MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT)
Mkoa wa Manyara Dorah Mushi amesema Serikali inatakiwa kuharakisha uanzishaji
wa eneo la uwekezaji wa biashara ya nje (EPZA) uliopo mji mdogo wa Mirerani.
Akizungumza juzi na wakazi wa Mji mdogo wa
Mirerani Wilayani Simanjiro wakati alipopokelewa baada ya kuchaguliwa kushika
nafasi hiyo Mushi alisema EPZA itakuwa tegemeo kubwa la Mirerani pamoja na
madini ya Tanzanite.
“Mradi wa EPZA ni tegemeo kubwa kwa wakazi wa
mji mdogo wa Mirerani na Simanjiro kwa ujumla kwani fursa za uchumi
zitaongezeka na kusababisha watu wasitegemee madini ya Tanzanite peke yake,”
alisema Mushi.
Alisema mradi huo ni wa muda mrefu na hatambui
kikwazo kinachokwamisha kuanzishwa kwa mradi huo ambapo wakazi waliokuwa
wanamiliki maeneo ya mradi huo walishakubali kuhama ili kuupisha.
“Jamii ya Mirerani na Simanjiro itanufaika
kiuchumi kupitia EPZA kwani bidhaa na mazao yatakayozalishwa na wakazi hao
ikiwemo madini ya Tanzanite, Tomarini ya kijani,gaineti,mifugo,ngozi yatafanya
wapige hatua,” alisema Mushi.
Alisema ni muda mrefu sasa umepita bila eneo
hilo kuendelezwa wakati ambapo ardhi ya kujengwa EPZA imeshatengwa na mji huo
hivyo kusubiri Serikali kuanza kujenga eneo hilo.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa watu wengi hasa
wanawake wa eneo hilo watanufaika kutokana na mradi huo ambao umekuwa tegemeo
kubwa lakini utekelezaji wake bado haujafanyika.
Alisema watu wamekuwa na maswali mengi kuliko
majibu kuhusiana na mradi huo ambao ni tegemeo kubwa kwao lakini kupitia nafasi
aliyonayo hivi saa atakuwa anawakumbusha viongozi wa Serikali juu ya hatima ya
EPZA Mirerani.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment