Baadhi ya
wajumbe wa mkutano mkuu wa uchaguzi wa Uvccm mkoani Arusha kutoka
wilayani Monduli wakiingia kwa mara ya pili kupiga kura za kumchagua
mwenyekiti wa umoja huo baada ya zoezi la awali kuvurugika jana katika
ukumbi wa CCM mkoa(picha na Mahmoud Ahmad Arusha)
…………………………………………………..
Mahmoud Ahmad Arusha
HALI ya tafrani imeibuka katika
uchaguzi wa jumuiya ya umoja wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi(Uvccm)
mkoa wa Arusha baada ya katibu wa CCM mkoani hapa,Mary Chatanda
kunusurika kipigo baada ya kutuhumiwa kuvuruga uchaguzi huo kwa lengo la
kumpitisha chaguo lake ambaye alitajwa kuwa ni ,Dk Harold Adamson.
Katika vurugu hizo Chatanda
alinusurika kipigo kutoka kwa wajumbe uliotoka wilayani ya Monduli baada
ya kuamuru zoezi la uchaguzi huo lilirudiwe kwa madai kwamba wajumbe
hao pamoja na wale wanaotoka wilayani Meru idadi yao ilikuwa na kasoro.
Katika vurugu hizo makundi ya
baadhi ya vigogo wa CCM hapa nchini yanayohusishwa na waziri mkuu
mstaafu aliyejiuzulu,Edward Lowasa pamoja na Bernad Membe
yalijidhihirisha waziwazi ambapo yalikuwa yakitambiana nje ya ukumbi wa
mkutano.
Hata hivyo,katika hali isiyo ya
kawaida polisi pamoja na maofisa wa usalama wa taifa waliwatimua
waandishi wa habari waliokuwa nje ya ukumbi wa mkutano katika jengo la
CCM mkoani hapa kwa amri ya katibu wa CCM wilaya kwa madai kwamba hawana
mashati yenye rangi ya kijani.
Zoezi la kupiga kura za uchaguzi
wa nafasi ya mwenyekiti wa Uvccm mkoa lilianza majira ya saa 6;00
mchana ambapo upepo wa awali katika uchaguzi huo ulionyesha kwenda kwa
mgombea,Robinson Meitenyiku anayetokea wilayani Arusha.
Vurugu hizo zilianza majira ya
saa 9;00 mchana ambapo Chatanda alipoamuru wajumbe wa mkutano huo watoke
nje ya ukumbi kwa madai kwamba kuna baadhi yao kutoka wilaya za Meru na
Monduli walizidi.
Akitangaza uamuzi huo katibu
huyo alisema kwamba wajumbe kutoka wilayani Monduli idadi yao haikuwa
halali pamoja na ile ya wilayani Meru kwamba wajumbe watano walizidi
kitendo kilichopingwa vikali.
Hata hivyo,mara baada ya wajumbe
hao kutoka nje ya ukumbi wa uchaguzi walianza kupaza sauti kwamba
katibu huyo analengo la kuvuruga uchaguzi huo kwa kuwa anataka
kumpitisha mgombea wa nafasi hiyo,Dk Adamson.
Wakati vurugu hizo zikiendelea
ndipo baadhi ya wajumbe kutoka wilayani Monduli walitishia kumchapa
ndani ya ukumbi huo lakini juhudi zao zilizimwa na baadhi ya walinzi
wakiwemo askari wa jeshi la polisi mkoani Arusha.
Mmoja wa wajumbe hao kutoka
wilayani Monduli,Isaac Kadogoo alimwakia vikali Chatanda ndani ya ukumbi
huo na kumtuhumu kwamba kitendo chake cha kukaa karibu na sanduku la
kura kilikuwa na lengo la kutaka kuchakachua kura hizo.
“Mheshimiwa katibu rudi ukae
meza kuu hata kama wewe ni msimamizi wa uchaguzi huu ondoka hapo kwenye
sanduku la kura tuna wasiwasi na wewe”alisikika Kadogoo
Wakati hayo yakijiri nje ya
ukumbi wa mkutano huo baadhi ya wajumbe walipinga kitendo cha Chatanda
kuwatoa nje na kusema kwamba ana lengo la kuuvuruga uchaguzi huo ili
chaguo lake lipite.
Hata hivyo,ilipotimu
majira ya saa 9;15 mchana ndipo wajumbe hao walitangaziwa kurudi ndani
ya ukumbi huo kwa lengo la kurudia zoezi la kupiga kura na ndipo
walipojipanga kwa mistari na kuelekea katika ukumbi wa uchaguzi kupiga
kura kwa mara nyingine.
Maofisa wa usalama wa taifa
sanjari na askari wa jeshi la polisi mkoani Arusha walikuwa wakiranda
randa nje na ndani ya ukumbi wa mkutano kuimarisha ulinzi wakiwemo na
baadhi ya maofisa wa Takukuru mkoani hapa.
No comments:
Post a Comment