishia Juni, 2012
kwa kuonesha mchanganuo sahihi kabla kikao kijacho na kubadilisha mfumo
wa utaratibu wa malipo ya fedha taslimu,badala yake watumie benki ili
kulinda mapato ya shirika.
Aidha Mwenyekiti wa kamati hiyo
alilipongeza shirika hilo kwa kwa kujiendesha kifaida kutoka sh.
bilioni tatu hadi kufikia sh.bilioni sita na thamani ya mali za shirika
hilo kwa sasa imefikia sh. trilioni 1.75.
Zitto aliongeza kuwa shirika hilo
linatakiwa kuendelea mchakato wa kujiendesha kama kampuni ili liweze
kupata mtaji wa kutosha.
Kamati hiyo ilitaka shirika hilo,
kuzingatia mpango wa kujenga nyumba zenye gharama nafuu kwa watu wenye
kipato cha chini hususan maeneo ya vijijini.
No comments:
Post a Comment